Test
Hukumu kesi ya Wema Sepetu, Julai 20

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeahirisha kesi ya dawa za kulevya inayomkabili muigizaji wa filamu nchini, Wema Sepetu hadi Julai 20, 2018 siku ya Ijumaa kwa ajili ya kutoa uamuzi juu ya kesi hiyo.

Hayo yameelezwa mbele ya Mahakama hiyo na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba na kusema sababu kubwa ya kesi hiyo kuahirishwa ni kutaka kupata muda wa kupitia baadhi ya masuala yanayohusiana na kesi ya msanii huyo.

Wema Sepetu anakabiliwa na kesi ya kutumia dawa za kulevya aina ya bangi.

Kylie Jenner amfukuzia tajiri wa Facebook

Nyota wa zamani wa kipindi cha Keeping Up with the Kardashians Kylie Jenner anadaiwa kuwa na utajiri wa thamani ya dola milioni 900 akiwa na umri wa miaka 20 kwa mujibu wa kulingana na Forbes.

Jarida hilo la biashara limesema kuwa nyota huyo wa mtandao wa kijamii anaelekea kuwa bilionea mwenye umri mdogo duniani.

Nyota huyo wa mitindo ambaye ndiye mdogo wa familia ya Kardashian, alizindua Kampuni ya vipodozi miaka miwili iliyopita.

Jenner ambaye hajafikisha miaka hata ya kunywa pombe nchini Marekani atafikisha umri wa miaka 21 mwezi ujao huku toleo jipya la jarida la Forbes likitoa picha yake katika ukurasa wa mbele wa jarida hilo.

Kylie ambaye ni mdogo wa kambo wa Kim Kardashain West mwenye umri wa miaka 37, amempiku dada yake huyo mwenye utajiri wa thamani ya dola takriban milioni 350 ikiwa ni sawa na mara tatu ya kiwango anachomili mtoto huyo wa mwisho wa familia ya Kardashain.

Mapema wiki hii Jenner ambaye ni mama ya mtoto mmoja wa kike kwa jina Stormi alitangaza kuwa atasita kudungwa sindano za kuongeza ukubwa wa midomo yake.

Warembo 16 wajitoa katika Fainali za Miss Burundi 2018

Wasichana 16 kutoka mikoa ya Burundi waliokuwa wamefika kwenye hatua ya fainali ya mashindano ya kumchagua mrembo wa Burundi (Miss Burundi) wamejitoa katika shindalo hilo.

Hatua hiyo sasa inaonekana kutishia uwezekano wa kufanyika kwa shindano hilo la taifa kwa mwaka huu 2018.

Wasichana hao katika waraka wao wamesema, wamefikia uamuzi huo kutokana na kuwepo na sintofahmu kubwa katika maandalizi ya mwaka huu wakitaja baadhi kuwa ni ahadi za atakachotunukiwa mrembo wa kwanza na wa pili.

Mapema iliahidiwa kuwa mshindi angejinyakulia gari jipya na kupewa kiwanja chenye ukubwa wa mita mraba 400. Lakini pia ingeambatana na fedha taslim.

Wasichana hao wamesema, licha ya aahidi hizo bado hawajaona uwezekano wa kutimizwa kwa ahadi hizo na waandaaji ambao ni Shirika la Burundi Event.

Shindano hilo la Miss Burundi lilidhamiriwa kuonyesha utamaduni, uweledi na urembo wa wanawake wa Burundi.

Fainali hiyo ambayo ilipangwa kufanyika Julai 21 kwa sasa  imeahirishwa na shirika hilo la Burundi Event limetangaza kuwa imesogezwa mbele hadi Julai 28. Na haijafahamika iwapo wataendesha mchakato mwingine wa kuwapata warembo wa shindano hilo ama la.

Washiriki wa Urembo watakiwa kuzingatia maadili ya kitanzania

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Juliana Shonza ametoa wito kwa washiriki wa mashindano ya urembo  nchini kuzingatia maadili na tamaduni za kitanzania  kwa kuwa kielelezo bora kwa jamii .

Shonza ameyasema hayo jijini Arusha wakati wa shindano la kumtafuta mrembo wa Jiji hilo, yaliyoshirikisha warembo 19.

“ Ninyi  ni kioo cha jamii, mnaangaliwa na jamii nzima hivyo msibweteke mnapopata umaarufu bali muwe kielelezo bora cha utamaduni na maadili ya Kitanzania.” amesema Juliana Shonza .

Naibu waziri huyo akafafanua zaidi kuwa sanaa ya urembo ni ajira kama zilivyo ajira nyingine,na kuwaomba wazazi na jamii kutoa ushirikiano wa karibu katika kuhakikisha mabinti hao wanatimiza ndoto zao katika sanaa hiyo.

Aidha amesema, Serikali haitasita kuwachukulia hatua wale wote watakaojihusisha  na vitendo vya unyanyasaji na uzalilishaji kwa washiriki wa mashindano hayo.

Naibu waziri huyo pia hakuacha kuzungumzia yaliyopita baada ya mashindano hayo kuingia doa na kusimamishwa kwa kipindi cha mwaka mmoja kutokana na madai ya kuwepo kwa ubabaishaji na kukiukwa wa taratibu na sheria za kuendesha mashindano hayo.

“Serikali ilichukua uamuzi wa kumfutia leseni mwendeshaji wa awali, ila kwa sasa yamefunguliwa tena na jukumu hili linasimamiwa na Basila Mwanukuzi naamini tutaona mabadiliko mazuri katika tasnia hii,” amesema Shonza.

Katika mashindano ya kumtafuta mrembo wa kuwakilisha Mkoa wa Arusha kwenye mashindano ya kitaifa yalishuhudia mrembo Rukia Mhona akiibuka mshindi, huku nafasi ya pili ikichukuliwa na Teddy Mkenda na nafasi ya tatu ikienda kwa Belinda Matemu.

Wengi wamlilia mtoto maarufu mitandaoni 'Patda smart boy'

Mtoto wa msanii wa Filamu za Bongo na Mjasiriamali, Rose Alphonce maarufu kama 'Muna Love' ameaga Dunia.

Mtoto Patrick Dickson ambaye alikua na umaarufu mwingi katika mitandao ya kijamii amefariki jana Julai 3 nchini Kenya alipokuwa akipatiwa matibabu.

Patrick alianza kuugua tangu mwaka 2016 ambapo alisumbuliwa zaidi na maradhi ya mguu hali iliyompelekea kushindwa kutembea.

Kuanzia hapo Patrick alilazwa na kufanyiwa upasuaji mara kadhaa kwa lengo la kutafuta suluhu ya afya yake.

Mwaka 2017, Patrick alirejea tena na kuonekana akiwa na afya nzuri japo alikuwa akichechemea mguu mmoja.

Aliweka wazi kuwa ameokoka kwa kurusha video akihubiri neno la Mungu, pia alionekana na wasanii mbalimbali wa muziki wa Injili kama vile Joel Lwaga, Chris Shalom na Jimmy Psalmist.

Mpaka sasa kupitia mitandao ya kijamii watanzania mbalimbali waliopo ndani na nje ya nchi wanahamasishana kuchanga fedha ili kumsaidia mama yake aweze rejesha mwili wa Patrick Tanzania kwaajili ya mazishi.

Patrick maarufu kama Patda smart boy, alikuwa ni mtoto mwenye vipaji mbalimbali kama vile mwigizaji na mwana mitindo.

Mkurugenzi wa tamasha la Sheffield afariki dunia

Mkurugenzi wa Tamasha maarufu la Sheffield Tramlines amefariki dunia akiwa na miaka 36.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, waratibu wa tamasha hilo wamesema, Sarah Nulty amefariki dunia kufuatia  "kuumwa kwa muda mfupi".

Tamasha hilo la Tramlines lilizinduliwa rasmi mwaka 2009 kwa usaidizi wa mwanamke huyo, na kufanikiwa kuvutia mashabiki  wa muziki takribani  35,000.

Baada ya mafanikio yaliyopatikana tangu kuanza kwake, aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Tamasha hilo mwaka 2013.

Waratibu wa tamasha hilo wamemuelezea Nulty kama "uhai na roho ya  Tramlines" na kutoa heshima zao kwa "jasiri, mwenye maono na asiyevunja miiko ya kazi".

Nulty alijiunga na Sheffield kama mwanafunzi mwaka 1999 na kufanya kazi katika klabu za usiku ikiwemo Gatecrasher  na Bed, kabla ya kufanikiwa kusimamia shughuli kadhaa zilizokuwa zikifanyika mubashara katika maeneo tofauti kwenye mji huo nchini Uingereza.

Waratibu wa tamasha hilo wamesema,: "Sarah alijitoa kikamilifu katika kazi yake ya kuandaa matamasha ya muziki kwenye mji wa Sheffield.

Nyota wa muziki Marekani Cheryl na Liam Payne watengana rasmi

Wanamuziki  Cheryl na mpenzi wake Liam Payne wametangaza kuachana rasmi baada ya kuwa katika uhusiano wao uliodumu kwa miaka miwili.

Mwanamuziki huyo nyota wa lililokuwa kundi la  Girls Aloud (35) na mpenzi wake  mwanachama wa One Direction  (24), wanadaiwa kuachana wiki mbili zilizopita  kwa mujibu wa gazeti la Sun.

Wawili hao walifanikiwa kupata mtoto wa kiume pamoja aliyepewa jina la Bear, ambaye alizaliwa mwezi Machi mwaka jana.

Wamethibitisha kutengana kwao huko kupitia mtandao wa kijamii na kusema, " ni masikitiko” na ilikuwa ngumu kwao "kufanya uamuzi huo mzito", na kuongeza kuwa : "Bado tunao upendo mkubwa kwa kila mmoja wetu kama familia".

Cheryl katika ukurasa wake wa Twitter aliandika: "Bear ni dunia yetu na tunawaomba muheshimu faragha yake wakati tukiangalia njia ya kupita katika hili pamoja."