Majaliwa ataka matamasha ya biashara Z'bar kutangaza utalii

|
Waziri mkuu Kassim Majaliwa akimshukuru Waziri wa Biashara Zanzibar, Balozi Amina Salum Ali kwa zawadi ya picha baada ya kufungua Tamasha la 4 la Biashara.

Waziri mkuu, Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko ya Zanzibar kuhakikisha inatumia Tamasha la Biashara la Zanzibar kama chachu ya kukuza biashara ya Utalii kama ilivyo kwa Tamasha la manunuzi la Dubai na matamasha mengine Duniani.

“Natambua kwamba kazi ya kulipandisha hadhi zaidi tamasha letu hili siyo ndogo, hata hivyo ninayo imani kubwa kwamba  siyo tu uwezo wa kufikia malengo hayo mnayo bali pia mnaweza.” Alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Waziri mkuu ameyasema hayo jana Jumatano,  wakati akifungua Tamasha la Nne la Biashara la Zanzibar lililofanyika kwenye Viwanja vya Maisara katika Mkoa wa Mjini Magharibi, Wilaya ya Mjini.

Tamasha hilo limefunguliwa jana ikiwa ni miongoni mwa maandalizi ya shamrashamra za kuelekea  sherehe za kuadhimisha miaka 54 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, ambayo yalitokea Januari 12, 1964.

Alisema Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko inatakiwa kutumia fursa ya uwepo wa tamasha hilo katika kuhakikisha inakuza biashara ya Utalii kwa kuwa linajumuisha wafanyabiashara kutoka mataifa mbalimbali.

Waziri mkuu amesema Tamasha la Biashara ni nyenzo muhimu ya kukuza biashara na huduma pamoja na uchumi wa nchi, pia hutoa fursa ya kuwakutanisha wafanyabiashara na watoa huduma na wateja wao.

”Hali hii humwezesha mzalishaji kupata mrejesho kuhusu namna bidhaa yake inavyokubalika katika soko, mapungufu yaliyopo kwenye bidhaa husika pamoja na kuelewa maboresho anayotakiwa kuyafanya katika bidhaa au huduma.”

Waziri mkuu amesema kuwa tamasha hilo linaweza kutumika kama nafasi muhimu katika kuanzisha uhusiano mzuri wa kibiashara kati ya mteja  na mfanyabiashara, hivyo kuwawezesha wajasiriamali kuwa na masoko ya uhakika.

Amesema kuwa kufanyika kwa tamasha hilo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 katika Ibara ya 84 (f).

“Ilani imeweka wazi azma ya Serikali ya kuanzisha na kuendeleza ujenzi wa kiwanja cha maonyesho ya biashara cha kimataifa na kuhakikisha ushiriki wa wajasiriamali wa Zanzibar  katika maonyesho ya biashara ya kimataifa ndani na nje ya nchi.”

Baada ya kufungua tamasha hilo waziri mkuu alitembelea mabanda mbalimbali katika viwanja hivyo yakiwemo ya taasisi za umma pamoja na wajasiriamali ambao wanatoka Zanzibar, Tanzania Bara, Kenya, Uturuki, Misri, Uganda na Burundi.

Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Zanzibar, Balozi Amina Salum Ali awali kabla ya ufunguzi huo alisema tamasha hilo lenye washiriki zaidi ya 200 limeandaliwa na wizara yake pamoja na TanTrade.

Balozi Amina amesema kauli mbiu ya tamasha hilo kwa mwaka 2018 ni “ Wekeza kwenye viwanda kwa uchumi na ajira”  lengo likiwa ni kuhamasisha wadau kuongeza uelewa kwa wananchi juu ya falsafa na dhima ya ujenzi wa viwanda.

Utalii
Maoni