Serikali kujadiliana na wauzaji 'boflo' sababu za kupanda kwa bei

|
Mikate ya 'Boflo' inayodaiwa kupanda bei

Wizara ya Biashara na Viwanda Zanzibar unatarajia kukutana na wafanyabiashara  wa mikate ya Boflo ili kujadili kuhusu kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo muhimu kwa matumizi ya chakula visiwani humo.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Hassan Khamis Hafidh wakati ajibu swali la Mwakilishi wa Mpendae Mohamed Said Dimwa katika Baraza la Wakilishi alihoji  kuhusu kupanda bei mikate hiyo.

Akitolea majibu kuhusu swali hilo, naibu waziri huyo amesema, Serikali inafuatilia suala hilo na kesho watakutana na wahusika wa bidhaa hiyo ili kujua sababu za wao kupandisha bei huku wakijua fika kuwa bidhaa hiyo ni kimbilio la wananchi wengi katika maisha yao ya kila siku.

Waziri huyo alisema kuwa biashara Zanzibar ni huria, hivyo kila mwananchi anaweza kufanya biashara kwa mujibu wa uwezo wa kifedha alionao pamoja na kuzingatia sheria za nchi.

Amesema hadi sasa Serikali inaamini kuwa mfumko wa biashara visiswani humo ni wa kuridhisha huku Serikali ikiwa katika juhudi za kuhakikisha biashara zinakuwa zenye maendeleo kwa kuweka miundombinu ya sera na sheria za uendeshaji biashara.

Aidha Naibu huyo aliongeza kuwa serikali iko makini juu ya bei za bidhaa muhimu za chakula kama vile mchele, unga wa ngano na sukari ambapo bidhaa hizo ni muhimu kwa matumizi ya wananchi wa Zanzibar.

Hata hivyo alisema wafanyabiashara hupanga bei za bidhaa zao kulingana na gharama za ununuzi, gharama za usafirishaji kutoka nchi za nje na gharama za kodi wanazolipa katika tasisi za Serikali.

Bei ya mkate mmoja wa Boflo kwa sasa Zanzibar imepanda na kuuzwa kati ya Shilingi 200 hadi 350 wakati bei ya awali ilikuwa shilingi 150 hadi 200.

Chakula
Maoni