Mgomo wa daladala Bukoba wasababisha adha kwa abiria

|
Mabasi yanayofanya safari zake ndani ya Bukoba yakiwa yamegoma baada ya kupandishiwa ushuru

Abiria waliokuwa wakisafiri kutoka Kituo Kikuu cha mabasi Bukoba kwenda Wilaya za Mkoa wa Kagera wamekwama leo, Jumanne baada ya wamiliki na madereva wa magari madogo ya abiria aina ya Hiace kugoma wakipinga kupanda kwa ushuru mpya wa stendi wilayani Bukoba.

Mgomo huo ulianza alfajiri ya leo, Jumanne wakati wamiliki wa magari na madereva walipokumbana na ongezeko la kushtukiza la ushuru uliopandishwa na Manispaa ya Bukoba kutoka shilingi 1000 hadi  shilingi 2000

Wakizungumzia hali hiyo, madereva hao wamesema hawapingi kupanda kwa ushuru hiyo ila wanachotaka, kituo hicho kiboreshwe na kuwekwa miundombinu yote muhimu tofauti na sasa kituo hicho hakina chochote cha kusababisha ongezeko la ushuru huo.

Nao abiria walioadhirika na kadhia hiyo wamesema, kitendo cha kupandisha ushuru ni cha uonevu kwani kimewasababishia usumbufu wa kukwamisha shughuli zao za kiuchumi na kuhoji sababu za kupandisha ushuru kwa kiwango kikubwa hivyo wakati maderevba hao wamekuwa akilipa ushuru katika vituo tofauti tofauti.

Hata hivyo mbali na kuahirishwa kwa zoezi hilo hilo leo, uongozi wa manispaa wamewataka madereva watakaoshindwa kulipia shilingi 2000 kuanzia kesho kutofikisha magari yao kituoni hapo.

Katika hatua nyingine Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Bukoba ilikutana na wamiliki na madereva hao na kufikia uamuzi wa kuendelea kutolewa kwa huduma hiyo kwa ushuru waliokuwa wakilipa wa shilingi 1000.

Kutokana na mazungumzo ambayo yamefanyika katika kituo hicho cha mabasi kati ya kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya na wamiliki wa magari pamoja na madereva  kutozaa matunda ,wameamua kukaa kikao cha pamoja katika ofisi ya mkurugenzi ili kuweza kutafuta muhafaka wa swala hilo.

Biashara
Maoni