Serikali yatangaza kufuta kodi ya VAT kwenye madini

|
Madini tofauti yanayopatikana nchini ambayo yamefutiwa VAT

Serikali imesema imeendelea kutekeleza maelekezo ya Rais John Magufuli aliyoyatoa Januari 22, 2019, alipokutana na wadau wa sekta ya madini na moja ya utekelezaji huo ni kufuta kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na Kodi ya Zuio ya asilimia tano ya mwisho inayotozwa kwenye bei ya kuuzia madini ya aina zote kwa wachimbaji hao.

Hayo yamewekwa bayana na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipokuwa akiahirisha vikao vya Bunge la Kumi na Nne jijini Dodoma leo, Februari 9,2019.

Waziri Mkuu amesema hatua hiyo inatarajiwa kupunguza utoroshwaji wa madini; kuwatambua wachimbaji wadogo kupitia masoko ya madini yatakayoanzishwa pamoja na kusaidia kuwapunguzia gharama wachimbaji wadogo na hivyo kuendesha shughuli zao kwa ufanisi pamoja na kuongeza wigo wa mapato kwa kuwa madini yatauzwa ndani ya nchi.

Nitoe rai kwa wachimbaji wote wadogo kushirikiana na Mamlaka mbalimbali za Serikali kutekeleza maazimio yaliyofikiwa katika kikao na mheshimiwa Rais.”

Amesema siku zote Watanzania wanamuenzi Rais Magufuli, kwa hatua za makusudi anazochukua katika kuhakikisha anaimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato.

Waziri Mkuu amesema Rais Magufuli anafanya hayo yote kwa lengo la kuona Tanzania inapunguza utegemezi wa misaada kutoka katika mataifa mengine.

“Mifano maelekezo aliyoyatoa kwa mawaziri, wakuu wa mikoa wawasilishe mapendekezo kuhusu namna bora ya kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani katika maeneo yao.”

Waziri mkuu amesema tayari Serikali imeshapokea mapendekezo hayo na imetoa maagizo mahsusi kwa TRA na TAMISEMI zishirikiane katika ukusanyaji wa kodi za majengo.

Akizungumzia kuhusu hali ya uchumi, waziri mkuu amesema imeendelea kuimarika, ambapo kati ya Januari hadi Septemba 2018, pato la Taifa lilikua kwa wastani wa asilimia 6.7 ikilinganishwa na asilimia 6.2 katika kipindi kama hicho mwaka 2017.

Amesema Ongezeko hilo la ukuaji wa uchumi limechochewa zaidi na uwekezaji mkubwa kwenye miundombinu hususan ujenzi wa barabara, reli na viwanja vya ndege.

Waziri Mkuu amesema masuala mengine yaliyochangia ukuaji mzuri wa uchumi ni kutengemaa kwa upatikanaji wa nishati na hali nzuri ya hewa kwa upande wa kilimo.

“Shughuli za kiuchumi zilizoendelea kutoa mchango mkubwa katika pato la Taifa kwa kipindi hicho ni kilimo (asilimia 33.4), ujenzi (asilimia 15.7) na biashara (asilimia 10.2).”

Amesema kutokana na umuhimu wa sekta ya kilimo, Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya umwagiliaji, kuhakikisha pembejeo za kilimo zinapatikana kwa wakati.

Pia kuhakikisha huduma za ugani zinaimarishwa katika maeneo yote nchini pamoja na  kuboresha upatikanaji wa miundombinu ya hifadhi na masoko.

Lengo la Serikali ni kuongeza tija kwenye uzalishaji wa mazao ya kilimo na hivyo kumwongezea kipato mkulima kitakachomwezesha kujikimu na kujikwamua na umaskini.

Madini
Maoni