Karatu wajipanga kutumia vitunguu kuimarisha uchumi wao

|
Zao la Vitunguu linalotarajiwa kuimarisha uchumi wa Karatu

Halmashauri ya Wilaya ya Karatu imeanza Mkakati wake wa kuhakikisha inatumia zao la Vitunguu kukuza pato na kuimarisha uchumi wa eneo hilo kwa ajili ya maendeleo ya watu na kukuza miradi na huduma za kijamii kwenye eneo hilo.

Zao la vitunguu wilayani Karatu huzalishwa katika Bonde la Kilimo cha Umwagilaji la Eyasi kwenye eneo la Mang'ola ambapo kwa kutambua umuhimu na uhitaji wa zao hilo ndani na nje ya nchi, Wilaya ya Karatu imetaja kuwa na mkakati madhubuti wa kujenga Soko Maalumu kwa ajili ya wakulima na wafanyabiashara wa zao hilo.

Mpango huo unatajwa kuwa na shabaha ya kukuza myororo wa thamani katika zao hilo ambalo husafirishwa kwa wingi katika nchi mbalimbali ikiwemo Sudani ya kusini.

Pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Karatu kuweka mipango hiyo, Sekta ya Utalii imeendelea kuwa nguzo muhimu ya mapato ya ndani ya wilaya hiyo na taarifa zinaeleza kuwa ukusanyaji wa mapato umesaidia mno kuboresha huduma za kijamii.

Karatu ni miongoni mwa wilaya sita za mkoani Arusha ambayo ni lango Kuu la kuingilia katika Hifadhi za Serengeti na Ngorongoro na hali hiyo inatajwa kusisimua zaidi uchumi wa eneo hilo.

Kilimo
Maoni