Harusi ya Harry na Meghan yazua mjadala Kenya

|
Windsor Golf Hotel and Country Club yajipanga kushiriki kwa mbali harusi ya Prince Harry na mkewe Meghan

Mgahawa mmoja jijini Nairobi umezua mjadala katika mitandao ya kijamii nchini Kenya baada ya kutangaza hafla ya kufuatilia harusi ya mwanamfalme wa Uingereza, Prince Harry na Meghan Markle ambapo wanaotaka kushiriki watatakiwa kulipa Shilingi milioni moja sawa na dola 10,000 za Marekani.

Mgahawa huo unaojulikana kwa jina la Windsor Golf Hotel and Country Club umeandaa hafla hiyo kwa ushirikiano na runinga ya binafsi ya KTN na Kampuni inayotangaza masuala ya sherehe za harusi ya Samantha's Bridal.

Cha kushangaza zaidi wale wote watakaohudhuria sherehe hiyo watatakiwa kuvalia mavazi ya harusi na chakula kitakachopikwa siku hiyo kitakuwa kwa mtindo wa Kiingereza.

Sherehe hiyo inayotarajiwa kufanyika saa 5:30 asubuhi hadi saa 11 jioni ambapo watakaohudhuria watatumbuizwa na kufahamishwa kuhusu yatakayokuwa yakiendelea katika harusi hiyo.

Kwa mujibu wa tangazo la hafla hiyo, kwa wale washiriki walio kwenye uchumba watapata ofa ya kusafirishwa kwa helikopta hadi Mlima Kenya ambapo huko wataweza kujionea jua likichomoza kileleni na kupata kifungua kinywa huko.

Hata hivyo tangazo hilo halijaweka wazi iwapo ni wote watakaopata ofa hiyo ama la.

Baadhi ya Wakenya mtandaoni wameshangazwa na tangazo hilo na kuhoji inawezekanaje mtu akatumia dola 10,000 milioni  'kutazama sherehe kupitia runinga' ilhali fedha hizo zingeweza kugharimia safari ya kwenda hadi Kasri la Windsor na kushuhudia harusi hiyo moja kwa moja.?

Maisha
Maoni