Test
Kashfa za ngono zazidi kumharibia R.Kelly Marekani

Mwanamuziki wa Marekani, Robert Kelly maarufu R. Kelly na mmiliki wa lebo ya Sony wameafikiana kuachana katika uhusiano wao wa kikazi, vyombo vya habari nchini Marekani vimeripoti.

Kupitia tovuti mbalimbali nchini humo zimevinukuu vyanzo tofauti vikidai kuwa wawili hao waliafikiana kuhusu mpango wa uamuzi huo pasipo kutangazwa rasmi.

Taarifa zaidi zinadai kuwa kutengana huko kumekuja kufuatia kashfa ya ngono ya miongo kadhaa iliyomuhusisha mshindi huyo wa Tuzo ya Grammy mwenye miaka 52, shutuma ambazo amekuwa akizikanusha wakati wote.

Shutuma hizo zimechukuliwa na kutengenezewa Makala iliyopewa jina la  ‘Surviving R Kelly’, iliyozinduliwa mapema mwezi huu.

Makala hiyo ina sehemu sita zilizolenga wanawake waliodai kudhalilishwa kingono na mwanamuziki huyo kwa miaka mingi sasa.

Licha ya umaarufu na mafanikio katika kazi zake za muziki wa R & B, R.Kelly 2008 alishtakiwa kwa makosa hayo lakini baadaye alipatikana hana kosa kuachiwa huru. 

Mrembo wa El Salvador atembelea vivutio vya utalii nchini

Mwanamitindo maarufu nchini Marekani ambaye pia ni mrembo wa El Salvador mwaka 2018,  Marisela De Montecristo amewasili nchini kwa shughuli za utalii akilenga kutembelea vivutio kadhaa vya utalii.

Mrembo huyo ambaye ameambatana na mchumba wake pamoja na mama yake walipokewa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa KIA na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira.

Watalii hao wanatarajia kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Tarangile na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kabla ya kwenda visiwani Zanzibar.

Hii ni mara ya kwanza kwa mrembo huyo kuzuru Afrika na amejitolea kuwa Balozi wa Tanzania katika masuala ya utalii ambapo Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro amesema ugeni huo ni hatua mojawapo inayoleta heshima kwa Tanzania.

Kim na Kanye watarajia mtoto wa nne

Kim Kardashian amethibitisha kuwa yeye na mumewe Kanye West wanatarajia kupata mtoto wao wa nne.

Kim ameweka wazi kuhusu wawili hao kutarajia kupata mtoto mwingine wa kiume kupitia kwa mama mbadala (surrogate mother) katika mahojiano na kituo cha Runinga cha Marekani.

Kim na mumewe Kanye tayari wamefanikiwa kupata watoto watatu ambao ni North, Saint na Chicago wenye umri kati ya miaka mitano na mwaka mmoja.  Mtoto Chicago pia alizaliwa na mama mbadala baada ya Kim kutahadharishwa na madaktari wake kuwa iwapo atabeba tena ujauzito huenda akahatarisha maisha yake.

Hata hivyo, familia yake Kim imepokea taarifa hizo kwa mshtuko licha ya kwamba hakuweka wazi lini mtoto huyo anatarajiwa kuzaliwa zaidi ya kusema "hivi karibuni".

Alikiba na Abdulkiba wapata pigo

Msanii Alikiba na ndugu yake Abdukiba wamepata pigo baada ya kufiwa na baba yao mzazi mzee Saleh Kiba aliyekutwa na mauti katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alipokuwa akipatiwa matibabu.

Taarifa hizi zimethibitishwa na mmoja wa mwanafamilia ya kina Alikiba na kusema kwa sasa msiba upo nyumbani kwao na marehemu anatarajiwa kuzikwa leo, Alhamisi saa 10 za jioni.

 “Ndiyo mzee amefariki na msiba upo nyumbani kwa Mama Alikiba Kariakoo, atazikwa leo saa kumi, kuhusu ugonjwa au chanzo cha kifo hayo ni mambo ya kifamilia siwezi kuyazungumzia” alinukuliwa mmoja wa ndugu wa Alikiba aliyefahamika kwa jina moja Aidan.

Mlimbwende wa Algeria 2019 aonja joto la ubaguzi wa rangi

Mrembo aliyeshinda taji la mashindano ya ulimbwende wa Algeria, Khadija Ben Hamou hivi karibuni amewajibu wanaomkashifu kwa maneno ya kibaguzi kutokana na rangi ya ngozi yake.

Mrembo huyo anayetokea katika mkoa wa kusini wa Adrar, amesema anaona fahari ya jinsi alivyo na kuweza kushinda mashindano hayo.

"Nimepata heshima kubwa na nimetimiza ndoto yangu, na ninajisikia nimepewa heshima kubwa na Mkoa wangu wa Adrar ninakotokea," alisema mrembo hayo ambaye ushindi wake umekumbana na maneno ya kashfa ya kibaguzi huku wakosoaji hao wakimkosoa kuhusu rangi ya ngozi yake, pua na midomo katika mitandao ya kijamii ya Facebook na Twitter.

"Sitarudi nyuma kwa sababu ya watu wanaonikosoa," alisema Khadija Ben Hamou alipozungumza na mtandao wa habari nchini  humo wa TSA.

Kwa mujibu wa jarida la mitindo la Vogue, mrembo huyo aliyeshiriki mizunguko 20 kabla ya kuvikwa taji hilo la ulimbwende nchini Algeria Jumamosi iliyopita mwaka huu ni mwanamke wa pili mwenye rangi nyeusi baada ya Nassima Mokadem aliyeshinda mashindano hayo mwaka 2005 nchini humo.

Wanaompinga wanadai kuwa mrembo huyo siyo taswira halisi ya uzuri wa Algeria. Licha ya watu weusi katika nchi hiyo kukumbana na ubaguzi wa rangi wa wazi, mrembo huyo amewapa ushauri wabaguzi hao kwa kuwaeleza kuwa, "usihukumu watu bila wao kujua, hakuna tofauti kati ya weupe na weusi."

Kwa upande wa waandaaji wa mashindano ya Miss Algerie, wamesema kuwa wamesikitishwa na "tabia ya ubaguzi wa rangi na maoni ya watu kadhaa kutokana na machapisho na picha za kutengenezwa".

MC Pilipili amvisha pete mchumba wake, amwaga chozi la furaha

Mchekeshaji na mshereheshaji katika shughuli mbalimbali nchini Emmanuel Mathias maarufu kama MC Pilipili ameanza mwaka mpya wa 2019 kwa kumvisha pete mchumba wake anayetarajia kufunga naye ndoa baadaye mwaka huu.

MC Pilipili  kupitia ukurasa wake wa Instagram aliweka picha za tukio hilo la kumvisha pete mchumba wake huyo tukio lililopokelewa kwa hisia tofauti.

Miongoni mwa waliolipokea kwa furaha tukio hilo ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambaye kupitia ukurasa wake wa Instagram alimpongeza Mchekeshaji huyo na kumtaka kuwahamashisha wenzake maarufu kufuata nyayo zake.

“Nakuomba mc Pilipili umsaidie na @diamondplatnumz kwani yeye kila tarehe ikikaribia anasogeza mbele ona sasa anamsubiri Rick Ross aje, sasa sijui ni harusi au Tamasha,” ilisema sehemu ya ujumbe wake

Hata hivyo kiongozi huyo kijana pia alitumia jukwaa hilo kumpongeza mmiliki na mkurugenzi wa E TV na Redio, @Majizo na mchumba wake Elizabeth Michael aka Lulu wanaodaiwa kufungia ndoa yao nchini China.

Amewataka vijana maarufu nchini kuishi maisha yenye uhusiano safi na wenye afya kwa kufuata nyayo za MC Pilipili na wengineo.

Tabia za Harmonize zamkimbiza meneja wake

Mmoja wa mameneja hodari wa muziki nchini Joel Vincent maarufu kama Puaz amethibitisha kuachana na Kundi la Muziki la Wasafi (WCB) baada ya kutokea kutoelewana na mwanamuziki Harmonize.

Kwa mujibu wa meneja huyo kupitia mazungumzo yake na mitandao ya kijamii, amesema, ameamua kumalizana na mwanamuziki huyo kufuatia kukosekana kwa maelewano baina yao katika biashara.

Puaz ameushukuru uongozi wa Wasafi kwa ushirikiano na fursa mbalimbali walizompatia kwa kipindi chote walichofanyakazi pamoja kujivunia mafanikio aliyoyapata mwanamuziki huyo huku yeye akiwa ni msaada mkubwa kwake.

Amesema, awali wakati akianza kazi na Harmonize alikuwa ni kijana mstaarabu lakini kadri siku zilivyokuwa zikisonga, mwanamuziki huyo aliyekiri kuwa anajituma alianza kubadilika suala alilodai kuwa huenda ni kutokana na mafanikio aliyoyapata na kwamba hana kinyongo naye na wala nia ya kumchafua.

Puaz amesema katika maisha licha ya kumtengeneza Harmonize kuwa ‘Brand’ inayouzika ameshindwa kuendelea kuvumilia tabia kadhaa za mwanamuziki huyo zikiwemo za dharau na kiburi na hivyo kuona ni bora afanye masuala yake.

''Naelewa kwamba ni kijana mdogo ambaye ametoka katika familia masikini, lakini utajiri na umaarufu aliopata kutokana na mafanikio ya muziki wake umeathiri tabia yake.

''Niliketi chini na Diamond Platinumz na kumuelezea yaliojiri na tukakubaliana kwamba sitaendelea kusimamia tena muziki wa Harmonize''. alisema  Puaz.

Kabla ya kuwa meneja wa Harmonize Puaz aliwahi kumsimamia mwanamuziki wa mtindo wa Rap nchini Shetta.

Akishirikiana na Harmonize kama maneja wake Puaz alihusika katika kuuza nyimbo kama vile DM Chick akimshirikisha msanii Sarkodie, Khadamshi ulioimbwa na Duly Syke, Nitarudi mbali na Kwangwaru uliogonga vichwa vya habari.