Ndugai awaanika vinara wa utoro Bungeni

Spika wa Bunge, Job Ndugai ametaja orodha ya wabunge na mawaziri ambao ni watoro kwenye vikao vya Bunge na Kamati ambao mahudhurio yao yapo chini zaidi  huku Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Dkt. Augustine Mahiga akiwa na mahudhurio hafifu zaidi wakati kwa upande wa wabunge ni Godbless Lema wa Arusha Mjini.

Spika Ndugai ametangaza mahudhurio hayo Bungeni na kusema suala hilo limetokana na tathmini iliyofanyika kuanzia vikao vya Machi, Agosti na Oktoba mwaka huu.

Katika hatua nyingine aliyekuwa Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea ametangaza uamuzi wa kujiuzulu Ubunge na kujivua nyadhifa zake zote ndani ya Chama Cha Wananchi (CUF) akiwa ndani ya Bunge.

Orodha hiyo iliyotajwa na wabunge inayongozwa na Lema inafuatiwa na Mbunge Suleiman Nchambi wa Jimbo la Kishapu akifuatiwa na Salim Turki ambaye ni Mbunge wa Mpendae wakati kwa mawaziri orodha hiyo inayoongozwa na Dkt. Mahiga  akifuatiwa na January Makamba na Profesa Palamagamba Kabudi.

Kinara wa mahudhuria mazuri Bungeni ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama pamoja na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji.

Zana haramu za uvuvi zateketezwa kwa moto Muleba

Zana haramu za uvuvi zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 124 zilizokamatwa ndani ya Ziwa Victoria kwenye Kisiwa cha Iyumbo kilichoko Kata ya Bumbile wilayani Muleba mkoani Kagera zimeharibiwa kwa kuteketezwa na moto.

Uteketezaji huo ni sehemu ya operesheni Sangara awamu ya tatu inayoendeshwa na kikosi maalumu kinachofanya doria katika Ziwa Victoria.

Akizungumza wa wananchi wa Kisiwa cha Iyumbo baada ya zoezi  hilo la kuteketeza zana hizo haramu, Afisa Mfawidhi wa Ulinzi wa Rasilimali za Uvuvi wa Kanda ya Ziwa Victoria, Didas Mtambalike ametoa onyo kwa wale wote wanaojihusisha na vitendo vya uvuvi haramu.

Aidha, Mtambalike amesema kuwa wamefanikiwa kukamata pia samaki  waliokuwa wakisafirishwa kwenda nchi jirani ya Uganda na kueleza kuwa Serikali itaendelea kutaifisha samaki wanaokamatwa  pamoja na kuharibu vitendea kazi vinavyotumiwa na wavuvi haramu.

Samaki hao waliokamatwa wamegawiwa kwenye  taasisi za serikali na binafsi ambazo ni pamoja na shule za sekondari ambapo Mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi ya Rweikiza, Baraka Mwambinga ambayo ni miongoni mwa shule zilipata mgao wa samaki hao amepongeza juhudi zinazofanywa serikali za kupambana na uvuvi haramu.

Licha ya Vikosi vya doria ya kudhibiti uvuvi haramu katika Ziwa Victoria kufanikiwa katika baadhi ya operesheni zao, vikosi hivyo vimeendelea kuweka kambia katika visiwa kadhaa ndani ya ziwa hilo ili kuhakikisha samaki hawatoroshwi kwenda nje ya nchi kupitia majini.

Prof. Mbarawa avunja mikataba ya wakandarasi wa Lindi na Kigoma

Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa amevunja mikataba ya wakandarasi wawili  wanaotekeleza miradi mikubwa ya maji katika Mkoa wa Lindi na Kigoma  kwa kile kinachodaiwa kuwa wameshindwa kutekeleza miradi hiyo kwa wakati  na kupelekea wananchi  wa maeneo hayo  kutopata huduma ya maji safi na salama kwa muda mrefu kinyume na matarajio.

Waziri mbarawa amesema  miradi hiyo imechukua muda mrefu  kukamilika  ambapo mkandarasi wa Lindi alipaswa kukamilisha mradi huo  Machi 17,  2015  kwa mujibu wa mkataba  huku mkandarasi wa mradi wa Kigoma  naye alipaswa kukamilisha mradi huo Machi 17, 2015  kwa mujibu wa mkataba  lakini hadi sasa wakandarasi hao hawajakalisha miradi hiyo.

Hata hivyo Waziri Mbarawa amesema  pamoja na kuwasimamisha kazi wakandarasi hao Serikali  itaendelea kuchukua hatua za kuwashughulikia  ili iwe fundisho  kwa wakandarasi wengine wenye tabia kama hizo .

Waziri mbarawa amesema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari.

SUMATRA: Madale - Goba sasa kusafiri hadi Posta
Mamlaka ya Udhibiti wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imetangaza njia mpya za Daladala jijini Dar es Salaam.
 
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo, njia hizo ni pamoja na Madale kwenda Posta na Madale kwenda Gerezani kupitia barabara ya Goba hadi Ali Hassan Mwinyi huku magari hayo yakitakiwa kuwa na uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 40.
 
Njia hizo zinaanza rasmi kuanzia tarehe ya tangazo hilo lilipotolewa, Novemba 15, 2018.
Kura Maoni
Je serikali inawakabili ipasavyo wanaofanya mauaji wilaya ya Kibiti?
VOTE
Je serikali inawakabili ipasavyo wanaofanya mauaji wilaya ya Kibiti?
70% Complete
70% Ndiyo30% Hapana