Latest News
ATCL yakanusha madai ya uwepo wa ndege mbovu

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la ndege Tanzania ATCL, Ladislaus Matindi amesema hakuna ndege aina ya bombardier iliyombovu, zote tatu ziko vizuri zinaendelea na kazi ya usafirishaji wa abiri huku  wakisubiri ujio wa ndege kubwa aina ya  Boeing 787 Drimliener itakayowasili nchini kabla ya mwezi Julai mwaka huu.

Kiongozi huyo wa ATCL ameiambia Azam TV katika mahojiano maalumu kuwa, tayari Marubani wawili wameshafuzu kurusha ndege hiyo aina ya Boeing 787 Drimliener huku wengine Wanne wakiwa katika hatua za mwisho   kumaliza masomo yao ambapo wote ni wazawa hivyo  bado hakuna mpango wa kuajiri Marubani wageni na kusisitiza shirika lake limejipanga kuhakikisha linajiendesha kwa faida

Latest News
China na Marekani zaondoa hofu ya vita ya biashara

China imekubali kununua bidhaa na huduma za Marekani zaidi, kwa lengo la kupunguza mgogoro wa usawa wa kibiashara kati ya nchi hizo mbili na hivyo kuondoa hofu ya kuibuka kwa vita ya kibiashara.

Washington wamesema, hatua hiyo itasaidia "kupunguza gharama" ambayo kwa mwaka kibiashara China hupata upungufu wa Dola bilioni 335.

Lakini hata hivyo taarifa hiyo haijaeleza zaidi kuhusu punguzo hilo kubwa litakavyokuwa.

"Pande zote mbili zimekubaliana kwa mantiki  hiyo ya maana ya kuongeza uuzaji wa bidhaa za kilimo na nishati nchini Marekani ," imesema sehemu ya taarifa ya pamoja kati ya Marekani na China baada ya mazungumzo ya siku kadhaa yaliyofanyika nchini Marekani.

"Hali hii itasaidia kukua na kuongeza ajira ndani ya Marekani."

Nchi hizo pia zimekubaliana kuendelea kuyasimamia makubaliano ya biashara kwa lengo la kuondoa wasiwasi wao "kwa maana inayofaa".

Latest News
Spika Ndugai amaliza kiaina sakata la bei ya Sukari

Spika wa Bunge, Job Ndugai ameamua kumaliza sakata  la utofauti wa gharama ya bei ya sukari kati ya Tanzania Bara na Zanzibar ‘kiaina’ baada ya kutoridhishwa na majibu ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji juu ya suala hilo.

Hayo yamebainika Bungeni Jijini Dodoma, leo wakati Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ilipopata fursa ya kujibu swali ambalo liliwekwa kiporo juma lililopita baada ya Spika Ndugai kutoridhishwa na majibu ya Waziri Charles Mwijage na kuiagiza Serikali iandae majibu ya uhakika.

Akijibu maswali hayo Bungeni, Naibu waziri Manyanya amesema, utofauti huo wa bei unatokana na utozaji kodi na tozo za vibali na hivyo kuifanya Zanzibar kuuza Sukari kwa bei ndogo wakati kwa upande wa Bara bei hiyo ikiwaelemea wananchi.

Aidha Naibu waziri huyo alishindwa kunyoosha majibu yake alipoulizwa swali kwa niaba ya Mbunge Jaku lililoulizwa na Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Keissy Mohamed ambaye alitaka kufahamu ni  wafanyabiashara wangapi wanavibali vya kuagiza sukari kutoka Zanzibar.   

Spika alimaliza hivyo lakini bado haijulikani nini suluhisho la tofauti hiyo ya bei ambayo wiki iliyopita Spika Ndugai alisema haikubaliki kulinda viwanda vya ndani huku wananachi wakiumia.

Latest News
BOT yaziunganisha Twiga Bancorp na TPB

Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imetangaza kuunganishwa kwa Benki ya Twiga Bancorp na Benki ya Posta TPB na kuifanya kuwa Benki moja ambapo wateja, wafanyakazi, mali na madeni yote yatahamishiwa kwenye Benki ya Posta ili kuongeza ufanisi wa utendaji.

Utekezaji wa suala hili unaanza rasmi kesho huku BOT ikiwatoa hofu wateja kuwa italinda amana za wateja wote na kutoa kwa Benki binafsi zinazojiendesha chini ya ufanisi kuungana ili kuwa na Benki chache zenye mtaji imara.

BOT imesema hatua ya kuunganisha benki zilizo chini ya Serikali haitaishia hapo bali itaendelea kwa benki zote ambazo zitaonekana mitaji yake inayumba na kuhatarisha uwezo wake wa kujiendesha.

Urasimu wa Tanesco wazuia kuzalishwa kwa 360 MW Rukwa

Wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda nchini wamelitupia lawama shirika la umeme (Tanesco) kwa  kuendekeza urasimu, tendo ambalo linarudisha nyuma juhudi za serikali za kujenga nchi ya viwanda.

“Kampuni yangu Edenville Energy inauwezo wa kuzalisha zaidi ya megawati 360 za umeme mkoani Rukwa. Tumekuwa na majadiliano ya muda mrefu sana na Tanesco bila sababu za msingi… uzalishaji wa umeme umekwama  kutokana na urasimu huo... hivyo basi… ninamuomba mwenyekiti wa baraza hili kuingilia kati,”Kasiano Kaegele, mmiliki wa kampuni ya Edenville energy ametoa kauli hiyo leo Machi 19, 2018 katika mkutano wa 11 wa Baraza la Taifa la Biashara unaofanyika Ikulu Dar es Salaam na kuongozwa na mwenyekiti wa baraza hilo, Rais John Magufuli.

Makamu Mwenyekiti wa Mfuko wa Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Salum Shamte amesema sekta ya umeme inaweza kukwamisha juhudi za uchumi wa viwanda.

Amesema kiwango cha wastani wa kuhudumia umeme kwa kila mtanzania bado kipo chini sana na hakiwezi kufanikisha juhudi hizo.

BOT yatolea ufafanuzi kuhusu anguko la kiuchumi

Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imetoa ufafanuzi kuhusu madai ya kushuka kwa uwekezaji wa Hati fungani na dhamana hadi kufikia asilimia Nne hadi Sita ambao umetajwa kuwa ni anguko la kiuchumi.

Gavana wa BOT, Profesa Florens Luoga ametoa ufafanuzi huo kwa Azam TV  kuhusu madai hayo ambayo yamezua mijadala kwenye mitandao ya kijamii.

Kushuka na kupanda kwa riba za dhamana hutokana na nguvu ya soko, na siyo kwa uamuzi wa Benki Kuu.

Gavana huyo amesema, Dhamana za serikali, hutolewa au huuzwa kwa njia ya mnada ambapo kila mwekezaji anawasilisha zabuni inayoonyesha bei ambayo yuko tayari kulipa kulingana na mahitaji yake.

Benki Kuu ikiwa ni wakala wa serikali, hushindanisha maombi ya wawekezaji kufuatana na kiasi ambacho serikali imepanga kukopa katika mnada husika. Ushindani huu ndiyo unaotoa riba ya soko.

Kushuka kwa riba ya dhamana ni ishara ya kuwepo ukwasi mwingi na hii inaendana na sera ya kujenga mazingira ya kuongeza mikopo kwa sekta binafsi.