Benki ya Biashara na Maendeleo kuipatia Tanzania mkopo nafuu

|
Ujumbe wa Serikali ya Tanzania (kulia) ukijadiliani na ujumbe wa Benki ya Biashara na Maendeleo ya Mashariki na Kusini mwa Afrika –TDB (kushoto)

Benki ya Biashara na Maendeleo ya Mashariki na Kusini mwa Afrika (TDB), itaikopesha Tanzania mkopo wenye masharti nafuu wenye thamani ya dola za Marekani milioni 400, sawa na takriban shilingi bilioni 900 kwa ajili ya ujenzi wa Reli ya Kiwango cha Kimataifa (SGR) na Mradi wa kuzalisha umeme wa gesi wa Kilwa.

Hayo yamesemwa Jijini Dar es Salaam na Rais wa Benki hiyo yenye Makao yake Makuu Jijini Nairobi nchini Kenya, Admassu Tadesse alipokutana na kufanya mazungunzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani.

Tadesse amesema kuwa benki yake imetenga kiasi cha dola za Marekani milioni 200 kwaajili ya ujenzi wa reli ya kati ya kisasa pamoja na kiasi kingine kama hicho kwaajili ya ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa gesi wa Kilwa mkoani Lindi.

"Tanzania ni mdau mkubwa wa Benki hii ikiwa inashika nafasi ya 7 kati ya nchi na taasisi 37 zinazomiliki hisa zake ambapo inamiliki hisa asilimia 6.4" alisema Tadesse.

Admassu Adesse amesema kuwa hadi Machi mwaka 2018, benki yake inatekeleza miradi 11 ya maendeleo nchini Tanzania, katika sekta ya kilimo, biashara, huduma za benki na fedha, nishati, ukuzaji miundombinu na viwanda, yenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani 284.6 milioni.

"Tuna miradi mingine iliyoidhinishwa na Benki, inayokadiriwa kufikia dola za Marekani milioni 157 na kiasi kingine cha dola za Marekani milioni 660 ambacho kimepangwa kutolewa kwa Tanzania ili kutekeleza miradi mbalimbali katika sekta za kilimo, biashara, ujenzi, kemikali na petroli pamoja na sekta ya nishati" aliongeza Adesse.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango ameipongeza benki hiyo kwa kuendelea kujiimarisha kimtaji na kiuendeshaji na kwamba Tanzania inapokea kwa mikono miwili ahadi ya Benki hiyo ya kushiriki katika ujenzi wa miradi ya kipaumbele ya Taifa ikiwemo ujenzi wa Reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa (SGR) na Mradi wa kuzalisha umeme wa Kilwa, itakayochochea uchumi wa nchi.

Aliahidi kuwa atahakikisha mazungumzo kuhusu upatikanaji wa mkopo huo nafuu yanakamilika ndani ya kipindi cha miezi mitatu kuanzia sasa ili fedha hizo ziweze kupatikana.

Fedha
Maoni