Test
Bidhaa bandia zazisababishia upotevu mkubwa wa fedha nchi za EAC

Ukanda wa Afrika Mashariki umekuwa ukipoteza dola za kimarekani takribani shilingi milioni 500 kila mwaka kutokana na uingizwaji wa bidhaa bandia katika nyanja mbalimbali ikiwepo vifaa vya umeme, mbolea, mbegu pamoja na vifaa tiba na dawa.

Hayo yamebanishwa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa alipofungua mafunzo ya kuwajengea uwezo wakuu wa uchunguzi wa makosa ya jinai kuhusiana na udhibiti wa bidhaa bandia yaliyotolewa na Tume ya Ushindani ambapo amesema ili kuweza kufikia ushindani huo kunahitaji zaidi uzalendo ili wapelelezi hao waweze kuwabaini waingiza wa bidhaa hizo na wapi zinapotengenezwa.

Magdalena Utouh ambaye ni Mkaguzi Mkuu wa Sheria za Alama za Bidhaa kutoka Tume ya Ushindani amesema ni jukumu la Jeshi la Polisi kuchunguza na kuendesha mashtaka dhidi ya makosa yanayohusiana na bidhaa bandia.

Ameongeza kuwa ili kufanikisha hilo ni lazima Polisi nchini wajengewe uwezo nna sasa ni muafaka na muhimu huku Mkuu wa Mafunzo wa Jeshi la Polisi DCP Ally Lugendo akisema biashara ya bidhaa bandia ni makosa ya jinai ambayo yanahusiana kwa kiasi kikubwa na makosa ya kifedha.

Katika kufikia azma ya Tanzania ya viwanda, uchumi wa viwanda vya kati kumebainika kuwa uwepo wa bidhaa bandia sokoni ni kikwazo kwa ukuaji wa viwanda na kuikosesha Serikali mapato.

Halmashauri 12 zawezeshwa kutekeleza miradi ya kimakakati

Serikali, kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, imezipatia halmashauri 12 nchini ruzuku ya shilingi bilioni 137 kwa ajili ya kutekeleza miradi 15 ya kimkakati  yenye lengo la kuhakikisha halmashauri zinaongeza mapato ya ndani  na kupunguza utegemezi wa kibajeti kutoka Serikali Kuu.

Hafla ya uwekaji wa saini mikataba ya ruzuku hiyo umefanyika Jijini Dodoma kati ya Katibu Mkuu na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Doto James na wakurugenzi wa halmashauri huku ikishuhudiwa na Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI, Dkt. Doroth Gwajina na baadhi ya makatibu Tawala wa Mikoa ambao halmashauri zao zimepata ruzuku hiyo.

Katibu Mkuu, Doto James amezitaka halmashauri  zilizopata fedha hizo kutumia fedha kwa malengo yaliyokusudiwa na kuonya kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa watendaji watakaokiuka makubaliano yaliyomo kwenye mkataba wa makubaliano.

"Maafisa masuuli mhakikishe mnafuata na kuzingatia Sheria ya Bajeti Namba 11 ya Mwaka 2015 na Kanuni zake, ambayo pamoja na mambo mengine inasisitiza juu ya matumizi bora ya fedha kwa shughuli zilizoidhinishwa," alisisitiza James.

Amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, ilipoanzisha utaratibu huu haikuwa inatania wala kufanya mazingaombwe, inayodhamira ya dhati ya kuzijengea uwezo halmashauri zijitegemee kiuchumi na kutoa huduma bora kwa wananchi badala ya kutegemea ruzuku ya Serikali Kuu na kuwahakikishia wadau kuwa fedha hizo zipo na kuzitaka halmashauri zichangamkie fursa hiyo kikamilifu.

Miradi inayotarajiwa kutekelezwa inahusisha masoko ya kisasa, kiwanda cha kusindika korosho, uendelezaji wa fukwe ya Oysterbay pamoja na maegesho ya malori, iliyopo katika halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Kigamboni, Tanga, Kibaha, Bagamoyo, Mwanza, Tarime, Hanang, Iringa na Biharamulo.

Kwa upande wake Kamishna wa Bajeti wa Wizara ya Fedha na Mipango, Mary Maganga amesema Awamu ya Pili ya Miradi ya Kimkakati kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa miradi iliyokidhi vigezo ni  15 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 137.38.

Amesema kuwa katika awamu ya Kwanza ya Mpango huo wa Serikali wa kuzijengea uwezo halmashauri kutekeleza miradi ya kimkakati kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019, Halmashauri 17 zenye miradi 22 zilifuzu vigezo na kupatiwa ruzuku ya shilingi bilioni 131 hivyo kufanya miradi yote mpaka sasa kufikia 37 ikiwa na thamani ya shilingi bilioni 268.38

Naye Naibu Katibu Mkuu, kutoka Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-TAMISEMI, Dkt. Doroth Gwajima, ameipongeza Wizara ya Fedha na Mipango kwa kufanikisha upatikanaji wa fedha ambazo zitachochea miradi ya maendeleo katika Halmashauri nchini.

Dkt. Gwajima, amezitaka Halmashauri zilizofanikiwa kusaini mikataba hiyo, kuhakikisha kuwa zinazingatia lengo la mkataba huo na kutekeleza miradi kwa muda mwafaka na viwango vilivyoainishwa na kwamba ufuatiliaji wa miradi hiyo utakuwa ni wa kiwango cha juu.

ATCL yarejeshwa rasmi IATA, watangaza safari za masafa marefu

Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), limesema limerejeshwa katika Uanachama wa Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (IATA) baada ya kusimamishwa kwa muda na sasa linaendelea na mipango yake ya kuanza safari za masafa marefu ikiwa ni pamoja na nchi za China na India.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirka hilo, Ladislaus Matindi katika uzinduzi wa ofisi ya mauzo sambamba na tovuti ambayo itawapa uwezo wateja wa ATCL kukata tiketi popote walipo duniani huku tayari safari za Entebe, Uganda, Comoro na Bujumbura, Burundi zikiwa zilishaanza na zitafuatiwa na awamu ya pili ya safari za kwenda Lusaka, Zambia, Harare  na Zimbabwe  kuanzia Februari 22.

Hatua hiyo imekuja baada ya Serikali ya awamu ya tano kudhamiria kulifufua shirika hilo la ATCL, tayari imeshanunua ndege saba ambazo zinasafirisha abiria ndani ya nchi ukiwa ni mkakati wa awamu ya kwanza wa shirika hilo.

Mkurugenzi mtendaji huyo amebainisha kuwa shirika hilo tayari limeshafunguliwa kwenye mfumo wa kimataifa wa IATA na kuanza kutoa huduma za usafiri wa anga kwa nchi jirani kabla ya kuanza safari za masafa marefu huku Mwenyekiti wa Bodi ya ATCL, Mhandisi EMMANUEL KOROSSO amewataka mawakala wa ndani na nje ya nchi kuchangamkia fursa hiyo.

Shirika hilo la ATCL pia limebainisha kuwa katika mpango wake wa miaka mitano hadi kufikia Juni mwaka 2022 litakuwa limejizatiti kuangalia fursa ya biashara katika soko la Uingereza kutokana na uwepo wa watalii wengi kutoka Bara la Ulaya.

Utafiti: Magari yasiyotumia funguo hatarini zaidi kuibwa na wadukuzi

Utafiti mpya umebaini kuwa mamia ya magari maarufu duniani ikiwemo aina nne kati ya tano zinazouzwa zaidi nchini Uingereza yameripotiwa kuwa katika mashaka ya kiusalama hususani kuibwa.

Magari hayo ambayo hayatumii funguo na badala yake hutumia kitufe maalum cha kuwashia gari na kuzimia ambavyo kwa pamoja na kufunga na kufungua milango ya gari hutumia teknolojia maalum yametajwa kuwindwa zaidi na wataalamu wa mambo ya teknolojia maarufu kama “wadukuzi”.

Kwa mujibu wa utafiti huo uliofanywa na chama cha watumiaji magari cha Which? Umesema kwa mujibu wa taarifa za chama cha kutoa msaada wa magari barabarani cha General German Automobile Club (ADAC) magari ya Ford Fiesta, Volkswagen Golf, Nissan Qashqai na Ford Focus yako kwenye hatari kubwa zaidi.

Wezi wanatajwa kutumia teknolojia za juu zaidi kuweka kuvuka kikwazo cha usalama wa magari hayo hivyo kuongeza uwezekano wa magari hayo kuwa katika hatari ya kuibwa.

Hata hivyo utafiti huo umepingwa na chama cha watengeneza magari na wauzaji cha Society of Motor Manufacturers & Traders (SMMT) kilichosema "magari mapya yako salama zaidi kuliko wakati wowote ule".

ADAC imesema imeyafanyia majaribio magari 237 yasiyotumia funguo na kuyakuta salama isipokuwa magari matatu tu ndio yalikuwa na mashaka ya kiusalama.

Matoleo mapya ya magari ya Discovery na Range Rover, na toleo la mwaka 2018 la Jaguar i-Pace, ambayo yote yanatengenezwa na kampuni ya Jaguar Land Rover yamekutwa salama.

BoT: Sisi tuko tayari kununua dhahabu za wachimbaji nchini

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema iko tayari kununua dhahabu moja kwa moja kutoka kwa wachimbaji kwa sababu tangu zamani walikuwa wakifanya hivyo.

Hayo yamesemwa leo na Naibu Gavana wa BoT, Dkt. Bernard Kibesse wakati wa mkutano mkuu wa Kisekta wa Madini uliolenga kujadili changamoto za wachimbaji wa madini nchini ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Rais John Magufuli ulifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa JNIC, jijini Dar es Salaam.

Naibu Gavana huyo amesema, kilichotokea awali Benki hiyo ilikuwa ikiweka akiba ya Taifa bidhaa hiyo yenye thamani duniani, lakini kutokana na kukosekana kwa uaminifu kati ya wauzaji na baadhi ya watumishi BoT ilijikutana ikipata hasara baada ya kununua dhahabu zisizo na ubora wa kiwango.

Amesema kufanya hivyo ni moja ya utunzaji wa fedha ukiachana na ile ya utunzaji wa dola za Marekani.

“Tuko tayari kununua dhahabu ambayo tayari iko ‘refined’ (chakatwa) kwa sababu ndiyo kiwango ambacho kinakubalika kimataifa na nimefurahi kusikia kuwa kuna watu wana mitambo ya kufanya hivyo na tayari mchakato wa kuwezesha hilo imeshaanza kwa ushirikiano na wizara ya madini na TRA,” amesema Dkt. Kibesse 

Amesema kinachofanyika kwa sasa ni majadiliano kati ya BoT, wizara ya madini na tume ya madini katika uanzishwaji wa kituo cha kuuzia dhahabu ili kuondoa kilio cha kukosekana soko.

“Benki kuu tumeandaa sehemu ya kuhifadhi madini ndani ya utaratibu maalumu ambazo tutakubaliana kuwa ni lazima dhahabu inayokuwa pale iwe na mpangilio wake wa uhifadhiwaji.” alisema Dkt. Bernard Kibesse. 

“Kwa mfano mnunuzi hajapatikana hiyo dhahabu hairuhusiwi kukaa hapo zaidi ya siku tano na badala yake ipelekwe Center’.” alisema Kibesse. 

Mauzo DSE yashuka kwa mwaka jana

Biashara katika Soko la Hisa la Dar Es Salaam DSE imeshuka katika kipindi cha mwaka 2018 ukilinganisha na ilivyokuwa mwaka 2017 ambapo ukwasi uliokusanywa kwa mwaka 2018 ulikuwa ni Shilingi Trilioni 1.2 ikiwa na utofauti kwenye hati fungani na hisa.

Mwaka 2018 hisa zilipungua na hati fungani zikaongezeka huku ukubwa wa soko ukishuka kwa bilioni 700 kutokana na baadhi ya bei ya hisa za makampuni kupungua sokoni.

Afisa Mtendaji Mkuu wa DSE, Moremi Marwa amewaambia wanahabari Jijini Dar Es Salaam kushuka huko ni kwa hali ya kawaida na imetokea katika masoko yote ya Afrika na ni kutokana na wawekezaji kuwekeza katika masoko makubwa ya nje ya Ulaya na Marekani.

Ndege ndefu zaidi duniani kuanza kutengenezwa

Kampuni inayotaka kuunda ndege ndefu zaidi duniani imepewa kibali na sasa iko mbioni kuunda ndege hiyo ianze kubeba abiria.

Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Uingereza (CAA) imetoa kibali kwa kampuni ijulikanayo kama Hybrid Air Vehicles (HAV) yenye makao yake katika mji wa Bedford.

Hatua hiyo inafuatia kufanikiwa kwa majaribio ya ndege ya mfano iliyopewa jina Airlander 10.

Inagwa Airlander haina kasi kubwa kama ndege nyingine, sifa yake kubwa ni kwamba inaweza kukaa angani kwa siku tano bila kuhitaji kuongeza mafuta.

Vile vile ina uwezo wa kubeba mizigo tani 50, jambo ambalo ni gumu kwa ndege za kawaida.