Buriani nguli wa Afro Jazz Oliver Mtukudzi

|
Mwanamuziki nguli wa nchini Zimbabwe, Oliver Mtukudzi aliyefariki dunia

Mwanamuziki nguli wa nchini Zimbabwe, Oliver Mtukudzi amefariki dunia.

Taarifa hizo zimetolewa leo, kupitia vyombo mbalimbali vya habari na zinadai amefariki leo katika Hospitali ya Avenues mjini Harare baada ya kuugua kwa muda sasa.

Awali katika shughuli zake za muziki, Oliver Mtukudzi amekuwa akifanya ziara mbalimbali kabla ya kuanza kuugua.

Hata hivyo hivi karibuni alilazimika kuahirisha baadhi ya ziara zake za muziki katika mataifa kadhaa duniani kutokana na kuugua kwake.

Mtukudzi atakumbukwa kwa aina yake ya Muziki ya mtindo wa Afro-Jazz uliovuka mipaka na kupata mashabiki wengi kote duniani.

Alipata umaarufu nchini Zimbabwe kabla ya nchi hiyo kupata uhuru mnamo 1980 alipojiunga katika jeshi na muimbaji mwenza wa Zimbabwe anayeishi Marekani, Thomas Mapfumo kwa lengo la kupaza sauti ya mapinduzi wakati ambapo nchi hiyo ilikuwa ikikaliwa na wakoloni chini ya Serikali ya Ian Smith.

Mtukudzi amekuwa katika fani ya muziki kwa zaidi ya miongo minne, na amefanikiwa kutoa albamu 67 huku albamu yake ya mwisho ikiangazia hali ya kisiasa ya sasa nchini Zimbabwe na matatizo ya kijamii.

Nyota huyo wa muziki kutoka Zimbabwe alikuwa akipewa heshima ya muziki wa Afrika kama ilivyo kwa wasanii kama Hugh Masekela, Steve Dyer, Miriam Makeba, Yousssou N dour, Angelique Kidjo, Yvonne Chaka Chaka na Lady Smith Black Mambazo.

Maisha
Maoni