TMRC yazindua mpango wa hatifungani

|
TMRC yazindua mpango wa hatifungani

Kampuni ya Utoaji Mikopo kwa Mabenki na Taasisi za fedha kwa ajili ya mikopo wa nyumba Tanzania (TMRC), leo imezindua mpango wa hatifungani wa miaka mitano kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).  

Uzinduzi huo ulifanywa na Mwenyekiti wa Bodi ya kampuni hiyo Bw. Ammish Owusu-Amoah jijini Dar es Salaam ulishuhudiwa na wawekezaji pamoja na wadau mbalimbali toka sekta za fedha, nyumba na sekta nyingine.

Uzinduzi wa utoaji wa dhamana ya TMRC ulifanyika baada ya TMRC kupokea kibali kwa ajili ya programu ya utoaji wa dhamana ya miaka 5 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 120. Mpango huo ulipata kibali kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Masoko ya Mitaji (CMSA) pamoja na Soko la Hisa (DSE). Kampuni hiyo ya TMRC itaorodheshwa katika soko la hisa la Dar es Salaam.

Aidha, CMSA na DSE, zilijiridhisha kuendelea kwa TMRC kutoa dhamana ya ushirika wake ambayo itakuwa kiasi cha Shilingi Bilioni 12. Afisa Mtendaji Mkuu wa TMRC, Oscar Mgaya alisema "tumepokea vibali vyote muhimu na tunatarajia kwenda kwenye Soko la Hisa kwa mara ya kwanza hivi karibuni".

TMRC ni taasisi maalum ya sekta binafsi ya Fedha ambayo hutoa fedha za muda mrefu kwa taasisi za fedha kwa madhumuni ya mikopo ya nyumba.

Taasisi hii ina lengo la kuunga mkono taasisi za kifedha kutoa mikopo ya nyumbaya muda mrefu ambayo husaidia kushusha marejesho ya kila mwezi na kuwezesha wateja wengi kumudu. Aina hii ya kukopesha pia inajulikana kama mikopo ya jumla.

TMRC inatafuta fedha ili kusaidia shughuli zake za mikopo ya nyumba. "Ilifikiriwa tangu mwanzo kwamba TMRC itapata fedha kutoka kwenye masoko ya mitaji kupitia utoaji wa dhamana kati ya vyanzo vingine" alisema Mgaya. Aliongeza kwamba "Ilikuwa tu suala la muda na sasa ni wakati mzuri kwa sababu riba za soko zimekua zikishuka"

 

Biashara
Maoni