Miss Mexico atwaa taji la Miss World 2018

|
Vanessa Ponce De Leon (katikati) alitwaa taji la Miss World 2018 akiwa na washindi wenzake wa pili na watatu

Hatimaye mshindi wa Taji la Miss World 2018 ametangazwa huko Sanya na taji hilo limekwenda kwa mrembo kutoka nchini Mexico, Vanessa Ponce De Leon.

Mshindi huyo ametangazwa leo muda mfupi uliopita kufuatia kinyang’anyiro cha warembo 118 kutoka nchi mbalimbali duniani Tanzania ikiwakilishwa na mrembo Queen Elizabeth Makune ambaye hakufanikiwa kuingia hata hatua ya warembo 30 bora.

Mshindi huyo wa mwaka 2018 ambaye pia ni Miss Mexico, ametangazwa kutwaa taji hilo lililokuwa likishikiliwa na Mrembo wa Dunia mwaka jana, Manushi Chhillar kutoka India baada ya kupitia hatua mbalimbali za mashindano hayo.

Mashindano hayo yamefanyika katika ukumbi maarufu uliopo mjini Sanya, China.

Akizungumza mara baada ya kutangazwa mshindi na kuvikwa taji zuri na la thamani kutoka kwa Manushi Chhillar mshindi wa mwaka jana, mrembo huyo kutoka Mexico amesema, amefurahi mno kutwaa taji hilo na kukiri mashindano yalikuwa magumu kutokana na kila mrembo kuwa na sifa yake.

Jumla ya warembo 30 waliingia katika fainali hiyo huku warembo watano wakishinda mataji ya vipaji maalum lililoenda kwa Miss Nepal huku mrembo wa Uganda akishinda taji la head to head.

mitindo
Maoni