Uamuzi wa Serikali wawaliza mawakala wa simu Uganda

|
Laini za simu zilizopigwa marufuku usajili wake hadi pale UCC itakapowapatia mashine maalum za kutambua usahihi wa taarifa za mhusika

Maelfu ya mawakala wa kampuni za simu nchini Uganda wameilalamikia serikali kufuatia uamuzi wake wa kusimamisha uuzaji wa vifurushi vya simu.

Tume ya Taifa ya Mawasiliano imeamuru kampuni zote za simu kusimamisha uuzaji huo ukiwemo hata wa namba mpya za simu hadi pale watakapopata mashine zilizo na uwezo wa kusoma vitambulisho ikiwa ni miongoni mwa hatua za haraka kukabiliana na uhalifu.

Wakizungumza na Azam TV wafanyabiashara hao wamesema, usitishwaji wa huduma hiyo umekuwa ni wa ghafla huku wao wakiwa tayari na shehena kubwa ya bidhaa hiyo “stock” na tayari wamesema wameshaanza kupata hasara hususan wale wafanyabiashara wadogo.

Kuhusu matumizi ya mashine hizo, kampuni za simu zimesema, licha ya Tume ya Mawasiliano kupitisha zuio hilo lenye lengo la kudhibiti vitendo vya uhalifu vilivyoongezeka hivi karibuni nchini humo, bado mashine hizo hazikabidhiwa kwao na hivyo kutishia kuyumba kwa biashara hiyo ya simu.

Uamuzi huo umekuja kufuati hivi karibuni binti wa miaka 28 kuuawa na wahalifu hao kudaiwa kutumia laini za simu takribani 16 wakati wakifanya madai ya kutaka wapewe fedha kwa lengo la kumwachia binti huyo ambaye hata baada ya fedha hiyo kulipwa walimuua na polisi bado wanaendelea na uchunguzi juu ya watu hao.

Mashine hizo ambazo zinatarajiwa kuanza kutumika nchini humo, zinadaiwa zitasaidia kutambua watumiaji kwa usahihi na uhakika na hivyo kuepusha uhalifu kwa njia ya simu.

Biashara
Maoni