Elizabeth Michael sasa kutumikia kifungo cha nje

|
Elizabeth Michael ambaye ameachiwa kwa msamaha wa Rais

Elizabeth Michael maarufu Lulu aliyekuwa akitumikia kifungo cha miaka miwili jela kwa kosa la kuua bila kukusudia ameachiwa na kutoka katika gereza la Segerea jijini Dar es Salaam ambapo sasa anatumikia kifungo cha nje kwa amri ya Mahakama Kuu.

Uamuzi huo umetangazwa na Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dar es Salaam, Naibu Kamishana wa Magereza Augustino Mboje.

Akizungumza na Azam TV, Naibu Kamishna huyo amesema, Elizabeth maarufu kama Lulu ni miongoni mwa wafungwa 3,319 ambao walipatiwa msamaha wa Rais, Aprili 26 wakati wa maadhimisho ya sherehe za Muungano ambapo kwa upande wake, alipata msamaha wa 1/6.

Lulu ambaye alihukumiwa kifungo cha miaka miwili kwa kosa la kumuua bila kukusudia  aliyekuwa mpenzi wake na mwigizaji wa filamu za kibongo, Steven Kanumba alitakiwa kutoka mwakani lakini kufuatia msamaha huo,  Naibu kamishna huyo amesema, alipaswa kumaliza kifungo chake hicho mwezi Novemba mwaka huu.

Naibu Kamishna huyo amethibitisha kuwa Lulu alitoka gerezani tangu Jumamosi ya Mei 12, na kwamba kwa sasa atatumikia kifungo mbadala kinachojulikana kama  Huduma ya Jamii.

Maisha
Maoni