Test
Uholanzi yahoji uhalali wa Rwanda kuidhamini Arsenal ilihali inapokea misaada

Rwanda imetetea uamuzi wake wa kuingia mkataba wa kutangaza utalii wa nchi hiyo kupitia klabu ya Arsenal ya Uingereza.

Utetezi huo umekuja baada ya bunge la Uholanzi kukosoa uamuzi wa serikali ya Rwanda kuidhamini klabu hiyo yenye maskani yake jijini London.

Rwanda na Arsenal zimeingia mkataba wa kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini Rwanda kupitia tangazo maalumu linalosomeka “Visit Rwanda” au “Tembelea Rwanda” ambalo kuanzia msimu ujao timu zote za Arsenal (Ya wanaume, wanawake, watoto nk) zitakuwa zikivaa jezi iliyochapishwa tangazo hilo kwenye sehemu ya juu ya upande wa kushoto.

Hata hivyo Bunge la Uholanzi limehoji uwezo wa Rwanda wa kuidhamini Arsenal wakati nchi hiyo inapokea misaada mbalimbali kwaajili ya kusaidia maendeleo nchini humo.

Mkataba huo wa udhamini unadaiwa kugharimu $40m.

Kufuatia kutoridhishwa na mkataba huo, bunge la Uholanzi limemtaka waziri wa misaada wan chi hiyo, Sigrid Kaag kufuatilia kwa karibu mkataba huo.

Inadaiwa kuwa mmoja wa wabunge wa bunge hilo alidai “inakuwaje nchi inayopokea misaada mingi inakuwa na uwezo wa kuwekeza kiasi kikubwa hivyo.”

Taarifa zinaendelea kudai kuwa mbunge mwingine alidai “Inahuzunisha kuona pesa nyingi kiasi hicho zikilipwa wakati jumuiya ya kimataifa ikijaribu kupambana kuondosha umaskini kwenye nchi hiyo hiyo”

Rwanda ni moja kati ya nchi 15 zinazopata misaada kutoka Uholanzi.

TMRC yazindua mpango wa hatifungani

Kampuni ya Utoaji Mikopo kwa Mabenki na Taasisi za fedha kwa ajili ya mikopo wa nyumba Tanzania (TMRC), leo imezindua mpango wa hatifungani wa miaka mitano kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).  

Uzinduzi huo ulifanywa na Mwenyekiti wa Bodi ya kampuni hiyo Bw. Ammish Owusu-Amoah jijini Dar es Salaam ulishuhudiwa na wawekezaji pamoja na wadau mbalimbali toka sekta za fedha, nyumba na sekta nyingine.

Uzinduzi wa utoaji wa dhamana ya TMRC ulifanyika baada ya TMRC kupokea kibali kwa ajili ya programu ya utoaji wa dhamana ya miaka 5 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 120. Mpango huo ulipata kibali kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Masoko ya Mitaji (CMSA) pamoja na Soko la Hisa (DSE). Kampuni hiyo ya TMRC itaorodheshwa katika soko la hisa la Dar es Salaam.

Aidha, CMSA na DSE, zilijiridhisha kuendelea kwa TMRC kutoa dhamana ya ushirika wake ambayo itakuwa kiasi cha Shilingi Bilioni 12. Afisa Mtendaji Mkuu wa TMRC, Oscar Mgaya alisema "tumepokea vibali vyote muhimu na tunatarajia kwenda kwenye Soko la Hisa kwa mara ya kwanza hivi karibuni".

TMRC ni taasisi maalum ya sekta binafsi ya Fedha ambayo hutoa fedha za muda mrefu kwa taasisi za fedha kwa madhumuni ya mikopo ya nyumba.

Taasisi hii ina lengo la kuunga mkono taasisi za kifedha kutoa mikopo ya nyumbaya muda mrefu ambayo husaidia kushusha marejesho ya kila mwezi na kuwezesha wateja wengi kumudu. Aina hii ya kukopesha pia inajulikana kama mikopo ya jumla.

TMRC inatafuta fedha ili kusaidia shughuli zake za mikopo ya nyumba. "Ilifikiriwa tangu mwanzo kwamba TMRC itapata fedha kutoka kwenye masoko ya mitaji kupitia utoaji wa dhamana kati ya vyanzo vingine" alisema Mgaya. Aliongeza kwamba "Ilikuwa tu suala la muda na sasa ni wakati mzuri kwa sababu riba za soko zimekua zikishuka"

 

Urasimu wa Tanesco wazuia kuzalishwa kwa 360 MW Rukwa

Wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda nchini wamelitupia lawama shirika la umeme (Tanesco) kwa  kuendekeza urasimu, tendo ambalo linarudisha nyuma juhudi za serikali za kujenga nchi ya viwanda.

“Kampuni yangu Edenville Energy inauwezo wa kuzalisha zaidi ya megawati 360 za umeme mkoani Rukwa. Tumekuwa na majadiliano ya muda mrefu sana na Tanesco bila sababu za msingi… uzalishaji wa umeme umekwama  kutokana na urasimu huo... hivyo basi… ninamuomba mwenyekiti wa baraza hili kuingilia kati,”Kasiano Kaegele, mmiliki wa kampuni ya Edenville energy ametoa kauli hiyo leo Machi 19, 2018 katika mkutano wa 11 wa Baraza la Taifa la Biashara unaofanyika Ikulu Dar es Salaam na kuongozwa na mwenyekiti wa baraza hilo, Rais John Magufuli.

Makamu Mwenyekiti wa Mfuko wa Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Salum Shamte amesema sekta ya umeme inaweza kukwamisha juhudi za uchumi wa viwanda.

Amesema kiwango cha wastani wa kuhudumia umeme kwa kila mtanzania bado kipo chini sana na hakiwezi kufanikisha juhudi hizo.

BOT yatolea ufafanuzi kuhusu anguko la kiuchumi

Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imetoa ufafanuzi kuhusu madai ya kushuka kwa uwekezaji wa Hati fungani na dhamana hadi kufikia asilimia Nne hadi Sita ambao umetajwa kuwa ni anguko la kiuchumi.

Gavana wa BOT, Profesa Florens Luoga ametoa ufafanuzi huo kwa Azam TV  kuhusu madai hayo ambayo yamezua mijadala kwenye mitandao ya kijamii.

Kushuka na kupanda kwa riba za dhamana hutokana na nguvu ya soko, na siyo kwa uamuzi wa Benki Kuu.

Gavana huyo amesema, Dhamana za serikali, hutolewa au huuzwa kwa njia ya mnada ambapo kila mwekezaji anawasilisha zabuni inayoonyesha bei ambayo yuko tayari kulipa kulingana na mahitaji yake.

Benki Kuu ikiwa ni wakala wa serikali, hushindanisha maombi ya wawekezaji kufuatana na kiasi ambacho serikali imepanga kukopa katika mnada husika. Ushindani huu ndiyo unaotoa riba ya soko.

Kushuka kwa riba ya dhamana ni ishara ya kuwepo ukwasi mwingi na hii inaendana na sera ya kujenga mazingira ya kuongeza mikopo kwa sekta binafsi.

NMB yafunga mwaka na faida ya shilingi Bilioni 95

Benki ya NMB imepata faida baada ya kodi ya shilingi Bilioni 95 mwaka 2017.

Kutokana na changamoto za kibiashara zilizojitokeza mwaka 2017, Benki ya NMB iliweza kuongeza pato lililotokana na biashara ya benki kwa asilimia 5 kutoka shilingi bilioni 614 mwaka 2016 mpaka bilioni 647 mwaka 2017, Biashara ya benki iliendelea kuwa imara kipindi hiki. Kwa miaka mitano mfurulizo, benki ilitajwa kama benki bora nchini na kwa mara ya kwanza, ilitajwa kuwa benki bora inayoendelea barani Afrika na taasisi ya kiamataifa ya Euromoney.

Benki ya NMB ilipata faida baada ya kodi ya shilingi Bilioni 95 kwa mwaka 2017 chini ya shilingi Bilioni 154 iliyofikiwa mwaka 2016. Kushuka kwa faida hiyo kunatokana na ongezeko la changamoto za urejeshwaji wa mikopo kutoka kwa Wateja.

Kiwango kikubwa cha riba kilikuwepo mwanzoni mwa mwaka 2017. Hii ilitokana na ongezeko la asilimia 18 ya gharama za riba kutoka shilingi Bilioni 102 ya mwaka 2016 mpaka shilingi bilioni 120 ya mwaka 2017. Wakati huo huo mapato ya riba yaliongezeka kwa asilimia 4 kutoka shilingi Bilioni 449 kwa mwaka 2016 mpaka shilingi bilioni 467 kwa mwaka 2017.

Mapato ya biashara ya fedha za kigeni ilikuwa kwa asilimia 15 kutoka shilingi Bilioni 15 mwaka 2016 mpaka shilingi bilioni 18 mwaka 2017. Ada na kamisheni zilikua kwa asilimia 11 hasa kutokana na kuongezeka kwa miamala kutoka njia mbalimbali za kibenki; Pato lisilokuwa na riba (non-interest revenue) liliongezeka kwa asilimia 9 mpaka shilingi Bilioni 180.

Katika robo ya nne ya mwaka 2017, Amana za wateja nazo ziliongezeka kwa asilimia 9 hadi kufikia kiasi cha shilingi trilioni 4.2 robo ya nne ya 2017.  Matokeo haya yaliifanya benki kukuza kitabu cha mikopo na hivyo mikopo ilikua mpaka kufikia shilingi bilioni 2,786 kwa robo ya tatu ya mwaka mpaka kufikia shilingi bilioni 2,787 katika robo ya nne ya mwaka 2017.

 

Wafanyakazi wa serikali waliobainika kuwa na vyeti feki na kuachishwa kazi na waajiri wao serikali katika robo ya kwanza ya mwaka 2017, ambapo baadhi yao walikuwa na mikopo ya NMB Bank na baadhi ya Wateja wakubwa walioshindwa kulipa mikopo yao kama ilivyotarajiwa ilisababisha kuongezeka kwa mikopo isiyolipika.

Benki ya NMB ipo kwenye mazungumzo na serikali na ina Imani kubwa kuwa kutakuwa na maamuzi ambayo yatasaidia kupunguza athari za mikopo, punguza mikopo isiyolipika na hivyo kuongeza faida ya benki.

Katika wakati ambapo biashara inalazimika kufanya marekebisho ili kuendana na mabadiriko ya mazingira ya ufanyaji biashara, benki ilichukua hatua mbalimbali ili kukabiliana na mikopo mibaya. Ikiwa ni pamoja na kupunguza baadhi ya huduma na pia kufuta mikopo isiyolipika kwenye vitabu vya mikopo ambayo imeweza kurekebisha Kiwango cha mikopo isyolipika (Non-Performing Loans) kutoka asilimia 9.3 ya robo ya tatu mpaka asilimia 6.4 kwa Desemba 31, 2017.

Mkurugenzi wa NMB Bank – Ms Ineke Bussemaker aliwahakikishia Wateja na wadau kuwa benki ipo imara na itaendelea na malengo yake ya kutoa huduma bora ya kifedha kwa watanzania wote. Mwaka 2017, benki ilifungua matawi mapya 23, vituo 10 vya kukusanya fedha na mawakala 2,389.

Katika utekelezaji wa IFRS 9, kuanzia Januari 1, 2018, Bi Bussemaker aliwahakikishia kuwa benki ina mtaji imara ambayo itaeendelea kuwa juu ya wastani uliowekwa na mamlaka za usimamiaji mabenki nchini. NMB Bank ilimaliza mwaka na uwiano wa utosherevu wa mtaji halisi wa benki wa asilimia 17 ukilinganisha na asilimia 14.5 inayotakiwa na Uwiano wa ukwasi wa benki (Liquid Asset Ratio) wa asilimia 39 ukilinganisha na Kiwango kinachohitajika cha asilimia 20.

Tanzania yaibuka kinara ukuaji wa uchumi jumuishi Kusini mwa Afrika

Tanzania kuibuka kinara miongoni mwa nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa kuwa na Uchumi Jumuishi (Inclusive Economy) unaokua duniani.

Taarifa iliyotolewa na Word Economic Forum kupitia mradi wake wa mradi wa ‘The Inclusive Development Index’, imeitaja Tanzania kushika nafasi ya kwanza kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara na ya 48 kati ya nchi 103 zilizofanyiwa tathmini ya nchi zenye Uchumi Jumuishi duniani.

Katika orodha ya kumi bora, nchi zilizofuatia na nafasi ziliyoshika kidunia ni pamoja na Ghana (52), Cameron (53), Burundi (55), Namibia (56), Rwanda (57), Uganda (59), Mali (60), Senegal (61) na Nigeria (63).

“Takwimu za ukuaji huu zinaakisi moja kwa moja kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ambaye amekuwa akielezea kutaka uchumi wa Tanzania umilikiwe na wananchi kwa njia mbalimbali ikiwemo kutekeleza sera ya uchumi wa viwanda ambapo watanzania wengi hivi sasa wamekuwa wakitekeleza sera hiyo kwa kuanzisha viwanda vikubwa na vidogo,” mtaalamu Mbobevu wa masuala ya Uchumi na Mhadhiri wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi ameeleza.

Amesema kwamba takwimu zilizotolewa na taasisi hiyo zinatafsiri kuwa uchumi wa Tanzania unaelekea kumilikiwa na watu wengi zaidi jambo ambalo litasaidia kupunguza pengo la kipato kati ya walionacho na wasionacho.

Profesa Ngowi ameeleza kuwa uchumi wa aina hiyo unawashirikisha wananchi kumiliki uchumi na kuwafanya watu wengi kufaidi matunda ya ukuaji wa uchumi wa nchi.

“Taarifa hizi ni njema kwani kitaalam tunaita broad based economy ambapo watu wengi wanashirikishwa kumiliki uchumi na wengi wanafaidi,” alieleza Profesa Ngowi na kuongeza kuwa kuna nchi zingine zinauchumi mzuri lakini unamilikiwa na watu wachache na kufanya kuwa na pengo kubwa kati ya walionacho na wasionacho.

Katika siku za hivi karibuni, Taasisi mbalimbali duniani zimekuwa zikitoa ripoti zikiielezea Tanzania kupaa kiuchumi ambapo ripoti za Shirika la Fedha Duniani (IMF), Benki ya Dunia (WB) na Taasisi ya Goldman Sachs ya Marekani hivi karibuni zilitabiri kuwa wakati uchumi wa dunia utakua kwa wastani wa asilimia 3.0 hadi 4.0, ukuaji wa uchumi wa Tanzania unatajwa kuendelea kuwa kati ya nchi tano bora za Afrika ukitarajiwa kukua kwa asilimia 6.5 hadi 7.0 katika mwaka 2018. 

 

 

Zantel yawakomboa wakulima wa zao la mwani Zanzibar

Watu wengi walio nje ya Zanzibar wanadhani kuwa Unguja na Pemba ni visiwa vya starehe na mahali pa kupumzika tu. Uzuri wa Zanzibar umekuwa kivutio kwa watalii kutoka nchi mbalimbali duniani jambo ambalo linaifanya Zanzibar kuimarika kwenye masuala ya Utaliii.

Hata hivyo ukija kwenye masuala ya Kilimo, watu wengi wamekuwa wakiamini kwamba Utalii na kilimo cha karafuu ndio mambo pekee ya kibiashara yanayofanyika visiwani humo.

Kilimo cha zao la ‘MWANI’ kimekuwa ni miongoni mwa mazao makubwa ya biashara yanayouzwa nje ya nchi tangu mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Shughuli za kilimo cha zao la mwani zilianza Zanzibar mwaka 1989 na zao hilo limewavuta watu wengi kujishugulisha na biashara hiyo licha ya kuwapo kwa changamoto kadhaa wanazokabiliana nazo.

Takribani asilimia 80 ya wanawake Zanzibar wanajishughulisha na kilimo cha zao hilo na wamekuwa wakitoa wito kwa Serikali na Taasisi za watu binafsi kuwasaidia katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Juni mwaka 2016, kampuni ya mawasiliano inayoongoza katika huduma ya intaneti ya Zantel ilikubali kushirikiana na wakulima baada ya kutoa msaada wa shilingi milioni 10 kwa Jumuiya ya Wakulima wa Mwani Zanzibar (JUWAMWANZA) ili kuwawezesha wanachama hao kununua vifaa vya kilimo hicho ikiwamo kamba na vijiti (pegs) ambavyo vilisambazwa kwa wakulima wa mwani katika vijiji 83 vilivyopo katika mwambao wa pwani ya Unguja, jambo lililofanikisha kilimo cha zao hilo kuendelea kufanya vizuri.

Mkuu wa Zantel Zanzibar, Mohamed Baucha alisema Kampuni hiyo ya Mawasiliano imefurahishwa kupata mrejesho kuwa msaada walioutoa umeleta mafanikio kwa wakulima wa mwani na kuwaahidi kuendelea kushirikiana na wakulima hao ili kuwasaidia kufanya kilimo cha kisasa na kuongeza uzalishaji zaidi.

Katika mahojiano ya hivi karibuni mjini Zanzibar, Baucha alisema, “Mwaka huu Zantel inasherehekea miaka miwili tangu Millicom ilipoichukua kutoka kwa Kampuni ya Etisalat ya Falme za Nchi za Kiarabu (UAE). Hivyo msaada wetu wa mwaka jana ulikuwa chini ya mradi wa wetu wa Uwajibikaji kwa jamii katika maeneo ambayo tunafanya shughuli zetu na hivyo tuliamua kuwasaidia wanawake ambao wawamejikita kwenye kilimo cha zao la mwani kisiwani hapa.”

Baucha alisema chini ya Millicom, miradi ya Zantel inayosimamiwa na Idara ya Uwajibikaji kwa jamii imejikita kuwasaidia wajasiriamali, makundi maalumu kama vile walemavu, vijana, pia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano sambamba na kuwainua wanawake katika kuleta maendeleo katika jamii na taifa kwa ujumla.

Alisema Zantel kuwasaidia wakulima wa zao la mwani, pamoja na kuitikia wito wa serikali baada ya kuziomba sekta binafsi kuunga mkono juhudi za wakulima 23,354 wa zao la mwani Zanzibar kuhakikisha kwamba wanauza mazao yao na kuongezea thamani.

Kiongozi huyo wa Zantel, Zanzibar aliongeza kwamba kampuni hiyo ipo tayari kuwasaidia wakulima wa mwani katika nyanja ya mafunzo ili kuwa na ujuzi zaidi kwa kilimo cha kisasa kwa kutumia intaneti ya Zantel kwa kujifunza zaidi kuhusu wakulima wengine wa mwani wa maeneo mengine duniani kujua nini wanachokifanya.

Licha ya kuwapa mafunzo ya jinsi ya kutumia intaneti, Zantel itawapa pia elimu ya kutumia huduma ya EzypESA ili kutunza fedha zao na wakati mwingine kuhamisha fedha zao kutoka benki kwenda kwenye mtandao wa Zantel au kwenda kwenye akaunti zao za benki pindi wanapovuna na kuuza mazao yao.

“Tunataka kuwarahishia maisha na kufanyaia wepesi kwa kuhakikisha wanapata  muda mwingi zaidi kwenye kazi zao za uzalishaji wa zao hilo ili waweze kuongeza mauzo badala ya kutumia muda mwingi kwenda mjini kufanya miamala au kukaa kwenye foleni kwa muda mrefu wakisubiri kulipia malipo ya huduma mbalimbali,” aliongeza.

Chini ya umoja wao wa Jumuiya ya Wakulima wa Mwani Zanzibar, imekuwa rahisi kwa Zantel kuwasaidia jambo ambalo wanakiri kwamba limekuwa na manufaa kwao.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa JUWAMWAZA, Pavu Mcha Khamis alisema, “Msaada wa Zantel daima utakumbukwa kutokana na kusaidia vijiji 48 Unguja na maeneo mengine ya Kisiwa cha Pemba.

Alisema wakulima wa mwani wanahitaji vifaa mbalimbali hivyo wanaendelea kutoa wa wito kwa Serikali na wadau wengine wanaoitakia mema sekta hiyo kuendelea kuwasaidia wakulima wa zao la mwani.

Pavu alifafanua kwamba wakulima wengi ambao wameelekeza nguvu zao kwenye kilimo cha mwani wanakabiliwa na kutokuwa na ujuzi kwenye kazi hiyo, uhaba wa vifaa ikiwamo viatu vya mpira, Kamba, vijiti na bei ndogo ya zao hilo sokoni vitu ambavyo viliisukuma Kampuni ya Zantel kuwa mstari wa mbele katika kutatua baadhi ya changamoto hizo  kwa kushirikiana na wanunuzi pamoja na serikali.

Kwa mujibu wa Pavu, Mwani aina ya Cottoni na Spinosum ndivyo vinastawi kwa wingi Zanzibar na kuna takribani makampuni saba ambayo hununua mwani kutoka kwa wakulima kisiwani humo lakini zaidi Makampuni hayo hununua Spinosum ambayo ndiyo huwa inauzwa pia nje ya nchi.

Alisema kwa kawaida mwani aina ya spinosum huchukua takriban siku 45 na 60 kukua hadi kuvuna na ndio unapatikana kwa wingi kwa sababu mwani aina ya Cottonii unauzwa bei ghali na wakati mwingine mwani huo hukabiliwa na hali mbaya ya mabadiliko ya hewa.

Katika mahojiano ya hivi karibuni na wakulima wa mwani wakielezea jinsi ambavyo wamenufaika na shilingi 10 milioni zilizotolewa na Zantel, Mjane Sharifa Thabit (51)  wa Kijiji cha Pongwe kilichopo, kilometa 43 toka Unguja Kusini,  amekuwa akilima zao hilo tangu lianze kulimwa Zanzibar zaidi ya mongoni mitatu iliyopita, alieleza jinsi ambavyo amefanikiwa kwenye kilimo hicho.

Alisema kwamba vifaa vya kilimo ambavyo vilitolewa na Zantel Juni mwaka jana, vimekuwa msaada mkubwa kwenye shughuli hiyo ya kilimo.

“Tunaishukuru Zantel kwa msaada wao na tunawaomba waendelee kutusaidia. Mipango yetu ni kupata mafunzo kuhusu kilimo cha kisasa cha mwani,” alisema.

Mkulima mwingine wa kijiji cha jirani cha Uroa ambaye anafanya shughuli ya kilimo kama hicho, Fatma Abbasi anasema huwa anavuna mazao yake na kwenda kuyakaushia nyumbani.

“Hii kazi ni ngumu sana lakini tunahitajika kuifanya ili kuendesha maisha,” alisema

Alipoulizwa ni kwa namna gani alinufaika na Shilingi milioni 10 zilizotolewa na Zantel,  Alisema “ Ninashukuru sana kuwa sehemu ya watu walionufaika na msaada ule mwaka jana. Imenisaidia sana kutuinua sisi wakulima.”

Alisema baada ya msaada huo wakulima wengi waliweza kuongeza kipato chao jambo lililowawezesha kuongeza uzalishaji na kwa upande wake alifanikiwa kujipatia kati ya shilingi 300,000 na 400,000 wakati wa mavuno ya kwanza.

Pongwe na Uroa ndio vijiji vyenye idadi kubwa zaidi ya watu wanaojishughulisha na kilimo cha mwani katika maeneo ya Visiwa vya Unguja na Pemba lakini bado wamekuwa wakikabiliwa na changamoto za vifaa vya kilimo na bei ndogo ya zao hilo.

Zanzibar huuza takriban tani 12,000 za mwani nje ya nchi kila mwaka ikiwa ni ya tatu kwa uuzaji wa mwani duniani ikiwa nyuma ya Phillipines inayoongoza na Indonesia. Zanzibar imeendelea kupata changamoto kubwa ya Soko kutokana na ushindani kutoka kwenye nchi kama Philippines.

Kwa mujibu wa wakulima wanaweza kuzalisha bidhaa zaidi ya 50 kutokana na zao la mwani ikiwamo juisi, dawa za hospitali, vipodozi na vingine vingi zaidi huku nchi za nje wakitumia mwani kama mbolea.

Maeneo mengi ambako hutumia zao hilo kama chakula ni barani Asia  hasa nchi za Japani, Korea na China ambako kilimo cha mwani kimekuwa muhimu katika kuinua Uchumi wa viwanda.