Wanasayansi Arusha wainua matumaini ya wakulima wa nyanya

|
Zao la nyanya lapata tumaini la kustawi bila kushambuliwa na wadudu

Wanasayansi katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela mkoani Arusha wamegundua Sumu inayoangamiza wadudu wanaoshambulia mazao ya Jamii ya Nyanya wanaofahamika kitaalamu kama (TUTA APSOLUTA) maarufu kwa jina la "Kantangaze" waliosababisha hasara kubwa kwa wakulima tangu uliporipotiwa nchini mwaka 2014.

Ugunduzi huo ni matokeo ya Utafiti wa Mwanasayansi Mwanamke Neva Mwambela anayechukua masomo ya Shahada ya Uzamivu, Kitengo cha Sayansi ya Maisha na Uhandisi Baiolojia katika taasisi hiyo.

Mwanasayansi Neva anasema imemchukua muda wa miaka mitatu (3) kufanikisha ugunduzi huo na hii ni baada ya dawa nyingi zinazotumiwa na wakulima katika maeneo mbalimbali nchini kushindwa kumuangamiza mdudu huyo.

Wakulima katika eneo la Ngarenanyuki wilayani Arumeru wameiambia Azam Tv kuwa ugunduzi huo unaibua matumaini mapya baada ya kufanya majaribio ya dawa hiyo na kuonekana kuwaangamiza wadudu hao waharibifu.

Profesa Kalor Njau ambaye ni Makamu Mkuu wa Taasisi ya Nelson Mandela anasema ugunduzi huo ni mwanzo tuu na kwamba gunduzi nyingi zitaibuka ili kutimiza malengo ya taasisi yanayojikita kutatua matatizo ya jamii na kukuza viwanda.

Kilimo
Maoni