Test
Miss Mexico atwaa taji la Miss World 2018

Hatimaye mshindi wa Taji la Miss World 2018 ametangazwa huko Sanya na taji hilo limekwenda kwa mrembo kutoka nchini Mexico, Vanessa Ponce De Leon.

Mshindi huyo ametangazwa leo muda mfupi uliopita kufuatia kinyang’anyiro cha warembo 118 kutoka nchi mbalimbali duniani Tanzania ikiwakilishwa na mrembo Queen Elizabeth Makune ambaye hakufanikiwa kuingia hata hatua ya warembo 30 bora.

Mshindi huyo wa mwaka 2018 ambaye pia ni Miss Mexico, ametangazwa kutwaa taji hilo lililokuwa likishikiliwa na Mrembo wa Dunia mwaka jana, Manushi Chhillar kutoka India baada ya kupitia hatua mbalimbali za mashindano hayo.

Mashindano hayo yamefanyika katika ukumbi maarufu uliopo mjini Sanya, China.

Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi na kuvikwa taji zuri na la thamani kutoka kwa Manushi Chhillar mshindi wa mwaka jana, mrembo huyo kutoka Mexico amesema, amefurahi mno kutwaa taji hilo na kukiri mashindano yalikuwa magumu kutokana na kila mrembo kuwa na sifa yake.

Jumla ya warembo 30 waliingia katika fainali hiyo huku warembo watano wakishinda mataji ya vipaji maalum lililoenda kwa Miss Nepal huku mrembo wa Uganda akishinda taji la head to head.

Mchekeshaji Kevin Hart ajitoa kusheheresha Oscar

Mchekeshaji na mwigizaji wa Marekani, Kevin Hart amethibitisha kujitoa katika shughuli ya ushehereshaji wa Tuzo za Oscar mwaka huu kufuatia kauli zake za utata alizodaiwa kuzitoa kupitia twitter kuhusu mapenzi ya jinsia moja.

Kupitia ujumbe wake huo amesema, hataki kuvuruga na asingependa kubadili msimamo wake na kuomba radhi  wote walioumizwa na kauli yake hiyo..

Uamuzi huo wa Hart ulitangazwa Jumanne.

Ujumbe huo ambao unadaiwa kuandikwa muda mrefu umeibuka hivi karibuni na hivyo kuzua mijadala mingi katika mitandao ya kijamii na kupelekea kelele za kutolewa kwake katika ushehereshaji huo.

Aidha, Kevin Hart amesema kusheheresha Tuzo za Oscars ilikuwa " moja ya malengo katika orodha yake ya muda mrefu".

Amesema: "Ninaomba radhi ya dhati kwa Jumuiya ya LGBTQ kwa maneno yangu yaliyowaumiza niliyoyatoa zamani."

Queen Elizabeth kuiwakilisha Tanzania, Miss World

Mwakilishi wa Tanzania katika mashindano ya Miss World, Queen Elizabeth Makune anatarajiwa kuiwakilisha nchi huko mjini Sanya nchini China leo Jumamosi.

Mrembo huyo aliyeshinda katika mashindano ya Miss Tanzania mapema mwaka huu, amekuwa akitajwa katika mitandao ya kijamii kufanya vizuri kwenye shughuli mbalimbali za kijamii licha ya kutopata nafasi ya kuwa miongoni mwa washindani 30 waliofahamika mapema.

Licha ya kampeni mbalimbali katika mitandao ya kijamii zilizohamasisha kumpigia kura mwakilishi huyo wa Tanzania, zoezi hilo halikuweza kumbeba katika shindano la Head to Head lililofanyika mwishoni mwa juma na badala yake ushindi wa taji hilo ulikwenda kwa  mrembo kutoka Uganda, Quiin ABENAKYO na kumwacha mbali Queen Elizabeth licha ya ukweli kuwa ameendelea kujiamini na kung’ara mitandaoni.

Mrembo huyo kutoka Kanda ya Kinondoni hivi karibuni alipata wasaa wa kufanya mahojiano na moja ya kituo cha runinga na kusema amefurahia jukwaa hilo kwani limemsaidia kupata nafasi ya kujitambua na kujitathimini kama mwanamke mwenye ndoto za kubadili maisha yake na alikuwa na Imani ya kuwa Mrembo wa Kwanza kutwaa taji la Miss World.

Hata asiposhinda baadhi ya mashabiki wa mitandaoni wamesema, mahojiano hayo yameonesha uwezo alionao katika kupambanua hoja.

Jumla ya washiriki  113 wanawania taji hilo ambalo kwa sasa linashikiliwa na mrembo kutoka nchini India, Manushi Chhillar ambaye ni mrembo wa sita tangu nchi hiyo ianze kushiriki mashindano hayo ya Miss World.

Mume wa Whitney Houston awashtaki BBC na Showtime

Aliyekuwa mume wa mwanamuziki nyota wa Marekani, marehemu Whitney Houston,  Bobby Brown amekishitaki kituo cha runinga cha BBC na Showtime Networks kwa madai ya kutumia picha za video mwaka 2017 kama Makala iliyopewa jina la Whitney: Can I Be Me bila ridhaa ya wahusika.

Mashtaka hayo yamefunguliwa katika Mahakama ya Wilaya jijini New York, Marekani jana Jumatano na Brown pamoja na wamiliki wa mali za binti yao Bobbi Kristina.

Mlalamika wa mashtaka hayo anadai kuwa, vipande hivyo vya video vimemuathiri yeye Brown, biashara yake pamoja na mali zinazomilikiwa na binti yake, Marehemu Bobbi Kristina.

Washtakiwa ambao ni Showtime, BBC na wakili wa Brown hawajasema chochote kuhusiana na kesi hiyo.

Mwanamuziki huyo wa R&B amesema dhima nzima ya kutumika kwa vipande hivyo vya picha za video haikupewa mtu yoyote kuitumia na kuongeza kuwa kazi hiyo ilipigwa miaka 15 iliyopita . Amesema picha hizo zilichukuliwa kabla ya wawili hao kuachana na marehemu Houston mwaka  2007 na kabla ya kifo chake mwaka 2012.

Mlalamikaji huyo amesema katika taarifa yake kuwa : "Kila mtu ni lazima awe na haki ya kudhibiti na kusimamia utambulisho wao au muonekano binafsi ama sauti au haiba yake katika biashara zinazofanywa na mwingine."

Filamu ama Makala hiyo inadaiwa kuwa ilioneshwa katika tamasha maarufu la Cannes mwaka uliopita na kisha kuoneshwa katika runinga za Showtime pamoja na BBC.

Wasanii nyota Diamond na Alikiba wafurahisha mashabiki wao

Baada ya kuwa katika upinzani wa muda mrefu, hatimaye wasanii nyota nchini Tanzania, Diamond Platinum na ALIKIBA wamekutana na kumaliza tofauti zao za muda mrefu.

Hatua hiyo imepokelewa kwa furaha na mashabiki wa pande zote mbili ambao wengi katika mitandao ya kijamii wamepongeza hatua hiyo.

Hivi karibuni, msanii Abdul Nasib maarufu kama Diamond akizungumza na waandishi wa habari, alimkaribisha mwenzake ALIKIBA kujumuika naye katika TAMASHA LA WASAFI 2018 linalotarajiwa kuanza Novemba 24.

Lakini katika kuonesha wawili hao wako tayari kufanya kazi kwa pamoja, ALIKIBA alijibu kupitia ukurasa wake wa Instagram kuwa amepokea mwaliko huo lakini kutokana na muingiliano wa ratiba yake ya kuzindua bidhaa yao ya Mofaya hataweza kushiriki na badala yake ametangaza  kudhamini tamasha hilo kupitia bidhaa hiyo.

“Ndugu zangu #Wasafi tumepata salamu zenu, nashukuru kwa mualiko wenu, ila kwa bahati sitoweza kushiriki kwa sasa kutokana na majukumu ya kuzindua Mofaya katika nchi zingine. Hata hivyo tusingependa kuwaacha hivi hivi, tupo tayari kuwapa support ya kudhamini tamasha lenu kupitia #MofayaEnergyDrink ili kuweza kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya sanaa yetu Tanzania na Africa . Management #RockstarAfrica yangu tutaendelea kuwasiliana nanyi tuweze kufanya hili jambo kubwa.”

'Endeleeni kuuheshimu utamaduni wetu'

Waziri mkuu, Kassim Majaliwa amewataka Watanzania waendelee kuuheshimu na kuuendeleza utamaduni ambao ndiyo urithi wao ili kulifanya Taifa liendelee kuwa hai.

Amesema suala la kuuenzi utamaduni ni jambo zuri ambalo linatoa fursa kwa watu wengine hususan wa mataifa ya nje kuja kujifunza historia ya Watanzania na maisha yao.

Waziri mkuu aliyasema yao jana jioni Ijumaa, Oktoba 26, alipotembelea shughuli za tamasha la utamaduni wa Mtanzania kwa jamii ya watu wa Lindi.

Katika tamasha hilo linalofanyika kwenye Kijiji cha Makumbusho jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwataka Watanzania kuendelea kuupenda utamaduni wao.

“Nimefurahi kuona nyumba zikiwa na zana mbalimbali za kitamaduni ambazo zilikuwa zikitumiwa na wazee wetu pamoja na namba ya utayarishaji wa vyakula vyetu vya asili.”

“Sikutarajia kuona haya ninayoyaona, nawashukuru wote walioshiriki katika kaandaa tamasha hilo pamoja na uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Kijiji cha Makumbusho.”

Waziri Mkuu alisema tamasha hilo ambalo limewakutanisha Wanalindi kutoka katika wilaya mbalimbali linatoa fursa ya wao pia kujadili maendeleo ya mkoa wao na Taifa kwa jumla.

Kadhalika, Waziri Mkuu aliwaomba wananchi wengi wajitokeze kwa wingi kwenda katika Kijiji cha Makumbusho kwaajili ya kujifunza historia ya Mkoa wa Lindi pamoja na fursa zilizoko.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi alisema mkoa umetumia tamasha hilo kutoa ujumbe kwa umma kuhusu vivutio mbalimbali walivyonavyo pamoja na fursa za uwekezaji.

Bodi ya Filamu yamfungia Wema Sepetu muda usiojulikana

Bodi ya Filamu Tanzania imemfungia kwa muda usiojulikana, msanii maarufu wa filamu nchini, Wema Sepetu maarufu Madame, kufuatia kusambaza picha zake chafu katika mitandao ya kijamii.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Katibu mtendaji wa Bodi, Joyce Fisso amesema, Wasanii ni vioo vya jamii na kazi yao kubwa ni kuhabarisha, kuonya na kuasa jamii yake kuhusu yale yanayotokea.

Amesema, kutokana na Wema kukiuka maadili, tamaduni na desturi za Kitanzania, Bodi hiyo imeamuru msanii huyo kusimamishwa kujishughulisha na sanaa yeyote inayohusu filamu na uigizaji.

Bodi hiyo imesema imepokea msamaha wa maandishi alioiomba, Bodi, watanzania, wapenzi wa filamu na masahabiki wake, na kwamba wataendelea kufuatilia mienendo yake katika jamii hadi hapo watakapojiridhisha.

Hivi karibuni, msanii huyo kupitia mtandao wake wa Instagram alitupia picha zinazomuonesha akiwa na mwanaume aliyedai kuwa ni mumewe mtarajiwa wakibusiana midomoni jambo ambalo ni kinyume na maadili ya Kitanzania na jana aliomba radhi Umma wa Watanzania na kujutia alichokifanya.