Kampuni ya Huawei yaishtaki Serikali ya Marekani

|
Kampuni ya Huawei iliyoishtaki serikali ya Marekani kwa kuweka zuio la biashara zao

Kampuni kubwa ya vifaa vya kielektroniki ya China, Huawei leo, Alhamisi imefungua mashitaka dhidi ya Serikali ya Marekani kupinga sheria ya nchi hiyo ambayo inazizuia kampuni nchini humo kununua bidhaa zake.

Huawei imesema kesi hiyo imefunguliwa katika Mahakama ya wilaya huko Plano, Texas ikipinga kuwa sheria hiyo ya Marekani ya masuala ya ulinzi ya mwaka 2019 inayozuia mashirika ya serikali kununua vifaa vyake au kushirikiana na wateja wa Kampuni ya Huawei inakiuka katiba.

Hatua hiyo inatuma ishara duniani kwamba Kampuni ya Huawei imedhamiria kutumia kila njia, zikiwemo mahakama za kitaifa, kupinga kuondolewa katika mbio za kuwania soko la mawasiliano ya simu ya 5G, ambayo ni mawasiliano ya spidi ya juu ya simu.

Mwenyekiti wa Kampuni ya Huawei, Guo Ping amesema Marekani mara kwa mara imeshindwa kutoa ushahidi kuhusu madai yake ya kuzuia bidhaa za Huawei, jambo ambalo amesema limeilazimu kampuni hiyo kuchukua hatua za kisheria kwa kuisababishia hasara kampuni hiyo.

Marekani kwa muda mrefu imeichukulia kampuni ya Huawei kama tishio kutokana na historia nyuma ya mwanzilishi wake, Ren Zhengfei, ambaye alikuwa mhandisi wa zamani katika jeshi la China.

Wasiwasi huo umechochea Huawei kuwa kinara duniani wa mtandao wa vifaa vya simu na moja ya kampuni inayoongoza kwa simu za kisasa ikishindana na Kampuni za Samsung na Apple.

Kwa upande wa Serikali ya China, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo, Lu Kang ameichambua Sheria ya Marekani ya mwaka 2019 iliyopitishwa na Baraza la Congress inayozuia shughuli za kibiashara za Kampuni ya Huawei nchini humo na kwingineko na pia hatua ya Huawei kwenda mahakamani kutafuta haki yake ya kibiashara.

Sheria iliyopitishwa hivi karibuni na Serikali ya China ambayo inazitaka kampuni za China kuisaidia serikali katika masuala ya usalama wa taifa kumeongeza wasiwasi huu.

Biashara
Maoni