Test
Wawakilishi Z'bar wamuomba Bakhresa kujenga viwanda vya kuongeza thamani ya mazao

Kamati ya Baraza la Wawakilishi Fedha, Biashara na Kilimo imezuru Viwanda vya Usindikaji na Uzalishaji wa Vinywaji Baridi vinavyomilikiwa na Mwekezaji mzawa, Said Salim Bakhresa na kumuomba ajenge viwanda vidogo vya kuongeza thamani ili kuokoa mazao ya wakulima.

Kamati hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Dkt. Mwinyihaji Makame imepongeza juhudi zinazofanywa na Kampuni za SSB kwa kuwapa soko wakulima na kulipa kodi kwa Serikali na kuahidi kusaidia kumaliza changamoto zinazozikabili kampuni hizo.

Wajumbe hao wa kamati  wametumia fursa hiyo pia kujifunza na kujionea uzalishaji wa bidhaa zitokanazo na matunda katika Kiwanda cha Mwandege kilichopo Mkurunga Mkoa wa Pwani.

Muswada wa sheria ndogo za fedha wawasilishwa bungeni

Serikali imewasilisha  muswada wa Sheria ndogo za Fedha wa Mwaka 2018 Bungeni kupita hati ya dharura ikiwa ni mkakati wa kutambua Sekta hiyo ili kuhakikisha kunakuwepo na usimamizi na udhibiti wa biashara za huduma ndogo za Fedha.

Muswada huo umewasilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip mpango ambaye amesema kwa sasa zaidi ya wananchi Milioni 15.4 sawa na  asilimia 55.3 wanatumia huduma hizo za fedha.

Amesema  sababu za kupeleka Muswada huo kupitia hati ya dharula ni  kutaka kulinda na kuboresha utoaji wa huduma ndogo za fedha  kwa kuweka masharti ya usimamizi ya udhibiti wa biashara za huduma ndogo za Fedha ikiwemo utaratibu wa kusajili na kutoa leseni kwa huduma hizo.

Mamlaka ya Mbolea yataja bei elekezi msimu mpya 2018/19

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Nchini (TFRA) imesema mbolea iliyopo nchini kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2018/19 ni wastani wa asilimia 82 ya mahitaji yote ya mbolea yanayohitajika na wakulima wa mazao mbalimbali nchini.

TFRA pia imetangaza bei elekezi kwa mbolea ambapo mfuko wa kilo 50 kwa mbolea ya kupandia kuwa utauzwa kwa Shilingi 56,000 wakati mbolea ya kukuzia kwa mfuko itauzwa kwa 48,000.

Aidha katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, TFRA imesema msimu mpya wa kilimo kwenye maeneo mengine nchini hususan Nyanda za juu Kusini umeshaanza kwa maandalizi ambapo wakulima kwa sasa wapo kwenye hatua za maandalizi za mashamba.

Akizungumzia hali hiyo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Lazaro Kitandu amesema bei elekezi ambazo zimetolewa huenda zikabadilika kulingana na maeneo inapopelekwa mbolea.

TFRA imeeleza kwamba mahitaji ya mbolea kwa msimu wa kilimo wa 2018/19 yameongezeka kwa asilimia 14 ukilinganisha na mahitaji halisi ya mbolea kwa mwaka wa kilimo 2017/18 ambapo Tani 450,000 ndiyo zilikuwa zinahitajika.

Wajasiriamali Dar watakiwa kuchangamkia fursa zinazojitokeza

Wajasiriamali wadogo jijini Dar es Salaam wametakiwa kuchangamkia fursa mbalimbali zinazojitokeza zikiwemo za mikopo itakayowasaidia kuendesha shughuli zao za kiuchumi.

Rai hiyo imetolewa leo, Jumamosi Novemba 10 na Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita katika mkutano wake na baadhi ya wajasiriamali ambao wamelalamikia taratibu za usajili kwenye shughuli zao.

Meya Mwita amesema, mara kadhaa amekutana na changamoto za wajasiriamali hao na kubaini kuwa, wengi wao hawajajitambua na hivyo kupitwa na fursa nyingi ambazo zinaenda kuchangamkiwa na watu wengine.

Serikali yakichukua rasmi kiwanda cha Korosho Lindi

Serikali imekitwaa Kiwanda cha Kuchakata Korosho Lindi maarufu kama BUKO kilichojengwa mwaka 1978 na kufanya uzalishaji kwa kipindi cha miaka nane tu kikiwa na uwezo wa kuzalisha tani 10,000 kwa mwaka huku lengo likiwa ni kufikia tani 60,000 kwa mwaka.

“Hii ni sehemu tu ya utekelezaji wa kasi na Sera ya urejeshaji viwanda vilivyobinafsishwa au kuuzwa na Serikali miaka ya nyuma na kubainika kutofanya kazi,” amesem Kaimu Msajili wa Hazina (TR) Peter Gwagilo katika kikao cha awali na Sekretarieti ya Mkoa wa Lindi.

Gwagilo amewasihi wawekezaji walioingia mikataba ya uwekezaji na Serikali kutekeleza kama mikataba inavyoainisha kwani zoezi la urejeshaji viwanda hivi bado ni endelevu na Serikali inaendelea na taratibu zinazotakiwa katika kupata wawekezaji wengine wenye uwezo, tija na nia madhubuti ya kuwekeza.

AfDB yaunga mkono Afrika kuvutia uwekezaji

Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Akinwumi Adesina amesema mashirika ya fedha yanaunga mkono Afrika wakati Bara hilo linajaribu kuvutia uwekezaji na kukabiliana na changamoto zilizopo kuhusu miundombinu.

Adesina ameyasema hayo kwenye kongamano la uwekezaji barani Afrika lililofanyika mjini Johannesburg, Afrika Kusini.

Amesema kuwa Afrika ina maliasili nyingi, kama vile madini, mafuta na kilimo na kuhimiza uwezo wa Afrika katika kukabiliana na changamoto za miundombinu.

“ Mashirika ya fedha yanaunga mkono Afrika, kuwa sehemu inayoweza kuwekezwa”.

Tanga wahimizwa kushuhudia maonesho ya ujasiriamali wa ndani

Wakazi wa Mkoa wa Tanga wametakiwa kujitokeza kwa wingi kwenye viwanja vya Tangamano ili wajifunze ujasiriamali kwa kujionea bidhaa zilizotengenezwa na wajasiriamali wa mkoa huo na wa nje ya mkoa.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa MKoa wa Tanga, Martin Shigela alipotembelea viwanja vya Tangamano na kujionea bidhaa mbalimbali zilizotengenezwa na wajasiriamali wa ndani.

Maonesho hayo ambayo yameandaliwa na Kikundi cha kina mama cha Anzia Sokoni Women Group na kupewa jina la karibu Tanga Faire,  yanalengo la kutangaza vivutio na fursa mbalimbali zilizopo katika mkoa huo ikiwemo ujenzi wa bomba la mafuta.

Baadhi ya wajasiliamali waliojitokeza kwenye maonyesho hayo wameomba kuwezwa katika kumaliza changamoto zinazowakabili huku Habibu  Issa  ambaye ni mfugaji wa sungura akiwataka vijana wenzake kujishughulisha na mradi wa ufugaji wa Sungura  kutokana na faida zake kuwa kubwa.

Maonesho hayo  yameanza tangu Oktoba 28  na yanashirikisha wajasiriamali kutoka nje na ndani ya Tanzania.