Dkt. Kijaji azitaka benki kushusha riba za mikopo

|
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji akizungumza wakati wa kufungua Tawi la Benki ya Azania, Dodoma

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji amezitaka Benki nchini kushusha viwango vya riba za mikopo ili wananchi wengi wanufaike kiuchumi na huduma za kifedha zinazotolewa na taasisi hizo za fedha nchini.

Ameyasema hayo Jijini Dodoma wakati akifungua rasmi Benki ya Azania, Tawi la Sokoine na kusisitiza kuwa Benki zote nchini hazina budi kushusha riba za mikopo baada ya hivi karibuni Serikali kuchukua hatua madhubuti za kiutawala na kisera ili kuhakikisha riba za mikopo katika soko zinapungua.

Amezitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kutoa mikopo ya muda mfupi kwa benki za biashara, kushusha riba kutoka asilimia 16 hadi 9 na kupunguza kiwango cha chini cha amana kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu na Benki za Biashara kutoka asilimia 10 hadi asilimia 8.

"Tumepunguza kiwango cha chini cha amana kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu na benki za biashara kutoka asilimia 10.0 hadi asilimia 8.0, hatua ambazo zimesaidia kupunguza riba katika soko kutoka wastani wa zaidi ya asilimia 20 hadi asilimia 17" aliongeza Dkt. Kijaji

"kama haya yote yamefanyika, iweje benki ziendelee kutoza riba ya asilimia 17 kwa kisingizio cha kuogopa mikopo chechefu wakati Serikali kupitia Benki Kuu, imeanzisha kanzi data ya kuhifadhi na kutoa taarifa ya wakopaji (Credit Reference Bureau System)" alihoji Dkt. Kijaji

Aidha, Dkt. Kijaji ameelezea kusikitishwa kwake na hatua ya benki hiyo kuwa miongoni mwa benki 5 zilizofungiwa kwa kipindi maalum kushiriki katika kuuza na kununua fedha za kigeni baada ya kukiuka taratibu za biashara hiyo.

" Kisheria, benki zote za biashara zinatakiwa kutoa taarifa Benki Kuu kuhusu miamala ya Soko la Fedha za Kigeni kati ya Mabenki waliyofanya kwa siku lakini Benki yako ni miongoni mwa benki zilizovunja utaratibu huu, hii niaibu!" alisisitiza Dkt. Kijaji "

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Azania, Charles Itembe, amesema Benki yake imeendelea kufanya vizuri katika soko kwa kupata faida na kwamba imejipanga kutoa mikopo na huduma za kifedha kwa wananchi mkoani Dodoma kwa viwango vya juu.

"Benki yetu, mwaka 2017, imetengeneza faida ya shilingi bilioni 1.81 ikilinganishwa na hasara ya Shilingi bilioni 6 iliyoripotiwa Desemba 2016, na imeongeza rasilimali zake kutoka sh. bilioni 338 hadi bilioni 390" alisema Charles Itembe.

Alisema kuwa Benki yake imeongeza kiasi cha mikopo iliyotoa kutoka shilingi bilioni 129 mwaka 2016 hadi shilingi bilioni 187.7  mwaka 2017, sawa na ongezeko la asilimia 10.23 huku akiba za wateja zikiongezeka kutoka shilingi bilioni 236 mwaka 2016 hadi shilingi bilioni 271 mwaka jana.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Azania ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ya Watumishi wa Umma (PSSSF), Eliud Sanga, ameitaka Benki hiyo kutekeleza mkakati wake wa kuanza kutoa mikopo ili kuimarisha Sekta ya ujenzi wa viwanda nchini. 

Fedha
Maoni