Test
Mchekeshaji Kevin Hart ajitoa kusheheresha Oscar

Mchekeshaji na mwigizaji wa Marekani, Kevin Hart amethibitisha kujitoa katika shughuli ya ushehereshaji wa Tuzo za Oscar mwaka huu kufuatia kauli zake za utata alizodaiwa kuzitoa kupitia twitter kuhusu mapenzi ya jinsia moja.

Kupitia ujumbe wake huo amesema, hataki kuvuruga na asingependa kubadili msimamo wake na kuomba radhi  wote walioumizwa na kauli yake hiyo..

Uamuzi huo wa Hart ulitangazwa Jumanne.

Ujumbe huo ambao unadaiwa kuandikwa muda mrefu umeibuka hivi karibuni na hivyo kuzua mijadala mingi katika mitandao ya kijamii na kupelekea kelele za kutolewa kwake katika ushehereshaji huo.

Aidha, Kevin Hart amesema kusheheresha Tuzo za Oscars ilikuwa " moja ya malengo katika orodha yake ya muda mrefu".

Amesema: "Ninaomba radhi ya dhati kwa Jumuiya ya LGBTQ kwa maneno yangu yaliyowaumiza niliyoyatoa zamani."

Wasanii nyota Diamond na Alikiba wafurahisha mashabiki wao

Baada ya kuwa katika upinzani wa muda mrefu, hatimaye wasanii nyota nchini Tanzania, Diamond Platinum na ALIKIBA wamekutana na kumaliza tofauti zao za muda mrefu.

Hatua hiyo imepokelewa kwa furaha na mashabiki wa pande zote mbili ambao wengi katika mitandao ya kijamii wamepongeza hatua hiyo.

Hivi karibuni, msanii Abdul Nasib maarufu kama Diamond akizungumza na waandishi wa habari, alimkaribisha mwenzake ALIKIBA kujumuika naye katika TAMASHA LA WASAFI 2018 linalotarajiwa kuanza Novemba 24.

Lakini katika kuonesha wawili hao wako tayari kufanya kazi kwa pamoja, ALIKIBA alijibu kupitia ukurasa wake wa Instagram kuwa amepokea mwaliko huo lakini kutokana na muingiliano wa ratiba yake ya kuzindua bidhaa yao ya Mofaya hataweza kushiriki na badala yake ametangaza  kudhamini tamasha hilo kupitia bidhaa hiyo.

“Ndugu zangu #Wasafi tumepata salamu zenu, nashukuru kwa mualiko wenu, ila kwa bahati sitoweza kushiriki kwa sasa kutokana na majukumu ya kuzindua Mofaya katika nchi zingine. Hata hivyo tusingependa kuwaacha hivi hivi, tupo tayari kuwapa support ya kudhamini tamasha lenu kupitia #MofayaEnergyDrink ili kuweza kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya sanaa yetu Tanzania na Africa . Management #RockstarAfrica yangu tutaendelea kuwasiliana nanyi tuweze kufanya hili jambo kubwa.”

Kanye West atangaza kuachana na siasa sasa

Mwanamuziki maarufu nchini Marekani Kanye West amesema kwa sasa  "anajitenga" kutoka kwenye siasa.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter mwanamuziki huyo amedai kuwa “nimekuwa nikitumika kusambaza ujumbe ambao siujui undani wake."

Mwanamuziki huyo amekuwa mfuasi mzuri wa Rais Donald Trump kwa muda mrefu lakini uamuzi huo unaonekana umekuja kufuatia kampeni aliyoingia inayojulikana kama Blexit.

Kampeni hiyo inaratibiwa na mchambuzi mwenye mrengo wa kihafidhina Candace Owens inayowahimiza Wamarekani weusi kujitoa katika Chama cha Democratic.

Mchambuzi huyo amedai kuwa, muziki umekuwa nyenzo nzuri kwaajili ya kampeni hiyo, kitu ambacho rapa huyo kwa sasa amekikanusha.

Mwanamuziki huyo wa nyimbo za kufokafoka aliandika katika ukurasa wake wa twitter pia: "Macho yangu kwa sasa yapo wazi. Ninajitenga mbali kutoka kwenye siasa na kujikita kikamilifu katika ubunifu."

Kwa hatua hiyo inaonekana wazi kuwa Kanye West ameamua kujitoa kabisa katika masuala ya siasa kwa sasa.

Bodi ya Filamu yamfungia Wema Sepetu muda usiojulikana

Bodi ya Filamu Tanzania imemfungia kwa muda usiojulikana, msanii maarufu wa filamu nchini, Wema Sepetu maarufu Madame, kufuatia kusambaza picha zake chafu katika mitandao ya kijamii.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Katibu mtendaji wa Bodi, Joyce Fisso amesema, Wasanii ni vioo vya jamii na kazi yao kubwa ni kuhabarisha, kuonya na kuasa jamii yake kuhusu yale yanayotokea.

Amesema, kutokana na Wema kukiuka maadili, tamaduni na desturi za Kitanzania, Bodi hiyo imeamuru msanii huyo kusimamishwa kujishughulisha na sanaa yeyote inayohusu filamu na uigizaji.

Bodi hiyo imesema imepokea msamaha wa maandishi alioiomba, Bodi, watanzania, wapenzi wa filamu na masahabiki wake, na kwamba wataendelea kufuatilia mienendo yake katika jamii hadi hapo watakapojiridhisha.

Hivi karibuni, msanii huyo kupitia mtandao wake wa Instagram alitupia picha zinazomuonesha akiwa na mwanaume aliyedai kuwa ni mumewe mtarajiwa wakibusiana midomoni jambo ambalo ni kinyume na maadili ya Kitanzania na jana aliomba radhi Umma wa Watanzania na kujutia alichokifanya.

Wasanii miongoni mwa wajumbe wa bodi BASATA

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt Harrison Mwakyembe amewateua wajunbe wapya wa Bodi ya Baraza la Sanaa la Taifa BASATA siku chache baada ya Rais Magufuli kumteua Mwenyekiti mpya wa Bodi hiyo, Habbi Gunze.

Miongoni mwa walioteuliwa ni mwanamuziki Hamis Mwinjuma maarufu 'MwanaFA'  pamoja na Msanii wa filamu, Single Mtambalike maarufu kama 'Richie'.

Wengine walioteuliwa ni pamoja na Asha Mshana, Mwadhiri msaidizi Sanaa UDOM, Dkt. Emmanuel Ishengoma wa Mnadhiri wa Chuo Kikuu Dodoma, Dkt. Saudin Mwakaje mwadhiri Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Uteuzi huo umeanza rasmi tangu Oktoba 5 na watatumikia kwa miaka mitatu.

Rais Museveni hafahamu Kim Kardashian anafanya kazi gani

Rais Yoweri Museveni wa Uganda jana alikutana na kufanya mazungumzo na nyota wa Muziki wa Rap, Kanye West aliyeambatana na mkewe Kim Kardashian.

Wawili hao mara baada ya kumtembelea Rais Museveni katika makazi yake jijini Kampala walimkabidhi zawadi ya raba za lebo ya Yeezy kwa lengo la kuweka kumbukumbu yao katika ziara hiyo.

Wakati wa mazungumzo yao yaliyolenga kuitangaza Uganda kupitia sekta ya Utalii, Rais Museveni alimuuliza mke wa Kanye anajishughulisha na nini kwaajili ya kujikimu na maisha.

Inadaiwa kuwa swali hilo lilitokana na malkia huyo wa kipindi cha maisha halisi cha runinga, mwenye miaka 37 aliyepo nchini humo kuonesha nia ya kutaka kumaliza haraka ziara hiyo.

'Walipokutana na Rais wa Uganda ndipo Rais alipomuuliza Kim, kwanini unataka kuondoka mapema,' moja ya chanzo kiliieleza Daily mail, na ndipo Kim alipomjibu nataka kurejea kazini.

'Rais akamuuliza tena, kazi gani unafanya na Kim, kwa upole akamjibu, anatengeneza shoo ya vipindi vya runinga na dada zake pamoja na familia na wote wanamsubiri yeye arudi.'

Kanye West ajivunia urafiki wake na Trump

Mwanamuziki machachari wa muziki wa kufokafoka maarufu kama RAP Kanye West ameendelea kuthibitisha ‘mahaba’ yake kwa Rais wa sasa wa Marekani Donald Trump baada ya kudai kuwa kofia ya Trump yenye maneno ya “Make America great again” humpa nguvu kama superman.

Mwanamuziki huyo ambaye mara kwa mara ameshindwa kuficha hisia zake kuhusu kumpenda na kumkubali Rais Trump kwa muda mrefu amekuwa akiweka wazi hisia zake kupitia ukurasa wake wa Twitter na mahojiano mbalimbali.

Katika kila unalofanya wapo watakaokuunga mkono na wale watakaokupinga, hata hivyo Kanye West amekuwa akiwazodoa wale wanaomkosoa na kuwataka wamuache awe huru.

Kanye West alialikwa katika Ikulu ya Marekani kwaajili ya chakula cha mchana na kujadili masuala mbalimbali ikiwemo mageuzi katika magereza, ajira na masuala ya wamarekani weusi.

Katika mjadala huo unadaiwa ulijaa vioja vingi kutokana na ukweli kwamba Trump na Kanye wote ni wazungumzaji na hutumia zaidi mtandao kuweka wazi hisia zao.

Katika majadiliano hayo yaliyolenga siasa, mageuzi na uzalishaji, West alinukuliwa akisema "wamejaribu kunitisha, marafiki zangu kuhusu kuvaa hii kofia, lakini hii kofia inanipa nguvu".

Kanye alienda mbali zaidi na kusema kofia hiyo iliyoandikwa "Make America great again" maneno yanayowakilisha kauli mbiu ya utawala wa Donald Trump inamfanya ajionee fahari  na kuongeza kuwa Trump ametengeneza kofia shujaa kwa ajili yake.