Test
TAA yaja na tozo mpya ya usalama wa abiria

 

Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imewataarifu Waendeshaji wa Mashirika ya ndege za abiria zinazofanya safari zake kuanzia Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) juu ya tozo mpya ya usalama wa abiria.

Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Richard Mayongela amewaeleza kuwa utekelezaji wa tozo hiyo ambayo ni dola tano (5) kwa abiria wa nje ya nchi na abiria wa ndani ni sh. 5,000 utaanza rasmi tarehe 1 Oktoba, 2018.

Mayongela amesema lengo la tozo hiyo ni uboreshwaji wa huduma na miundombinu ya Usalama katika Viwanja vya Ndege nchini ili kuhakikisha vinafikia viwango vya ubora vya Kimataifa na pia kutoa huduma bora za kiusalama kwa wadau wake.

Akitoa ufafanuzi zaidi kuhusiana na ada hiyo Kaimu Mkurugenzi wa Fedha na Biashara wa TAA, Pius Wankali ameeleza kwamba agizo la ukusanywaji wa tozo  hiyo ulitangazwa rasmi na Mamlaka ya Usafiri wa  Anga (TCAA) mwezi Juni mwaka huu.

“Tangazo la kuanzishwa kwa tozo hii lilichapishwa na TCAA kutoka kwenye nyaraka AIC Doc No. TCAA/FRM/ANS/AIS-30, tarehe 29 Juni, 2018 na utekelezaji wake utakuwa ni kuanzia Oktoba Mosi, 2018," amesema Wankali.

Kwa upande wa wawakilishi wa mashirika ya ndege kubwa kutoka Shirika la ndege Tanzania (ATCL), Ismail Ismail alitaka kuwepo kwa maelezo ya kina juu ya tozo hiyo, ambayo alitaka ijumuishwe ndani ya tiketi ili abiria awe ameilipia moja kwa moja.

Kwa upande wake mwakilishi mwingine wa ndege kubwa ya KLM, Bw. Alexander Van de Wint ameomba tozo hii ianze baadaye mwakani kutokana na wao tayari wameshauza tiketi za msimu hadi Desemba 2018 ili wasiwaumize abiria wao.

Mwenyekiti wa Waendeshaji wa Ndege ndogo za abiria, Chief Uyeka Rumbyambya amesema kuwe na taratibu za kumuhusisha Mkurugenzi Mkuu katika mikutano mbalimbali ya Waendeshaji wa Mashirika ya ndege, ili waweze kuwasilisha.

Naye Kaimu Meneja Mipango na Takwimu wa TAA, ambaye ni mratibu wa mkutano huo, Bw. Nasib Elias alitoa ufafanuzi juu ya ukusanywaji wa tozo hii, ambayo inatarajiwa pia kuwa ni moja ya chanzo cha mapato cha Mamlaka.

Benki za kibiashara sasa kukopesha kwa riba ndogo zaidi

Baada ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kupunguza riba kwa benki nchini kutoka asilimia tisa hadi saba, Watanzania wengi sasa watapata ahueni ya kukopeshwa kwa riba ndogo na kwa muda mrefu kuliko ilibyokuwa hapo mwanzo.

Punguzo hilo la riba litaanza rasmi Agosti 27 na litaendelea hadi yatakapofanyika mapitio mapya.

Barua ya Naibu Gavana wa BoT anayesimamia sera za uchumi na fedha (EFP), Dk Yamungu Kayandabila iliyoandikwa Agosti 23 kwenda kwa benki za biashara na taasisi za fedha inabainisha kushuka kwa riba hiyo kwa asilimia mbili huku utekelezaji wake ukielezwa kuanza kesho.

“Kama nilivyowaeleza kwenye waraka wa Agosti 3, 2017, nawafahamisha kupungua kwa riba itakayotozwa kwenye mikopo yote ambayo benki za biashara zitakopa kutoka Benki Kuu pamoja na amana za Serikali mpaka asilimia saba kutoka asilimia tisa iliyokuwapo (na) itakayotumika mpaka marekebisho mengine yatakapofanyika,” inasomeka taarifa hiyo. Nakala ya barua hiyo pia imepelekwa kwa katibu mkuu Wizara ya Fedha na Mipango.

Nakala nyingine imekwenda kwa Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Kamishna wa Mamlaka ya Mapato (TRA).

Katika taarifa hiyo, Dk Kayandabila alisema mabadiliko hayo yamezingatia mwenendo wa mauzo ya hatifungani za Serikali hasa zinazoiva baada ya siku 91 au 182.

“Mapitio haya yanadhihirisha juhudi za makusudi kukuza kiasi cha mikopo inayotolewa kufanikisha shughuli za uchumi,” ameandika Naibu Gavana kwenye taarifa yake kwa umma.

Tanzania, Benki ya Dunia warahisisha mfumo wa mikopo ya nyumba

Katika kuhakikisha mikopo ya nyumba inaanzishwa nchini, Serikali ikishirikiana na Benki ya Dunia imeanzisha mradi wa kuwezesha kuwepo kwa mfumo wa mikopo ya nyumba.

Mradi huo uitwao mikopo ya nyumba unalega kuanzisha mifumo ya mikopo ya nyumba kutokana na kufilisika kwa Benki ya Nyumba Tanzania mwaka 1995 ambayo ilikuwa inatoa mikopo ya muda mrefu kwa wateja kwaajili ya ujenzi na ununuzi wa nyumba za makazi.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji amesema hayo jijini Dar es Salaam kwenye hafla ya kuorodhesha hatifungani yenye thamani ya shilingi bilioni 120 za Kampuni ya Mikopo ya Nyumba (TMRC) katika Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE).

“Mradi huu una maeneo makuu matatu ambayo ni uanzishwaji wa mfumo wa mikopo ya nyumba, uanzishwaji wa mfuko wa mikopo midogo midogo ya nyumba na kuendeleza mfumo wa ujenzi wa nyumba wa gharama nafuu kwa lengo la kuwapunguzia wananchi gharama za ujenzi na kuwa na nyumba za gharama nafuu,” alisema Dkt. Kijaju.

Amefafanua ili kutekeleza malengo hayo matatu Serikali ilikopa jumla ya Dola za Marekani milioni 100 mwaka 2010 kutoka Benki ya Dunia ili kuwezesha mradi wa mikopo ya nyumba kufikia malengo.

Mwenyekiti mpya wa bodi ya Wakurugenzi wa TMRC, Theobald Sabi amesema katika kipindi cha miaka saba, TMRC imeweza kuongeza muda wa urejeshaji mikopo kwa miaka 15 hadi 25 kutoka miaka mitano (5) - 10 kwa mwaka 2010.

Sabi amesema "Idadi ya benki zinazotoa mikopo ya nyumba zimeongezeka hadi kufikia Machi 31 mwaka 2010 kulikuwa na benki tatu huku riba ya mikopo ya ujenzi ikipungua kutoka asilimia 22 na 24 hadi asilimia 16 hadi 19.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa TMRC, Oscar Philemon Mgaya, amesema wameongeza asilimia 1.0 kama ziada ya kiasi cha Shilingi bilioni 12.5 bilioni kilichopatikana kutoka kwenye hatifungani.

"Baada ya Benki Kuu kushusha riba, gharama nyingine ikiwemo riba kwenye mikopo zinaweza kushuka pia," Mgaya amesema.

 

Halotel yazindua laini mpya za watu mashuhuri (VIP)

 

Kampuni ya mawasiliano ya simu ya Halotel, kwa mara ya kwanza imezindua laini mpya za watu mashuhuri zilizopewa jina la VIP zitakazo wawezesha wateja wa mtandao huo kufanya mawasiliano kwa makato ya gharama nafuu zaidi kwa kila dakika na vifurusi vya data.

Laini hizo zitawawezesha wateja wa mtandao wa Halotel nchi nzima kupiga simu au kutumia intanenti kwa gharama nafuu kwa bila kuwa na ulazima wa kujiunga na kifurushi chochote.

“Huduma hii inawalenga wateja wa vipato vya aina zote, wale wenye matumizi ya kati, na matumizi makubwa, ambapo katika laini hii ya VIP makundi hayo yamegawanywa kwa kupewa majina ambayo ni Silver kwa wateja wenye matumizi madogo, Gold kwa wateja wa matumizi ya kati na Diamond kwa wateja wa matumizi makubwa. Makundi haya yana lengo la kukidhi mahitaji ya kila mteja kulingana na kundi alilomo.” Alisema Semwenda na kuongeza,” Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Kampuni hiyo, Mhina Semwenda, alisema wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo.

Aliongeza kuwa uzinduzi huo ni mwendelezo wa ubunifu na maboresho ya huduma za mawasiliano kwa wateja wa  Halotel kwa kuwaokolea muda na gharama ambapo badala ya mteja kutumia muda na gharama kujiunga na vifurushi vya kupiga simu kwa mtandao wa Halotel na mitandao yote au vifurushi vya intaneti mteja ataweza kutumia salio la muda wa maongezi kupiga simu  au kutumia intaneti bila kuhofia matumizi makubwa ya makato kwa gharama nafuu zaidi.

 “Mfano kwa mteja atakayenunua laini ya VIP ya Silver yenye thamani ya shilingi elfu tano (5,000) kwa pesa hiyohiyo anaweza kupiga simu Halotel kwenda Halotel kwa gharama ya makato ya shilingi thelathini tu kwa dakika ambapo kwa makato ya gharama ya kawaida ni shilingi 228 kwa dakika ambapo ni punguzo ya mara saba ya gharama za  kawaida.

Vile vile mteja katika kundi hili anaweza kupiga simu kwenda mitandao yote kwa gharama ya makato ya shilingi 45 tu kwa dakika tofauti na makato ya gharama ya kawaida ambayo ni shilingi 228 kwa dakika ambapo ni punguzo mara tano ya gharama za kawada. Kwa MB 1 mteja atatumia intanenti kwa gharama ya shilingi nne tu akiwa na laini ya Silver ya VIP gharama ambayo ni mara saba pungufu ya makato ya gharama ya kawaida ya shilingi 30.72 kwa MB huku akifurahia kutumia Facebook bure.” Alisema Semwenda.

Mteja yeyote wa Halotel wa kawaida ana uhuru wa kuweza kubadili laini yake na kuwa laini ya VIP na kuweza kufurahia kupiga simu Halotel na mitandao yote pamoja nakutumia Mb za intanenti kwa kupiga *148*66# kisha anachagua namba tisa na hivyo kuendelea kuchagua kundi atakalohitaji kujiunga, si hivyo tu mteja wa Halotel wa kawaida anaweza kuendelea kujiunga na vifurushi kama kawaida endapo atahitaji.

 

Uholanzi yahoji uhalali wa Rwanda kuidhamini Arsenal ilihali inapokea misaada

Rwanda imetetea uamuzi wake wa kuingia mkataba wa kutangaza utalii wa nchi hiyo kupitia klabu ya Arsenal ya Uingereza.

Utetezi huo umekuja baada ya bunge la Uholanzi kukosoa uamuzi wa serikali ya Rwanda kuidhamini klabu hiyo yenye maskani yake jijini London.

Rwanda na Arsenal zimeingia mkataba wa kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini Rwanda kupitia tangazo maalumu linalosomeka “Visit Rwanda” au “Tembelea Rwanda” ambalo kuanzia msimu ujao timu zote za Arsenal (Ya wanaume, wanawake, watoto nk) zitakuwa zikivaa jezi iliyochapishwa tangazo hilo kwenye sehemu ya juu ya upande wa kushoto.

Hata hivyo Bunge la Uholanzi limehoji uwezo wa Rwanda wa kuidhamini Arsenal wakati nchi hiyo inapokea misaada mbalimbali kwaajili ya kusaidia maendeleo nchini humo.

Mkataba huo wa udhamini unadaiwa kugharimu $40m.

Kufuatia kutoridhishwa na mkataba huo, bunge la Uholanzi limemtaka waziri wa misaada wan chi hiyo, Sigrid Kaag kufuatilia kwa karibu mkataba huo.

Inadaiwa kuwa mmoja wa wabunge wa bunge hilo alidai “inakuwaje nchi inayopokea misaada mingi inakuwa na uwezo wa kuwekeza kiasi kikubwa hivyo.”

Taarifa zinaendelea kudai kuwa mbunge mwingine alidai “Inahuzunisha kuona pesa nyingi kiasi hicho zikilipwa wakati jumuiya ya kimataifa ikijaribu kupambana kuondosha umaskini kwenye nchi hiyo hiyo”

Rwanda ni moja kati ya nchi 15 zinazopata misaada kutoka Uholanzi.

TMRC yazindua mpango wa hatifungani

Kampuni ya Utoaji Mikopo kwa Mabenki na Taasisi za fedha kwa ajili ya mikopo wa nyumba Tanzania (TMRC), leo imezindua mpango wa hatifungani wa miaka mitano kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).  

Uzinduzi huo ulifanywa na Mwenyekiti wa Bodi ya kampuni hiyo Bw. Ammish Owusu-Amoah jijini Dar es Salaam ulishuhudiwa na wawekezaji pamoja na wadau mbalimbali toka sekta za fedha, nyumba na sekta nyingine.

Uzinduzi wa utoaji wa dhamana ya TMRC ulifanyika baada ya TMRC kupokea kibali kwa ajili ya programu ya utoaji wa dhamana ya miaka 5 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 120. Mpango huo ulipata kibali kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Masoko ya Mitaji (CMSA) pamoja na Soko la Hisa (DSE). Kampuni hiyo ya TMRC itaorodheshwa katika soko la hisa la Dar es Salaam.

Aidha, CMSA na DSE, zilijiridhisha kuendelea kwa TMRC kutoa dhamana ya ushirika wake ambayo itakuwa kiasi cha Shilingi Bilioni 12. Afisa Mtendaji Mkuu wa TMRC, Oscar Mgaya alisema "tumepokea vibali vyote muhimu na tunatarajia kwenda kwenye Soko la Hisa kwa mara ya kwanza hivi karibuni".

TMRC ni taasisi maalum ya sekta binafsi ya Fedha ambayo hutoa fedha za muda mrefu kwa taasisi za fedha kwa madhumuni ya mikopo ya nyumba.

Taasisi hii ina lengo la kuunga mkono taasisi za kifedha kutoa mikopo ya nyumbaya muda mrefu ambayo husaidia kushusha marejesho ya kila mwezi na kuwezesha wateja wengi kumudu. Aina hii ya kukopesha pia inajulikana kama mikopo ya jumla.

TMRC inatafuta fedha ili kusaidia shughuli zake za mikopo ya nyumba. "Ilifikiriwa tangu mwanzo kwamba TMRC itapata fedha kutoka kwenye masoko ya mitaji kupitia utoaji wa dhamana kati ya vyanzo vingine" alisema Mgaya. Aliongeza kwamba "Ilikuwa tu suala la muda na sasa ni wakati mzuri kwa sababu riba za soko zimekua zikishuka"

 

Urasimu wa Tanesco wazuia kuzalishwa kwa 360 MW Rukwa

Wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda nchini wamelitupia lawama shirika la umeme (Tanesco) kwa  kuendekeza urasimu, tendo ambalo linarudisha nyuma juhudi za serikali za kujenga nchi ya viwanda.

“Kampuni yangu Edenville Energy inauwezo wa kuzalisha zaidi ya megawati 360 za umeme mkoani Rukwa. Tumekuwa na majadiliano ya muda mrefu sana na Tanesco bila sababu za msingi… uzalishaji wa umeme umekwama  kutokana na urasimu huo... hivyo basi… ninamuomba mwenyekiti wa baraza hili kuingilia kati,”Kasiano Kaegele, mmiliki wa kampuni ya Edenville energy ametoa kauli hiyo leo Machi 19, 2018 katika mkutano wa 11 wa Baraza la Taifa la Biashara unaofanyika Ikulu Dar es Salaam na kuongozwa na mwenyekiti wa baraza hilo, Rais John Magufuli.

Makamu Mwenyekiti wa Mfuko wa Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Salum Shamte amesema sekta ya umeme inaweza kukwamisha juhudi za uchumi wa viwanda.

Amesema kiwango cha wastani wa kuhudumia umeme kwa kila mtanzania bado kipo chini sana na hakiwezi kufanikisha juhudi hizo.