Majaliwa: Watanzania tumieni bidhaa zinazozalishwa nchini

|
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akikagua bidhaa zinazozalishwa mkoani Pwani

Waziri mkuu ametoa rai kwa taasisi zenye miradi mbalimbali nchini pamoja na wananchi kuthamini na kuzitumia bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya hapa nchini zikiwemo na za viwanda vya Mkoa wa Pwani kwani zina viwango vya ubora.

Waziri mkuu amesema hayo wakati wa kufunga maonesho ya Wiki ya Viwanda mkoani Pwani.

Waziri Mkuu amesema kupitia maonesho hayo ya viwanda vilivyopo katika Mkoa wa Pwani vimeudhihirishia umma kuwa vina uwezo mkubwa wa kuzalisha bidhaa zilizo bora na hata kuzidi zile zinazoingizwa kutoka nje, amewahamasisha wananchi kutumia bidhaa hizo za ndani.

“Wakati natembelea mabanda kwenye maonesho haya nimeshuhudia bidhaa nyingi nzuri na zenye ubora. Nimeona wazalishaji wa saruji, mabati, nondo, marumaru, mabomba ya plastiki, chuma, zana za kilimo, vyakula, vinywaji na vifungashio.” Alisema Waziri mkuu.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Selemani Jafo ameiagiza mikoa yote nchini kuhakikisha inatumia bidhaa zinatengenezwa na viwanda vya ndani katika miradi mbalimbali ya ujenzi wanayoitekeleza kama ujenzi wa hospitali za wilaya na vituo vya afya.

Amesema wakuu wa mikoa ni lazima wahakikishe bidhaa kama saruji, nondo, marumaru, mabati zinavyotumika katika ujenzi ziwe vimezalishwa na viwanda vya ndani kwa sababu vina viwango vya ubora unaotakiwa na pia itasaidia kuondoa tatizo la soko la bidhaa hizo.

Naye, Waziri Mwijage kwa upande wake amewataka watendaji wanaohusika na masuala ya viwanda kutoweka vikwazo kwa wawekezaji ambao wanakwenda katika ofisi zao kwaajili ya kutafuta maeneo ya kuwekeza kwenye viwanda au wanaohitaji vibali kwani jambo hilo halina tija.

Viwanda
Maoni