Test
Abiria wa FASTJET wakwama asubuhi, walia na uongozi

Zaidi ya abiria 20 waliokuwa wakisafiri leo, Alhamisi asubuhi kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza kwa ndege ya Kampuni ya Fast Jet, wamekwama kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyeyere wakiwa na tiketi zao mkononi kwa madai kuwa ndege waliyokuwa wasafirie ilikuwa imejaa.

Azam Tv ilishuhudia abiria hao wakiwa wameizonga ofisi za kampuni hiyo kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere wakita kufahamu mustakabali wa safari yao.

Abiria hao wamesema, walikata tiketi za alfajiri lakini baadaye walielezwa kuwa wataondoka jioni ya siku ya leo licha ya kuutaka uongozi uwafafanulie kama abiria watafidiwa vipi kuhusu muda wao na usafiri wa kwenda na kurudi.

Wamesema, wameshangazwa na majibu ya uongozi wa kampuni hiyo ambao licha ya kuwa makosa yaliyotokea ni ya kwao hawajaweza kuonesha kujali wateja wao hao.

Azam imewatafuta viongozi wa juu wa Fast Jet  na kufanikiwa kumpata Afisa Uhusiano na Masoko, Lucy Mbogoro kwa njia ya Simu, ambaye hata hivyo amesema abiria hao wameshindwa kusafiri kutokana na ndege yao jana kupata itilafu na kushindwa kufanya kazi, hivyo abiria wote wa jana wameondoka leo na wengine wachache walikuwa waondoke asubuhi ya leo.

Mahakama Canada wamwachia Meng Wanzhou kwa dhamana

Mahakama ya Canada imemwachia kwa dhamana Afisa wa Kampuni ya Mawasiliano ya Huawei aliyekamatwa kwa maombi ya Marekani katika kesi iliyozusha mgogoro wa kidiplomasia kati ya nchi tatu na kuzidisha ugumu wa mazungumzo ya kibiashara kati ya Marekani na China.

Saa kadhaa kabla ya kusikilizwa kwa dhamana huko Vancouver, Canada, nchi ya China ilimshikilia mwanadiplomasia wa zamani wa Canada huko Beijing kama kulipiza kisasi baada ya kukamatwa kwa raia wao Meng Wanzhou ambaye ni binti wa Mwanzilishi wa Kampuni ya Huawei.

Meng ambaye ni Afisa wa Kifedha wa Huawei alikamatwa Disemba Mosi mwaka huu.

Baada ya siku tatu za majadiliano, mahakama ilimwaachia kwa dhamana ya dola za Canada milioni 10 sawa na dola za Kimarekani milioni 7.5.

Masharti ya dhamana hiyo ni pamoja na Meng kusalimisha pasipoti yake na kusalia huko Vancouver, nchini Canada.

OPEC watafuta njia ya kusaidia kushusha bei ya mafuta

Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Nchi zinazozalisha mafuta duniani (OPEC) zimekutana huko Vienna, Austria  kwenye mkutano wake wa 175 wa jumuiya hiyo safari hii wakilenga kutafuta njia ya kusaidia kushuka kwa bei ya mafuta, huku wataalam wakitabiri kupungua kwa uzalishaji.

Bei ya mafuta ghafi imeelezwa kuanza kushuka tangu mwezi Oktoba mwaka huu huku ikitarajiwa kushuka zaidi  kwa sababu wazalishaji kama Marekani na Saudi Arabia wanazalisha kwa kiasi kikubwa na pia kwa kuhofia nchi zenye ukuaji hafifu wa uchumi zitapunguza uhitaji wa mafuta.

Wataalam wanasema mkutano huo wa OPEC utaipa nguvu bei ya mafuta kwa miezi ijayo.

Mkutano huo wa OPEC unafanyika baada ya Shirika la Taifa la Mafuta la Qatar hivi karibuni kutangaza kujitoa kwenye jumuiya hiyo ifikapo mwezi Januari mwakani kwa madai kuwa uwepo wake kwenye jumuiya hiyo haujawa na faida kwa QATAR kama nchi ambayo huzalisha taktiban mapipa 600,000 kwa siku

Binti wa mwasisi wa Huawei akamatwa Canada

Binti wa mwasisi wa Kampuni kubwa ya vifaa vya kielektoniki ya China ya Huawei amekamatwa nchini Canada na kukabiliwa na makosa yanayompasa kusafirishwa kwenda nchini Marekani.

Meng Wanzhou, ambaye ni Afisa mkuu wa masuala ya fedha na naibu mwenyekiti alikamatwa mjini Vancouver mwanzoni mwa mwezi huu wa Disemba.

Taarifa zaidi kuhusu kukamatwa kwake bado hazijatolewa rasmi lakini kumekuwepo na madai kuwa Marekani imekuwa ikkiichunga Kampuni hiyo ya Huawei dhidi ya uwezekano wa kukiuka vikwazo ilivyowekewa nchi ya Iran.

Ubalozi wa China nchini Canada umepinga kukamatwa kwake binti huyo wa mwasisi wa Kampuni hiyo ya vifaa vya kielektroniki zikiwemo simu na kutaka aachiwe mara moja.

Huawei kwa upande wao umesema, hauna taarifa nyingi kuhusu kukamatwa kwake na “hawafahamu kuhusu alichofanya hadi kufikia kukamatwa huko, Kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo kumekuja wakati ambapo China na Marekani wako katika kipindi chenye kuhitaji uangalifu mkubwa kuhusu uhusiano wa nchi hizo mbili.

Mataifa hayo mawili kwa muda mrefu yamekuwa katika vita ya kibiashara huku kila upande ukiongeza ushuru wa mabilioni ya dola kwa bidhaa za mwenzake.

Tanzania kinara kwa kuvutia wawekezaji Afrika Mashariki

Tanzania imeendelea kuweka rekodi ya kuvutia wawekezaji kwa nchi zilizopo ukanda wa Afrika Mashariki kwa kuwa na mtaji wa uwekezaji wa Dola Bilioni 1.18, ikifuatiwa na Uganda wenye uwekezaji wa dola za kimarekani 700.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu  wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Godffrey Mwambe amesema nchi ya Kenya inashika nafasi ya tatu wakiwa na uwekezaji wa dola za kimarekani 670 na hivyo kuiweka Tanzania kuwa juu ya nchini nyingine Afrika Mashariki.

Mwambe amesema kuwa Tanzania inaongoza kuvutia wawekezaji kutokana na mapinduzi makubwa yaliyofanywa na Serikali ambapo hadi sasa imewekeza jumla ya miradi mipya 905 katika sekta mbalimbali nchini, miradi ambayo itatengeneza ajira 115,055 kwa Watanzania na kuleta tija na manufaa kwa taifa.

Alisema kuwa katika kipindi hiki cha miaka mitatu TIC imeweza kuvutia wawekezaji  na kuweza kuandikisha, mfano kuanzishwa kwa viwanda mbalimbali ambavyo vimeweza kuongeza pato la Taifa.

Akifafanua zaidi amesema kuwa baadhi ya miradi mikubwa zaidi iliyowekezwa nchini ni pamoja na kiwanda cha Goodwill Ceremics Ltd kilichopo Mkuranga mkoani Pwani kinachojihusisha na utegenezaji vigae na kimewekeza jumla ya dola za kimarekani milioni 53, huku kikitoa ajira za moja kwa moja 1,500 kwa watanzania na ajira zisizo za moja kwa moja 3,000.

“Viwanda vingine ambavyo vimeiwezesha Tanzania kuwa kinara wa kuvutia wawekezaji ni KEDA (Twyford) Tanzania ceramic Ltd pia ni cha kutengeneza marumaru na hiki ni kikubwa zaidi kina mtaji wa Dola za kimarekani milioni 56, kimetoa ajira  za moja kwa moja zipatazo 2,000 kwa watanzania na  ajira zisizo za moja kwa moja 4,000” alisema.

Amevitaja Viwanda vingine kuwa ni Sayona Friut Ltd yenye mtaji wa milioni 55, KEDS(T) Co.Limited mtaji wa dola milioni 11.8 pamoja na kiwanda cha nondo cha Kiluwa Steel Group ambacho ni kikubwa kwa ukanda wa Afrika Mashariki kina mtaji wa dola milioni 130 na kinazalisha jumla ya tani 200 za nondo.

Aidha Mwambe alizitaja nchi zinazoongoza kwa kuwekeza nchini Tanzania ni pamoja na Jamhuri ya Watu wa China, Uingereza  na Marekani.

“Maendeleo ya China yaliyopatikana kwa miaka 40 kwa watanzania wote ni funzo kubwa la kuwa na uzalendo, China ndiyo inaongoza kwa kuwekeza nchini tangu miaka ya 1990, na kwa sasa ina miradi ya uwekezaji 723”, Mwambe Mkurugenzi Mkuu, TIC.

Akibainisha utoaji huduma, Mwambe amesema TIC imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika utoaji huduma kwa wateja ndani na nje ya nchi kwani kwa sasa huduma zote zinazomuhusu mwekezaji zinapatika TIC kupitia mfumo wa ‘Huduma za mahala pamoja’ ambapo huduma hii imeongeza wawekezaji kwa kuvutiwa zaidi na kuwezesha Tanzania kuwa kinara katika nchni za Afrika Mashariki.

 “Tumefanikiwa kuongeza Taasisi ambazo hazikuwepo katika huduma za mahala pamoja ndiyo maana tuliwatafuta kwenye maofisi yao na kuwaleta hapo katika Taasisi kama NIDA, OSHA, NEMC, TBS, TFDA pamoja na TANESCO, hawa wamekuja kuimarisha na kuondoa usumbufu kwa wawekezaji  na sasa tunaongelea jambo la kuwa kinara wa kuvutia wawekezaji Afrika  Mashariki” Mwambe.

Wizara ya Utalii yaendelea kujinadi nchini China

Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea na mikutano ya kuvitangaza vivutio vya utalii vya nchini katika miji mitano ya China ambapo moja ya ujumbe wao ni kuwahakikishia watalii wanaotoka nchi hiyo kuanzia mwezi Februari mwakani watakuwa na uhakika wa kuja Tanzania kwa usafiri wa moja kwa moja wa ndege wa Shirika la Ndege la Tanzania.

Hayo yamesemwa na Meneja wa Mauzo na Usambazaji wa Air Tanzania, Edward Nkwabi na Mkurugenzi mwendeshaji wa Bodi ya Utalii Tanzania, Devotha Mdachi wakati wakizungumza na wadau wa utalii wa nchini China katika mkutano uliofanyika jijini Guangzhou.

Wamesema huduma hizo za usafiri wa ndege zitarahisisha azma ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya kuongeza watalii wa China kutoka 30,000 kwa mwaka na kufikia takribani Watalii 60,000  hadi 100,000 kwa mwaka katika kipindi cha miaka miwili ijayo.

Wawakilishi Z'bar wamuomba Bakhresa kujenga viwanda vya kuongeza thamani ya mazao

Kamati ya Baraza la Wawakilishi Fedha, Biashara na Kilimo imezuru Viwanda vya Usindikaji na Uzalishaji wa Vinywaji Baridi vinavyomilikiwa na Mwekezaji mzawa, Said Salim Bakhresa na kumuomba ajenge viwanda vidogo vya kuongeza thamani ili kuokoa mazao ya wakulima.

Kamati hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Dkt. Mwinyihaji Makame imepongeza juhudi zinazofanywa na Kampuni za SSB kwa kuwapa soko wakulima na kulipa kodi kwa Serikali na kuahidi kusaidia kumaliza changamoto zinazozikabili kampuni hizo.

Wajumbe hao wa kamati  wametumia fursa hiyo pia kujifunza na kujionea uzalishaji wa bidhaa zitokanazo na matunda katika Kiwanda cha Mwandege kilichopo Mkurunga Mkoa wa Pwani.