Kituo kipya cha mabasi Moshi chazua hofu kwa wafanyabiashara

|
Kituo cha mabasi cha sasa mjini Moshi ambacho kinakwenda kupata mbadala

Ujenzi wa Kituo cha Kipya cha Mabasi  cha Mjini Moshi mkoani Kilimanjaro umeanza huku ukizua hofu kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara ambao ni wapangaji kwenye maduka ya kituo cha sasa .

Hofu hiyo inatokana na ukweli kuwa wateja hao wengi sasa hawatapita tena katika maduka yao na kujinunulia bidhaa badala yake wataelekea katika kituo kipya kinachojengwa katika eneo la Ngangamfumunyi nje kidogo ya viunga vya Manispaa ya Moshi.

Kituo hicho kipya cha mabasi kitakuwa na jengo la kuingia abiria na la kutokea lakini pia kutakuwa na vyumba kwa ajili ya maduka na hoteli na kinatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 28 hadi kukamilika kwake mwaka 2021.

Kwa mujibu wa Msimamizi wa ujenzi huo, Richard Sanga ambaye pia ni mhandisi katika Manispaa ya Moshi, kituo hicho kitakuwa na mwonekano kama mithili ya viwanja vya ndege vya kimataifa.

Wakizungumzia kituo hicho, wakati wafanyabishara wa kituo cha zamani wakielezea hofu zao, wengine wanaona fahari kwa kuwa na kituo bora cha mabasi.

Kituo hicho kipya cha mabasi kinajengwa na fedha za serikali na kinatarajiwa kubadilisha kabisa  mwonekano wa Manispaa ya Moshi mji wa kitalii ulioko katika ukanda wa kaskazini mwa Tanzania ambao tayari umeanza kupiga tambo kudai hadhi ya jiji  ifikapo mwaka 2025.

Biashara
Maoni