Binti wa mwasisi wa Huawei akamatwa Canada

|
Binti wa mwasisi wa Kampuni ya Simu ya Huawei ya China, Meng Wanzhou aliyekamatwa nchini Canada na kutakiwa kusafirishwa kwenda Marekani

Binti wa mwasisi wa Kampuni kubwa ya vifaa vya kielektoniki ya China ya Huawei amekamatwa nchini Canada na kukabiliwa na makosa yanayompasa kusafirishwa kwenda nchini Marekani.

Meng Wanzhou, ambaye ni Afisa mkuu wa masuala ya fedha na naibu mwenyekiti alikamatwa mjini Vancouver mwanzoni mwa mwezi huu wa Disemba.

Taarifa zaidi kuhusu kukamatwa kwake bado hazijatolewa rasmi lakini kumekuwepo na madai kuwa Marekani imekuwa ikkiichunga Kampuni hiyo ya Huawei dhidi ya uwezekano wa kukiuka vikwazo ilivyowekewa nchi ya Iran.

Ubalozi wa China nchini Canada umepinga kukamatwa kwake binti huyo wa mwasisi wa Kampuni hiyo ya vifaa vya kielektroniki zikiwemo simu na kutaka aachiwe mara moja.

Huawei kwa upande wao umesema, hauna taarifa nyingi kuhusu kukamatwa kwake na “hawafahamu kuhusu alichofanya hadi kufikia kukamatwa huko, Kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo kumekuja wakati ambapo China na Marekani wako katika kipindi chenye kuhitaji uangalifu mkubwa kuhusu uhusiano wa nchi hizo mbili.

Mataifa hayo mawili kwa muda mrefu yamekuwa katika vita ya kibiashara huku kila upande ukiongeza ushuru wa mabilioni ya dola kwa bidhaa za mwenzake.

Biashara
Maoni