Bodi ya Filamu yamfungia Wema Sepetu muda usiojulikana

|
Wema Sepetu aliyefungiwa kwa muda usiojulikana

Bodi ya Filamu Tanzania imemfungia kwa muda usiojulikana, msanii maarufu wa filamu nchini, Wema Sepetu maarufu Madame, kufuatia kusambaza picha zake chafu katika mitandao ya kijamii.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Katibu mtendaji wa Bodi, Joyce Fisso amesema, Wasanii ni vioo vya jamii na kazi yao kubwa ni kuhabarisha, kuonya na kuasa jamii yake kuhusu yale yanayotokea.

Amesema, kutokana na Wema kukiuka maadili, tamaduni na desturi za Kitanzania, Bodi hiyo imeamuru msanii huyo kusimamishwa kujishughulisha na sanaa yeyote inayohusu filamu na uigizaji.

Bodi hiyo imesema imepokea msamaha wa maandishi alioiomba, Bodi, watanzania, wapenzi wa filamu na masahabiki wake, na kwamba wataendelea kufuatilia mienendo yake katika jamii hadi hapo watakapojiridhisha.

Hivi karibuni, msanii huyo kupitia mtandao wake wa Instagram alitupia picha zinazomuonesha akiwa na mwanaume aliyedai kuwa ni mumewe mtarajiwa wakibusiana midomoni jambo ambalo ni kinyume na maadili ya Kitanzania na jana aliomba radhi Umma wa Watanzania na kujutia alichokifanya.

Utawala
Maoni