Rais wa Benki ya Dunia kung'atuka Februari Mosi

|
Rais wa Benki ya Dunia, (World Bank Group) Jim Yong Kim anayetarajiwa kuachia ngazi Februari Mosi

Rais wa Benki ya Dunia, (World Bank Group) Jim Yong Kim leo ametangaza kung’atuka katika nafasi hiyo ifikapo Februari Mosi baada ya kuhudumu katika nafasi hiyo kwa zaidi ya miaka sita.

Kiongozi huyo mkuu wa benki hiyo anaondoka huku akidai kuiacha taasisi hiyo yenye nguvu kifedha duniani ikiwa imara katika kusaidia jitihada mbalimbali za kifedha na maendeleo duniani.

“Imekuwa ni heshima kubwa kwangu kutumikia kama Rais katika taasisi maarufu zaidi dunia, iliyojaa watu wenye mapenzi ya dhati katika kujitoa kumaliza matatizo ya umasikini uliopitiliza katika maisha yetu ya kila siku,” amesema Kim katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari.

 “Kazi ya Benki ya Dunia kwa sasa ni muhimu kuliko wakati mwingine wowote kutokana na hali ya umasikini kuongezeka duniani, pamoja na matatizo mengi kama mabadiliko ya tabianchi, milipuko ya magonjwa, baa la njaa na suala  wakimbizi ambayo yameendelea kuongezeka katika viwango na ugumu wake.”

Amesema anajisikia vizuri kuondoka katika nafasi hiyo aliyihudumu kama Rais na kusaidia taasisi hiyo kujiweka katika nafasi nzuri licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali.

Chini ya Uongozi wa Kim, kwa ushirikiano kutoka kwa wanachama wa Benki hiyo kutoka nchi 189, taasisi katika mwaka 2012 iliwezesha kuanzisha malengo mawili: moja likiwa ni kumaliza kabisa umasikini ifikapo mwaka 2030 na  kuongeza utajiri huku wakiangazia zaidi nchi zilizopo mwishoni mwa orodha zenye asilimia 40 ya idadi ya watu katika nchi zinazoendelea.

Malengo hayo kwa sasa ndiyo yanayoiongoza na kuijulisha taasisi hiyo katika kazi zake za kila siku duniani.

Utawala
Maoni