Kanye West atangaza kuachana na siasa sasa

|
Mwanamuziki Kanye West aliyetangaza kujitenga na siasa nchini Marekani

Mwanamuziki maarufu nchini Marekani Kanye West amesema kwa sasa  "anajitenga" kutoka kwenye siasa.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter mwanamuziki huyo amedai kuwa “nimekuwa nikitumika kusambaza ujumbe ambao siujui undani wake."

Mwanamuziki huyo amekuwa mfuasi mzuri wa Rais Donald Trump kwa muda mrefu lakini uamuzi huo unaonekana umekuja kufuatia kampeni aliyoingia inayojulikana kama Blexit.

Kampeni hiyo inaratibiwa na mchambuzi mwenye mrengo wa kihafidhina Candace Owens inayowahimiza Wamarekani weusi kujitoa katika Chama cha Democratic.

Mchambuzi huyo amedai kuwa, muziki umekuwa nyenzo nzuri kwaajili ya kampeni hiyo, kitu ambacho rapa huyo kwa sasa amekikanusha.

Mwanamuziki huyo wa nyimbo za kufokafoka aliandika katika ukurasa wake wa twitter pia: "Macho yangu kwa sasa yapo wazi. Ninajitenga mbali kutoka kwenye siasa na kujikita kikamilifu katika ubunifu."

Kwa hatua hiyo inaonekana wazi kuwa Kanye West ameamua kujitoa kabisa katika masuala ya siasa kwa sasa.

Maisha
Maoni