Filamu 235 zasajiliwa Tuzo za SZIFF 2019

|
Mlezi wa SZIFF 2019 Jokate Mwegelo (katikati) katika mkutano na wanahabari (hawapo pichani). Kulia kwake ni Mratibu wa SZIFF Sophia Mgaza na kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Oparesheni wa Azam Media, Yahya Mohamed.

Jumla ya filamu 235 zimesajiliwa katika Tamasha la Kimataifa la Tuzo za Sinema Zetu (SZIFF) mwaka 2019, ikiwa ni ongezeko la filamu 121 ikilinganishwa na filamu 114 zilizosajiliwa katika msimu wa kwanza wa tamasha hilo, mwaka 2018.

Taarifa hiyo imetolewa leo na Mratibu wa Tamasha hilo Sophia  Mgaza wakati akizungumza na wanahabari katika ofisi za Azam TV, jijini Dar es Salaam.

Filamu hizo zimesajiliwa kupitia katika vituo vinane ambako wataalamu kutoka Azam TV, Bodi ya Filamu pamoja na COSOTA walitembelea na kukusanya kazi zilizokidhi vigezo, zoezi ambalo lilifanyika kati ya Oktoba 01 – Novemba 30 mwaka huu.

Vituo vilivyotembelewa ni mikoa ya Tanga, Arusha, Tabora, Mwanza, Mbeya, Mtwara, Lindi na Zanzibar. Mbali na mikoa hiyo, zoezi hilo pia liliendeshwa katika nchi za Kenya, Rwanda, Burundi na Congo DR.

Sophia amesema baada ya usajili huo kukamilika, kitakachofuata ni hatua tatu muhimu, ya kwanza ikiwa ni filamu zote zilizosajiliwa kuoneshwa katika runinga kupitia chaneli ya Sinema Zetu kwa muda wa mwezi mmoja ambapo kila siku zitaoneshwa filamu ndefu nne, filamu fupi tatu na tamthilia nne.

Zoezi la filamu hizo kuoneshwa litaanza Januari 01 na kuhitimishwa Januari 31, 2019 na kwa kipindi hicho watazamaji watapata nafasi ya kuzipigia kura hasa vipengelea vya filamu bora na muigizaji bora, kisha majaji watafanya mchujo ili kupata filamu zitakazoingia raundi ya pili.

Hatua ya pili itakuwa ni kuonesha filamu zilizopita katika mchujo wa awali wa majaji (nominated film) zikiwa zimegawanywa katika vipengele 24 vinavyoshindanishwa katika tuzo hizo.

Hatua ya mwisho itakuwa ni usiku wa Tuzo za SZIFF utakaofanyika usiku wa tarehe 23 Februari 2019 katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam ambapo washindi 24 watatangazwa na kupatiwa tuzo pamoja na fedha taslimu.

Filamu
Maoni