Test
Boeing wapunguza uzalishaji wa ndege zake aina ya 737

Kufuatia ajali ya kuanguka kwa ndege za Shirika la Ethiopia na Indonesia, Kampuni ya Boeing imefikia uamuzi wa kupunguza uzalishaji wa ndege zake aina ya 737 iliyofanya vizuri katika mauzo yake.

Kwa mujibu wa taarifa ya Boeing, hatua hiyo ya kupunguza uzalishaji huo umefanyika kutoka uzalishaji wa ndege 52 kwa mwezi  hadi  42 katika kipindi cha katikati ya mwezi Aprili.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa aumuzi huo ni matokeo ya kusikitisha kwa bidhaa ya ndege aina hiyo ya 737 Max – aina ya kisasa iliyosababisha ajali mbili mfululizo.

Ndege hiyo kwa sasa imezuiwa kufanya safari zozote kama sharti mojawapo la kuhakikisha wanatafuta sababu ya ajali hizo zinazodaiwa kutokana na madai ya kuwepo kwa tatizo katika mifumo ya umeme.

 Ndege ya Shirika la Ethiopia aina ya Boeing 737 Max ilipata ajali kwa kuanguka dakika chache baada ya kuruka kutoka Uwanja wa Addis Ababa mwezi Machi, na kuua watu wote 157.

Aidha nayo Ndege ya Shirika la Lion Air ya Indonesia ilipata ajali kwa kuanguka baharini miezi mitano iliyopita muda mfupi baada ya kuruka ikitokea Jakarta na kuua watu wote 189.

Kituo kipya cha mabasi Moshi chazua hofu kwa wafanyabiashara

Ujenzi wa Kituo cha Kipya cha Mabasi  cha Mjini Moshi mkoani Kilimanjaro umeanza huku ukizua hofu kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara ambao ni wapangaji kwenye maduka ya kituo cha sasa .

Hofu hiyo inatokana na ukweli kuwa wateja hao wengi sasa hawatapita tena katika maduka yao na kujinunulia bidhaa badala yake wataelekea katika kituo kipya kinachojengwa katika eneo la Ngangamfumunyi nje kidogo ya viunga vya Manispaa ya Moshi.

Kituo hicho kipya cha mabasi kitakuwa na jengo la kuingia abiria na la kutokea lakini pia kutakuwa na vyumba kwa ajili ya maduka na hoteli na kinatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 28 hadi kukamilika kwake mwaka 2021.

Kwa mujibu wa Msimamizi wa ujenzi huo, Richard Sanga ambaye pia ni mhandisi katika Manispaa ya Moshi, kituo hicho kitakuwa na mwonekano kama mithili ya viwanja vya ndege vya kimataifa.

Wakizungumzia kituo hicho, wakati wafanyabishara wa kituo cha zamani wakielezea hofu zao, wengine wanaona fahari kwa kuwa na kituo bora cha mabasi.

Kituo hicho kipya cha mabasi kinajengwa na fedha za serikali na kinatarajiwa kubadilisha kabisa  mwonekano wa Manispaa ya Moshi mji wa kitalii ulioko katika ukanda wa kaskazini mwa Tanzania ambao tayari umeanza kupiga tambo kudai hadhi ya jiji  ifikapo mwaka 2025.

Manyara walilia kuporomoka kwa bei za nyanya

Wakulima wa nyanya wilayani Babati mkoani Manyara wameeleza masikitiko yao mara baada ya bei ya bidhaa hiyo kuonekana kusuasua sokoni kutokana na uzalishaji kuwa mkubwa jambo lililosababisha zao hilo kuporomoka bei kutoka 65,000 kwa kreti hadi 20,000.

Wakulima hao wamesema kuwepo kwa uzalishaji mwingi wa nyanya katika msimu huu kumepelekea kuathiri sana jitihada zao hususani katika uchumi kutokana na bei hiyo ya nyanya kusuasua sokoni na kusababisha kupata hasara, kinyume na matarajio yao.

Wamesema, mara nyingi hulima kutegemeana na msimu huku wao wakilima kwa kutumia mbegu na kuhudumia kwa gharama kubwa huku katika biashara wakipambania soko na wakulima wa kawaida na waliotumia mbegu za kawaida.

Kwa upande wake, Mtaalamu wa Kilimo kutoka TAHA amesema wakulima ni lazima wajue kalenda ya kilimo na namna ya kwenda na wakati  kwa kuangalia uhitaji wa bidhaa husika ili kuepusha zao moja kulimwa kwa wingi.

Wakulima wanashauriwa kufuata kanuni na kalenda ya kilimo bora ili kuepuka changamoto zinazoweza kuzuilika.

Watanzania wahamasishwa kulima karanga miti

Watanzania wamehamasishwa kulima kilimo cha zao la Karanga Miti lililoanza kuzalishwa wilayani Mbozi mkoani Songwe na mahitaji yake katika soko la dunia bado ni makubwa.

Kilimo hicho cha makademia  ama karanga miti kinalimwa kwa wingi katika nchi za Afrika Kusini na Kenya sasa kimeingia nchini Tanzania ili kupata matokeo ya haraka ambapo inashauriwa kufanya upandikizaji badala ya kutumia mbegu kama inavyoshauriwa na mtaalamu.

Tofauti ya kilimo cha karanga miti na karanga za kawaida karanga hizi zinaota juu ya miti kama matunda.

Mkurugenzi mtendaji wa shamba la Lima lililopo katika Kata ya Nyimbili wilayani Mbozi,  Tinson Nzunda ambaye pia ndiye mzalishaji mkubwa wa mbegu za karanga hizo nchini, amesema zao la karanga miti ni vyema likawa la kimkakati.

Karanga hizo miti ambazo zikiwa tayari yaani zikishabanguliwa zinafaa kuliwa kama chakula cha kawaida na  katika soko karanga hizo zinauzwa shilingi 40,000 kwa kilo huku karanga ambazo hazijabanguliwa zikiuzwa shilingi 24,000 mpaka 10,000 kwa kilo moja.

Kampuni ya Huawei yaishtaki Serikali ya Marekani

Kampuni kubwa ya vifaa vya kielektroniki ya China, Huawei leo, Alhamisi imefungua mashitaka dhidi ya Serikali ya Marekani kupinga sheria ya nchi hiyo ambayo inazizuia kampuni nchini humo kununua bidhaa zake.

Huawei imesema kesi hiyo imefunguliwa katika Mahakama ya wilaya huko Plano, Texas ikipinga kuwa sheria hiyo ya Marekani ya masuala ya ulinzi ya mwaka 2019 inayozuia mashirika ya serikali kununua vifaa vyake au kushirikiana na wateja wa Kampuni ya Huawei inakiuka katiba.

Hatua hiyo inatuma ishara duniani kwamba Kampuni ya Huawei imedhamiria kutumia kila njia, zikiwemo mahakama za kitaifa, kupinga kuondolewa katika mbio za kuwania soko la mawasiliano ya simu ya 5G, ambayo ni mawasiliano ya spidi ya juu ya simu.

Mwenyekiti wa Kampuni ya Huawei, Guo Ping amesema Marekani mara kwa mara imeshindwa kutoa ushahidi kuhusu madai yake ya kuzuia bidhaa za Huawei, jambo ambalo amesema limeilazimu kampuni hiyo kuchukua hatua za kisheria kwa kuisababishia hasara kampuni hiyo.

Marekani kwa muda mrefu imeichukulia kampuni ya Huawei kama tishio kutokana na historia nyuma ya mwanzilishi wake, Ren Zhengfei, ambaye alikuwa mhandisi wa zamani katika jeshi la China.

Wasiwasi huo umechochea Huawei kuwa kinara duniani wa mtandao wa vifaa vya simu na moja ya kampuni inayoongoza kwa simu za kisasa ikishindana na Kampuni za Samsung na Apple.

Kwa upande wa Serikali ya China, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo, Lu Kang ameichambua Sheria ya Marekani ya mwaka 2019 iliyopitishwa na Baraza la Congress inayozuia shughuli za kibiashara za Kampuni ya Huawei nchini humo na kwingineko na pia hatua ya Huawei kwenda mahakamani kutafuta haki yake ya kibiashara.

Sheria iliyopitishwa hivi karibuni na Serikali ya China ambayo inazitaka kampuni za China kuisaidia serikali katika masuala ya usalama wa taifa kumeongeza wasiwasi huu.

Wanajeshi Kenya wahudumu wasafiri walikwama JKIA, Kenya

Wanajeshi wa nchini Kenya wamechukua jukumu la kutoa huduma katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta kwa lengo la kukabiliana na usumbufu uliojitokeza leo kufuatia  mgomo wa wafanyakazi ulioanza mapema leo Jumatano.

Tangu asubuhi maelfu ya abiria wamejikuta wakikwama kuendelea na safari zao huku baadhi ya ndege zikielekezwa kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam na ndege nyingine zikifuta safari zake.

Mgomo huo unatokana na wafanyakazi hao kupinga mpango wa kuunganisha mamlaka ya usimamizi wa viwanja vya ndege (KAA) na Shirika la Ndege la Taifa (Kenya Airway).

Uwanja huo kwa siku hudaiwa kuhudumia ndege za abiria 120 na kwa leo kwa mujibu wa BBC, walipozungumza na Afisa mkuu Mtendaji wa KQ, Sebastian Mikos takribani  safari 24 za ndege zimeathirika kutokana na mgomo huo.

''Tumekuwa tukiwasiliana na wafanyakazi wote wa KAA tangu saa kumi asubuhi, kwa kweli ni shughuli katika Uwanja wa JKIA na viwanja vingine nchini zimeathirika kutokana na mgomo huo kwa wakati huu tutasema kwamba safari za ndege zimechelewa... safari za ndege 24 zimeathirika'' alisema  Mikos alipozungumza na BBC.

Watanzania watakiwa kuchangamkia fursa ya maparachichi

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amewataka watanzania, hususan vijana kuchangamkia fursa ya kilimo cha parachichi kwa kuwa zao hilo lina thamani kubwa na soko la uhakika.

Dkt. Mpango, ametoa wito huo wilayani Hai mkoani Kilimanjaro alipokutana na wadau mbalimbali wanaojihusisha na kilimo cha kahawa wakiwemo wawekezaji wa zao la kahawa na parachichi.

Amesema kuwa zao hilo lililopewa jina la dhahabu ya kijani, mtaji wake wa uwekezaji ni mdogo lakini baada ya miaka mitatu mkulima anaweza kupata faida kubwa kupindukia.

Naye Waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia uwekezaji, Angela Kairuki amesema kuwa Serikali kwa upande wake imejipanga kuvutia wawekezaji wengi hususan katika kilimo ambacho kinategemewa na wananchi wengi nchini na yeye akatoa wito kwa watanzania kuikimbilia fursa hiyo ya kilimo cha parachichi.