Dkt. Shein apongeza kukamilika kwa soko la kisasa Mkoa wa Kaskazini

|
Rais Dkt. Shein akikagua sehemu ya soko la kimataifa baada ya kulizindua huko Mkoa wa Kaskazini

Rais wa Zanzibar, Dkt. Mohamed Shein mapema juma hili, amezindua soko jipya la Kinyasini lililojengwa kupitia Programu ya miundombinu ya masoko, uongezaji thamani na huduma za Kifedha vijijini ili kutatua uhaba ukosefu wa masoko ya kisasa katika Mkoa wa Kaskazini.

Katika uzinduzi huo  Dkt. Shein amesema, soko hilo litawagusa na kuwafikia  watu wenye kipato cha chini kuinuka kiuchumi hususani wale wa vijijini pamoja na wafanyabiashara wengine.

Amesema, faida ya soko hilo pia litazigusa a sasi ndogo za kifedha zinazotoa huduma vijijini,  vyama vya msingi vya Ushirika na asasi za vijijini zinazojishughulisha na usindikaji wa mazao na masoko ya mazao kwa kushirikisha wanawake katika  makundi yote.

“Soko hili litakuwa lenye tija kubwa kwa wananchi wa Zanzibar bila kujali maeneo wanakotoka. Soko hili ni letu sote, lisingeweza kujengwa kila mahali au hewani lazima lingewekwa mahali, hivyo eneo hili la kaskazini lilipata fursa hii, hivyo niwaombe liwe la wananchi wote wa Zanzibar.”Alisema Rais Shein.

Sambamba na hilo Dkt. Shein amesema, kujengwa kwa soko hilo ni matunda ya Muungano na kuwataka wananchi kuuenzi na kuulinda muungano huo.

“Miradi hii inayohusisha Bara ni moja ya mafanikio na matokeo makubwa ya Muungano wetu na hatuna budi kuuenzi,” alisisitiza Dkt.Shein.

Katika hatua nyingine, Rais aliitaka halmashauri husika kuendelea kuweka mikakati mizuri ya kulitunza na kuliendeleza soko hilo ili liweze kuleta tija iliyokusudiwa kwa Wazanzibar wote.

“Niwaombe Halmashauri kuona njia nzuri za kuendeleza kazi hii iliyofanywa na Programu hii na kuhakikisha wananchi wananufaika zaidi kama ilivyokusudiwa hususan kwa wakulima na wavuvi,”alisisitiza  rais Shein.

Kwa Upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama aliwataka wananchi kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kuzingatia mafanikio ya mradi huu ikiwemo kusaidia kupambana na umasikini na kuleta tija.

“Kuwepo kwa soko hili kutasaidia kupambana na umasikini na kuongeza mapato, hivyo washiriki watunze miundombinu hiyo pamoja na kuongeza thamani ili kuleta tija.”Alisema Mhagama .

Biashara
Maoni