ATCL yarejeshwa rasmi IATA, watangaza safari za masafa marefu

|
Miongoni mwa Ndege za Shirika la Ndege la Tanzania ambayo imeanzisha safari zake ndani na nje.

Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), limesema limerejeshwa katika Uanachama wa Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (IATA) baada ya kusimamishwa kwa muda na sasa linaendelea na mipango yake ya kuanza safari za masafa marefu ikiwa ni pamoja na nchi za China na India.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirka hilo, Ladislaus Matindi katika uzinduzi wa ofisi ya mauzo sambamba na tovuti ambayo itawapa uwezo wateja wa ATCL kukata tiketi popote walipo duniani huku tayari safari za Entebe, Uganda, Comoro na Bujumbura, Burundi zikiwa zilishaanza na zitafuatiwa na awamu ya pili ya safari za kwenda Lusaka, Zambia, Harare  na Zimbabwe  kuanzia Februari 22.

Hatua hiyo imekuja baada ya Serikali ya awamu ya tano kudhamiria kulifufua shirika hilo la ATCL, tayari imeshanunua ndege saba ambazo zinasafirisha abiria ndani ya nchi ukiwa ni mkakati wa awamu ya kwanza wa shirika hilo.

Mkurugenzi mtendaji huyo amebainisha kuwa shirika hilo tayari limeshafunguliwa kwenye mfumo wa kimataifa wa IATA na kuanza kutoa huduma za usafiri wa anga kwa nchi jirani kabla ya kuanza safari za masafa marefu huku Mwenyekiti wa Bodi ya ATCL, Mhandisi EMMANUEL KOROSSO amewataka mawakala wa ndani na nje ya nchi kuchangamkia fursa hiyo.

Shirika hilo la ATCL pia limebainisha kuwa katika mpango wake wa miaka mitano hadi kufikia Juni mwaka 2022 litakuwa limejizatiti kuangalia fursa ya biashara katika soko la Uingereza kutokana na uwepo wa watalii wengi kutoka Bara la Ulaya.

Usafiri
Maoni