Latest News
Kim na Kanye watarajia mtoto wa nne

Kim Kardashian amethibitisha kuwa yeye na mumewe Kanye West wanatarajia kupata mtoto wao wa nne.

Kim ameweka wazi kuhusu wawili hao kutarajia kupata mtoto mwingine wa kiume kupitia kwa mama mbadala (surrogate mother) katika mahojiano na kituo cha Runinga cha Marekani.

Kim na mumewe Kanye tayari wamefanikiwa kupata watoto watatu ambao ni North, Saint na Chicago wenye umri kati ya miaka mitano na mwaka mmoja.  Mtoto Chicago pia alizaliwa na mama mbadala baada ya Kim kutahadharishwa na madaktari wake kuwa iwapo atabeba tena ujauzito huenda akahatarisha maisha yake.

Hata hivyo, familia yake Kim imepokea taarifa hizo kwa mshtuko licha ya kwamba hakuweka wazi lini mtoto huyo anatarajiwa kuzaliwa zaidi ya kusema "hivi karibuni".

Latest News
Alikiba na Abdulkiba wapata pigo

Msanii Alikiba na ndugu yake Abdukiba wamepata pigo baada ya kufiwa na baba yao mzazi mzee Saleh Kiba aliyekutwa na mauti katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alipokuwa akipatiwa matibabu.

Taarifa hizi zimethibitishwa na mmoja wa mwanafamilia ya kina Alikiba na kusema kwa sasa msiba upo nyumbani kwao na marehemu anatarajiwa kuzikwa leo, Alhamisi saa 10 za jioni.

 “Ndiyo mzee amefariki na msiba upo nyumbani kwa Mama Alikiba Kariakoo, atazikwa leo saa kumi, kuhusu ugonjwa au chanzo cha kifo hayo ni mambo ya kifamilia siwezi kuyazungumzia” alinukuliwa mmoja wa ndugu wa Alikiba aliyefahamika kwa jina moja Aidan.

Latest News
Mlimbwende wa Algeria 2019 aonja joto la ubaguzi wa rangi

Mrembo aliyeshinda taji la mashindano ya ulimbwende wa Algeria, Khadija Ben Hamou hivi karibuni amewajibu wanaomkashifu kwa maneno ya kibaguzi kutokana na rangi ya ngozi yake.

Mrembo huyo anayetokea katika mkoa wa kusini wa Adrar, amesema anaona fahari ya jinsi alivyo na kuweza kushinda mashindano hayo.

"Nimepata heshima kubwa na nimetimiza ndoto yangu, na ninajisikia nimepewa heshima kubwa na Mkoa wangu wa Adrar ninakotokea," alisema mrembo hayo ambaye ushindi wake umekumbana na maneno ya kashfa ya kibaguzi huku wakosoaji hao wakimkosoa kuhusu rangi ya ngozi yake, pua na midomo katika mitandao ya kijamii ya Facebook na Twitter.

"Sitarudi nyuma kwa sababu ya watu wanaonikosoa," alisema Khadija Ben Hamou alipozungumza na mtandao wa habari nchini  humo wa TSA.

Kwa mujibu wa jarida la mitindo la Vogue, mrembo huyo aliyeshiriki mizunguko 20 kabla ya kuvikwa taji hilo la ulimbwende nchini Algeria Jumamosi iliyopita mwaka huu ni mwanamke wa pili mwenye rangi nyeusi baada ya Nassima Mokadem aliyeshinda mashindano hayo mwaka 2005 nchini humo.

Wanaompinga wanadai kuwa mrembo huyo siyo taswira halisi ya uzuri wa Algeria. Licha ya watu weusi katika nchi hiyo kukumbana na ubaguzi wa rangi wa wazi, mrembo huyo amewapa ushauri wabaguzi hao kwa kuwaeleza kuwa, "usihukumu watu bila wao kujua, hakuna tofauti kati ya weupe na weusi."

Kwa upande wa waandaaji wa mashindano ya Miss Algerie, wamesema kuwa wamesikitishwa na "tabia ya ubaguzi wa rangi na maoni ya watu kadhaa kutokana na machapisho na picha za kutengenezwa".

Latest News
MC Pilipili amvisha pete mchumba wake, amwaga chozi la furaha

Mchekeshaji na mshereheshaji katika shughuli mbalimbali nchini Emmanuel Mathias maarufu kama MC Pilipili ameanza mwaka mpya wa 2019 kwa kumvisha pete mchumba wake anayetarajia kufunga naye ndoa baadaye mwaka huu.

MC Pilipili  kupitia ukurasa wake wa Instagram aliweka picha za tukio hilo la kumvisha pete mchumba wake huyo tukio lililopokelewa kwa hisia tofauti.

Miongoni mwa waliolipokea kwa furaha tukio hilo ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambaye kupitia ukurasa wake wa Instagram alimpongeza Mchekeshaji huyo na kumtaka kuwahamashisha wenzake maarufu kufuata nyayo zake.

“Nakuomba mc Pilipili umsaidie na @diamondplatnumz kwani yeye kila tarehe ikikaribia anasogeza mbele ona sasa anamsubiri Rick Ross aje, sasa sijui ni harusi au Tamasha,” ilisema sehemu ya ujumbe wake

Hata hivyo kiongozi huyo kijana pia alitumia jukwaa hilo kumpongeza mmiliki na mkurugenzi wa E TV na Redio, @Majizo na mchumba wake Elizabeth Michael aka Lulu wanaodaiwa kufungia ndoa yao nchini China.

Amewataka vijana maarufu nchini kuishi maisha yenye uhusiano safi na wenye afya kwa kufuata nyayo za MC Pilipili na wengineo.

Messi aitabiria Juventus ubingwa wa Ulaya msimu huu

Lionel Messi amekiri kuwa kwa mwaka huu klabu ya Juventus ni miongoni mwa timu ambazo zinaweza kuchukua kombe la ligi ya mabingwa ulaya (UEFA Champions League) kutokana na uwepo wa nyota Cristiano Ronaldo katika kikosi cha mabingwa hao wa Serie A.

Messi amesema kuwa kuondoka kwa Ronaldo kwenye kikosi cha Real Madrid kumeifanya timu hiyo kutopewa kipaumbele cha kushinda kombe hilo kwa msimu huu, akiweka wazi kuwa jambo hilo limeidhoofisha klabu hiyo ambayo ni mabingwa watetezi wa kombe hilo.

Akizungumza na Redio Catalunya Messi alisema “Real Madrid ni moja kati ya klabu bora duniani na wana kikosi kikubwa ila ni dhahiri kuwa kutokuwepo kwa Ronlado kunawafanya kupungua ubora na Juventus kuwa na nafasi zaidi ya kushinda Kombe la Mabingwa Ulaya (UEFA),".

“Ilinishangaza kiukweli. Sikufikiria yeye kuondoka Madrid wala kujiunga na Juventus. Kulikuwa na timu nyingi zinamuhitaji. Ilinishangaza, lakini amekwenda kwenye timu nzuri sana.”

Barcelona wamekuwa na mfululizo wa misimu mibaya ya Kombe la Mabingwa Ulaya tangu waliposhinda kombe hilo mwaka 2015. Wametolewa na PSG, Atletico Madrid na AS Roma, mara zote kwenye hatua ya robo fainali. Lakini Messi amejipa moyo kwa kujihakikishai kuwa msimu huu watafanya vizuri.

“Umefika wakati sasa,” alisema, “Tumetolewa katika hatua ya robo fainali kwenye misimu mitatu iliyopita. Matokeo ya msimu uliopita katika jiji la Roma yanaumiza zaidi, lakini tuna kikosi kizuri sana na tunaweza kulipigania (kombe la UEFA).”

Watoto waliopotea Thailand wapatikana pangoni

Vijana kumi na wawili na makocha wao waliokuwa wamenasa katika pango nchini Thailand wamepatikana hai huku wakitakiwa kuanza kufundishwa kuogolea au kusubiri miezi kadhaa kwa mafuriko yaliyopo kupungua kabla ya kutolewa nje ya pango hilo, imesema taarifa ya Jeshi.

Kundi hilo lilitoweka kwa takribani siku tisa na kugunduliwa walipo na waogeleaji wawili kutoka nchini Uingereza, jana Jumatatu katika kiupenyo kidogo kilichopo ndani ya pango hilo lililozingirwa na maji.

Waokoaji kwa sasa wanapambana kuona namna ya kuyavuka maji hayo ili kufikisha mahitaji muhimu kwa kundi hilo.

Watahitaji chakula kitachoweza kuwasaidia katika kipindi cha miezi minne, kwa mujibu wa wanajeshi.

Gavana wa Jimbo la Chiang Rai, Narongsak Osotthanakon amesema, jitihada kadhaa zilifanyika kwa kuunganisha umeme na kufikisha mawasiliano ya simu ndani ya pango hilo kwa ajili ya vijana hao kuzungumza na wazazi wao jambo lililoinua matumaini na kurejesha furaha zaidi.

Waokoaji hao wa Uingereza waliwasili nchini Thailand kwa ajili ya kujiunga na kikosi cha operesheni uokoaji cha nchi hiyo na kufanikiwa kuwapata watoto hao na makocha wao jana usiku.

Vijana hao walionekana kupitia nuru ya tochi wakiwa wamekaa juu ya jiwe lililokuwa ndani ya maji huku wakiwa wanawajibu waogeleaji hao kuwa wote 13 wapo pale na wana njaa sana.