Wanajeshi Kenya wahudumu wasafiri walikwama JKIA, Kenya

|
Wanajeshi nchini Kenya wakiwa katika Uwanja wa JKIA wakisaidia kuwasikiliza na kuwahudumia wasafari waliokwama uwanjani hapo kufuatia mgomo

Wanajeshi wa nchini Kenya wamechukua jukumu la kutoa huduma katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta kwa lengo la kukabiliana na usumbufu uliojitokeza leo kufuatia  mgomo wa wafanyakazi ulioanza mapema leo Jumatano.

Tangu asubuhi maelfu ya abiria wamejikuta wakikwama kuendelea na safari zao huku baadhi ya ndege zikielekezwa kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam na ndege nyingine zikifuta safari zake.

Mgomo huo unatokana na wafanyakazi hao kupinga mpango wa kuunganisha mamlaka ya usimamizi wa viwanja vya ndege (KAA) na Shirika la Ndege la Taifa (Kenya Airway).

Uwanja huo kwa siku hudaiwa kuhudumia ndege za abiria 120 na kwa leo kwa mujibu wa BBC, walipozungumza na Afisa mkuu Mtendaji wa KQ, Sebastian Mikos takribani  safari 24 za ndege zimeathirika kutokana na mgomo huo.

''Tumekuwa tukiwasiliana na wafanyakazi wote wa KAA tangu saa kumi asubuhi, kwa kweli ni shughuli katika Uwanja wa JKIA na viwanja vingine nchini zimeathirika kutokana na mgomo huo kwa wakati huu tutasema kwamba safari za ndege zimechelewa... safari za ndege 24 zimeathirika'' alisema  Mikos alipozungumza na BBC.

Usafiri
Maoni