Uholanzi yahoji uhalali wa Rwanda kuidhamini Arsenal ilihali inapokea misaada

|
Wachezaji wa Arsenal wakionyesha jezi zitakazotumia na timu yao kwenye msimu ujao huku mikononi zikiwa na tangazo la "Visit Rwanda" au "Tembelea Rwanda"

Rwanda imetetea uamuzi wake wa kuingia mkataba wa kutangaza utalii wa nchi hiyo kupitia klabu ya Arsenal ya Uingereza.

Utetezi huo umekuja baada ya bunge la Uholanzi kukosoa uamuzi wa serikali ya Rwanda kuidhamini klabu hiyo yenye maskani yake jijini London.

Rwanda na Arsenal zimeingia mkataba wa kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini Rwanda kupitia tangazo maalumu linalosomeka “Visit Rwanda” au “Tembelea Rwanda” ambalo kuanzia msimu ujao timu zote za Arsenal (Ya wanaume, wanawake, watoto nk) zitakuwa zikivaa jezi iliyochapishwa tangazo hilo kwenye sehemu ya juu ya upande wa kushoto.

Hata hivyo Bunge la Uholanzi limehoji uwezo wa Rwanda wa kuidhamini Arsenal wakati nchi hiyo inapokea misaada mbalimbali kwaajili ya kusaidia maendeleo nchini humo.

Mkataba huo wa udhamini unadaiwa kugharimu $40m.

Kufuatia kutoridhishwa na mkataba huo, bunge la Uholanzi limemtaka waziri wa misaada wan chi hiyo, Sigrid Kaag kufuatilia kwa karibu mkataba huo.

Inadaiwa kuwa mmoja wa wabunge wa bunge hilo alidai “inakuwaje nchi inayopokea misaada mingi inakuwa na uwezo wa kuwekeza kiasi kikubwa hivyo.”

Taarifa zinaendelea kudai kuwa mbunge mwingine alidai “Inahuzunisha kuona pesa nyingi kiasi hicho zikilipwa wakati jumuiya ya kimataifa ikijaribu kupambana kuondosha umaskini kwenye nchi hiyo hiyo”

Rwanda ni moja kati ya nchi 15 zinazopata misaada kutoka Uholanzi.

Biashara
Maoni