Test
Messi aitabiria Juventus ubingwa wa Ulaya msimu huu

Lionel Messi amekiri kuwa kwa mwaka huu klabu ya Juventus ni miongoni mwa timu ambazo zinaweza kuchukua kombe la ligi ya mabingwa ulaya (UEFA Champions League) kutokana na uwepo wa nyota Cristiano Ronaldo katika kikosi cha mabingwa hao wa Serie A.

Messi amesema kuwa kuondoka kwa Ronaldo kwenye kikosi cha Real Madrid kumeifanya timu hiyo kutopewa kipaumbele cha kushinda kombe hilo kwa msimu huu, akiweka wazi kuwa jambo hilo limeidhoofisha klabu hiyo ambayo ni mabingwa watetezi wa kombe hilo.

Akizungumza na Redio Catalunya Messi alisema “Real Madrid ni moja kati ya klabu bora duniani na wana kikosi kikubwa ila ni dhahiri kuwa kutokuwepo kwa Ronlado kunawafanya kupungua ubora na Juventus kuwa na nafasi zaidi ya kushinda Kombe la Mabingwa Ulaya (UEFA),".

“Ilinishangaza kiukweli. Sikufikiria yeye kuondoka Madrid wala kujiunga na Juventus. Kulikuwa na timu nyingi zinamuhitaji. Ilinishangaza, lakini amekwenda kwenye timu nzuri sana.”

Barcelona wamekuwa na mfululizo wa misimu mibaya ya Kombe la Mabingwa Ulaya tangu waliposhinda kombe hilo mwaka 2015. Wametolewa na PSG, Atletico Madrid na AS Roma, mara zote kwenye hatua ya robo fainali. Lakini Messi amejipa moyo kwa kujihakikishai kuwa msimu huu watafanya vizuri.

“Umefika wakati sasa,” alisema, “Tumetolewa katika hatua ya robo fainali kwenye misimu mitatu iliyopita. Matokeo ya msimu uliopita katika jiji la Roma yanaumiza zaidi, lakini tuna kikosi kizuri sana na tunaweza kulipigania (kombe la UEFA).”

Watoto waliopotea Thailand wapatikana pangoni

Vijana kumi na wawili na makocha wao waliokuwa wamenasa katika pango nchini Thailand wamepatikana hai huku wakitakiwa kuanza kufundishwa kuogolea au kusubiri miezi kadhaa kwa mafuriko yaliyopo kupungua kabla ya kutolewa nje ya pango hilo, imesema taarifa ya Jeshi.

Kundi hilo lilitoweka kwa takribani siku tisa na kugunduliwa walipo na waogeleaji wawili kutoka nchini Uingereza, jana Jumatatu katika kiupenyo kidogo kilichopo ndani ya pango hilo lililozingirwa na maji.

Waokoaji kwa sasa wanapambana kuona namna ya kuyavuka maji hayo ili kufikisha mahitaji muhimu kwa kundi hilo.

Watahitaji chakula kitachoweza kuwasaidia katika kipindi cha miezi minne, kwa mujibu wa wanajeshi.

Gavana wa Jimbo la Chiang Rai, Narongsak Osotthanakon amesema, jitihada kadhaa zilifanyika kwa kuunganisha umeme na kufikisha mawasiliano ya simu ndani ya pango hilo kwa ajili ya vijana hao kuzungumza na wazazi wao jambo lililoinua matumaini na kurejesha furaha zaidi.

Waokoaji hao wa Uingereza waliwasili nchini Thailand kwa ajili ya kujiunga na kikosi cha operesheni uokoaji cha nchi hiyo na kufanikiwa kuwapata watoto hao na makocha wao jana usiku.

Vijana hao walionekana kupitia nuru ya tochi wakiwa wamekaa juu ya jiwe lililokuwa ndani ya maji huku wakiwa wanawajibu waogeleaji hao kuwa wote 13 wapo pale na wana njaa sana.

Dada wa kiongozi wa Korea Kaskazini ashangaza dunia kwa ulinzi

Dada wa Kiongozi wa Korea Kaskazini amekuwa mtu wa kwanza katika familia ya utawala wa nchi hiyo kuzuru Korea Kusini tangu kumalizika kwa vita kati ya nchi hizo mbili ya mwaka 1950 hadi 1953.

Mwanafamilia huyo ni sehemu ya ujumbe mzito unaohudhuria sherehe za ufunguzi wa michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi inayofanyika jijini Pyeongchang.

Kim Yo Jong ametumia ndege ya kaka yake, Kim Jong U akiwa ameambatana na mfalme wa nchi hiyo Kim Yong Nam mwenye umri wa miaka tisini na kuzingirwa na ulinzi wa kutisha.

 

Viongozi hao mara baada ya kuwasili walipokelewa na rais wa nchi hiyo wenyeji wa michezo ya Olympiki, Rais Moon Jae-in kabla ya kushiriki ufunguzi wa michezo hiyo iliyofufua uhusiano wa nchi hizo mbili zilizokuwa kwenye uhusiano wa kusuasua kwa muda mrefu.

Kim Yo Jong ametumia ndege ya kaka yake, Kim Jong U akiwa ameambatana na mfalme wa nchi hiyo Kim Yong Nam mwenye umri wa miaka tisini.

Watakuwepo Korea Kusini kwa siku tatu na wanatarajiwa kukutana na Rais Moon Jae-in kesho Jumamosi katika hafla itakayofanyika Ikulu.

 

Dada wa kiongozi Korea kaskazini kuhudhuria Olimpiki

Dada wa Kiongozi wa Korea Kaskazini na mwenye ushawishi mkubwa kwa kaka yake, Kim Jong-un anatarajiwa kuhudhuria sherehe za ufunguzi wa michezo ya Olimpiki zitakazofanyika Ijumaa,  taarifa hiyo imethibitishwa.

Kim Yo-jong ni mtoto mdogo wa marehemu kiongozi Kim Jong-il na jukumu lake liliongozeka wakati alipopandishwa cheo na kuwa kiongozi wa masuala ya sera ndani ya chama (politburo).

Nchi hizo mbili za Korea zimekubaliana kupita na bendera moja katika sherehe hizo za ufunguzi.

Ushiriki wa Kaskazini katika mashindano hayo, unaonekana kama suluhu ya mwanzo ya kuimarisha uhusiano wa nchi hizi mbili.

Hata hivyo wataalamu wa mambo wanasema, ukaribu huo hauoneshi kuwepo kwa matokeo chanya kuhusu matamanio ya kutengeneza nuklia kwa Kaskazini.

Kim Yo-jong, na  Kim Jong-un, ni ndugu waliozaliwa na mama mmoja, ambaye ataongozana na kiongozi mkuu wa Kaskazini, Kim Yong-nam, ambaye ushirika wake ulitangazwajuma lililopita.

Zaidi ya wajumbe 280 kutoka nchini Korea Kaskazini wakiwemo viongozi wa Timu ya ushangiliaji, wameshawasili nchini humo, jana Jumatano kwa majira yao.

Polisi wapambana na waandamanaji Korea kusini

Kumetoka maandamano huko Korea Kusini muda mfupi kabla ya kuwasili kwa Meli ya Korea Kaskazini katika bandari ya Mukho ikiwa na watu 140 wa kundi la sanaa.

Polisi wameonekana wakiwasukuma waandamanaji hao na kuleta tafrani ya aina yake bandarini hapo.

Nchi mbili majirani za Korea Kusini na Kaskazini zimekuwa zikifanya jitihada mbalimbali za kushirikiana hasa katika kipindi hiki cha michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi ili kupunguza ukali wa mzozo baina yao kutokana na mipango ya Korea Kaskazini ya makombora ya nyuklia.

Mamia ya Polisi wenye ngao za kujikinga, walikuwa kwenye bandari hiyo kuzuia waandamanaji hao waliofika wakati wa kuwasili kwa meli hiyo huku wakipeperusha bendera ya nchi yao ya Korea kusini na ile ya Marekani na kuimba wimbo wa Taifa wa Korea Kusini.

Katika bendera hizo hakukuonekana bendera ya Umoja wa nchi hizo za Korea kama ilivyotarajiwa kufuatia makubaliano ya kubeba bendera moja kwenye ufunguzi wa michezo hiyo ya Olimpiki inayotarajiwa kufunguliwa Ijumaa, kama kuonesha kufikia hitimisho la uhasama wa miaka takribani 16.

Korea Kaskazini wakubaliana kushiriki olimpiki Kusini

Korea Kaskazini imesema kuwa itatuma ujumbe wake katika michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi 2018 inayotarajiwa kufanyika Korea Kusini mwezi ujao.

Tamko hilo limetolewa wakati ujumbe wa mataifa hayo yalipokutana kwa mazungumzo ya kihistoria baada ya kupita miaka miwili. Ujumbe huo utashirikisha wanariadha na mashabiki.

Korea Kusini pia ilipendekeza kukutanisha familia zilizotenganishwa na vita vya Korea wakati wa michezo hiyo ya majira ya baridi.

Hata hivyo suala hilo lina utata mkubwa miongoni mwa mataifa hayo mawili, kutokana na Korea Kusini kusisitiza familia ziendelee kukutanishwa.

Mpango huo wa kuzikutanisha familia unatarajiwa kufanyika wakati wa likizo ya mwaka mpya, ambayo hufanyika katikati ya michezo ya Pyeongchang.

Mji wa Seoul pia umepekekeza wanariadha wa mataifa hayo ya Korea kufanya gwaride la pamoja katika sherehe ya ufunguzi ya michezo ya Olimpiki.

Bado haijafahamika Korea Kaskazini imejibu nini kuhusu mapendekezo hayo.

Mataifa hayo kwa mara ya mwisho yalifanikiwa kufanya gwaride la pamoja chini ya bendera ya rasi ya Korea takribani miaka zaidi ya 10 iliyopita katika michezo ya olimpiki ya 2006.

Akizungumzia mkutano huo, Waziri wa Muungano wa Korea Kusini , Cho Myoung-Gyon amesema mazungumzo hayo yanajikita zaidi katika masuala ya olimpiki lakini pia hautaacha masuala mengine muhimu kama ya fursa iliyopo ya kuimarisha uhusiano wao.

"Tunahudhuria mkutano huu ili kuzungumzia suala la Korea Kaskazini kushiriki katika mashindano ya Olimpiki ya majira ya baridi yatayofanyika Korea Kusini na kuimarisha uhusiano wa nchi hizi mbili. Ninaelewa kuwa matarajio ya wengi juu ya mkutano huu , kwanza ni kuhusu mawasiliano baina ya nchi hizi mbili ambayo yalisitishwa kwa muda.Tuna lengo la kufanya mashindano haya ya Olimpiki kuwa ya hatua ya kwanza ya kuboresha Amani baina ya nchi hizi mbili hivyo hii ni hatua nzuri na hatuna haraka." alisema Cho Myoung-Gyon.

Mazungumzo hayo yamekuja kufuatia salama za mwaka mpya za kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-Un alizozitoa ambapo aliweka wazi kufungua milango ya majadiliano pamoja na kuweka wazi matamanio yake ya ujumbe wa Korea Kaskazini kushiriki michezo ya Olympiki ya majira ya baridi nchini Korea Kusini mwaka huu, Februari hatua iliyopokelewa kwa shangwe na Korea Kusini na kupanga leo, Jumanne Januari 9 ufanyike mkutano huo .

George Weah ashinda uchaguzi wa rais Liberia

Mwanasoka bora wa zamani wa dunia, George Weah ametangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa rais katika mzunguko wa pili.

Weah ambaye alishinda kwenye mzunguko wa kwanza uliokuwa na wagombea zaidi ya 10 kwa kupata 38% ya kura zote lakini hakutangazwa kuwa rais wa nchi hiyo kwasabbau katiba ya nchi hiyo inataka mshindi wa kiti cha urais apate kura zinazoanzia 50% ya kura zote.

Weah anakuwa rais wa kwanza wa Afrika ambaye amewahi kutwaa tuzo kubwa za soka duniani ikiwemo tuzo ya mchezaji bora wa dunia.

Tume ya uchaguzi nchini Liberia ilimtangaza Weah kuwa mshindi wa mzunguko wa pili wa uchaguzi huo kwa kujikusanyia zaidi ya 61% huku mpinzani wake Joseph Boakie akipata 38.5% ya kura.

Wafuasi wa Weah walionekana wakishangilia kwenye mji mkuu wa Monrovia wakati matokeo yalipokuwa yakiendelea kutangazwa na tume hiyo.

Kwenye mzunguko wa pili Weah alikuwa akipambana na makamu wa rais wa nchi hiyo Boakie  ambaye amehudumu kwenye nafasi hiyo kwa zaidi ya miaka 10 chini ya uongozi wa rais wa kwanza mwanamke barani Afrika aliyeshika wadhifa huo kwa kuchaguliwa, Ellen Johnson Sirleaf.