Korea Kaskazini wakubaliana kushiriki olimpiki Kusini

|
Wajumbe wa Korea Kaskazini na Kusini wakiwa katika mkutano wa pamoja baada ya kushindikana kwa takribani miaka miwili iliyopita

Korea Kaskazini imesema kuwa itatuma ujumbe wake katika michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi 2018 inayotarajiwa kufanyika Korea Kusini mwezi ujao.

Tamko hilo limetolewa wakati ujumbe wa mataifa hayo yalipokutana kwa mazungumzo ya kihistoria baada ya kupita miaka miwili. Ujumbe huo utashirikisha wanariadha na mashabiki.

Korea Kusini pia ilipendekeza kukutanisha familia zilizotenganishwa na vita vya Korea wakati wa michezo hiyo ya majira ya baridi.

Hata hivyo suala hilo lina utata mkubwa miongoni mwa mataifa hayo mawili, kutokana na Korea Kusini kusisitiza familia ziendelee kukutanishwa.

Mpango huo wa kuzikutanisha familia unatarajiwa kufanyika wakati wa likizo ya mwaka mpya, ambayo hufanyika katikati ya michezo ya Pyeongchang.

Mji wa Seoul pia umepekekeza wanariadha wa mataifa hayo ya Korea kufanya gwaride la pamoja katika sherehe ya ufunguzi ya michezo ya Olimpiki.

Bado haijafahamika Korea Kaskazini imejibu nini kuhusu mapendekezo hayo.

Mataifa hayo kwa mara ya mwisho yalifanikiwa kufanya gwaride la pamoja chini ya bendera ya rasi ya Korea takribani miaka zaidi ya 10 iliyopita katika michezo ya olimpiki ya 2006.

Akizungumzia mkutano huo, Waziri wa Muungano wa Korea Kusini , Cho Myoung-Gyon amesema mazungumzo hayo yanajikita zaidi katika masuala ya olimpiki lakini pia hautaacha masuala mengine muhimu kama ya fursa iliyopo ya kuimarisha uhusiano wao.

"Tunahudhuria mkutano huu ili kuzungumzia suala la Korea Kaskazini kushiriki katika mashindano ya Olimpiki ya majira ya baridi yatayofanyika Korea Kusini na kuimarisha uhusiano wa nchi hizi mbili. Ninaelewa kuwa matarajio ya wengi juu ya mkutano huu , kwanza ni kuhusu mawasiliano baina ya nchi hizi mbili ambayo yalisitishwa kwa muda.Tuna lengo la kufanya mashindano haya ya Olimpiki kuwa ya hatua ya kwanza ya kuboresha Amani baina ya nchi hizi mbili hivyo hii ni hatua nzuri na hatuna haraka." alisema Cho Myoung-Gyon.

Mazungumzo hayo yamekuja kufuatia salama za mwaka mpya za kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-Un alizozitoa ambapo aliweka wazi kufungua milango ya majadiliano pamoja na kuweka wazi matamanio yake ya ujumbe wa Korea Kaskazini kushiriki michezo ya Olympiki ya majira ya baridi nchini Korea Kusini mwaka huu, Februari hatua iliyopokelewa kwa shangwe na Korea Kusini na kupanga leo, Jumanne Januari 9 ufanyike mkutano huo .

Utawala
Maoni