Test
Eto'o akanusha uvumi uliosambazwa

Msakata kabumbu nyota, raia wa Cameroon, Samuel Eto'o amekanusha kuhusu uvumi ulioenea katika mitandao ya kijamii kuwa, ameahidi kugawa fedha kwa wahamiaji haramu walioko Libya iwapo watakubali kurejea nyumbani sanjari na kukodi ndege binafsi.

Amewataka wanaofanya hivyo kuwekeza zaidi katika upendo dhidi ya udhalimu wa kupenda fedha pamoja na kulijenga bara la Afrika kwa kusaidia wenye uhitaji na wale wanaonyimwa utu. 

Hivi karibuni kumekuwepo na taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii zikidai kuwa Eto'o ameahidi kuwapa fedha watakaokubali kurejea Cameroon taarifa zilizosambazwa na picha zinazoonyesha wacameroon na raia wengine wa Afrika magharibi wakiuzwa huko Libya.

“Ninachoweza kusema ni kwamba kaka zangu wapendwa na dada zangu ni wakati sasa wa kusisitiza upendo utawale uovu badala ya kudhani fedha inaweza kutatua matatizo tuliyonayo.”

Akaongeza kuwa, “ Tuache kupoteza muda wetu adhimu katika vitu vya kufurahisha kwaajili ya mateso na maumivu ya wengine, na tusaidia kuwazuia ndugu zetu wasipoteze utu wao.”

Amesema , siyo wakati wa kulaumu wakati kulikuwa na uwezekano wa kuzuia kutokana na wanaofanya hivyo wengi wao ni ndugu, jirani au jamaa.

Mahakama yamuongezea kifungo Oscar Pistorius

Mahakama nchini Afrika Kusini, imemuongezea muda wa kifungo mshindi na mkimbiaji wa mbio za Olympiki, Oscar Pistorius kwa kosa la kumua mpenzi wake kutoka miaka mitano ya awali hadi kumi na mitatu na miezi mitano.

Waendesha mashtaka wa serikali katika kesi hiyo ndiyo waliopinga adhabu hiyo ya miaka sita ya awali kwa madai kuwa ilikuwa adhabu ‘nyepesi’ kwa mauaji ya Reeva Steenkamp

Msemaji wa familia ya Steenkamp amesema, uamuzi huo uliotolewa sasa  "umethibitisha kuwa hali imetendeka".

Pistorius amedaiwa kuwa alimpiga risasi iliyomuua Steenkamp siku ya Valentine mwaka 2013 kwa bahati mbaya baada ya kudhani ni mhalifu.

Mahakama hiyo kuu ya Bloemfontein imempunguzia adhabu iliyopaswa kuwa miaka 15 kwa madai kuwa tayari alishatumikia kifungo hicho kwa mujibu wa sheria ya Afrika kusini.

Wakati wa uamuzi wa hukumu hiyo, mwanamichezo huyo hakuwepo mahakamani.

Mwaka 2014, katika hukumu ya awali mwanamichezo huyo alihukumiwa miaka mitano jela kwa kosa la kuua bila kukusudia baada ya kupatikana na hatia na mwaka 2015 ilikatwa rufaa kupinga adhabu hiyo.

Kucheza muziki kunasaidia ubongo kutozeeka

Utafiti mpya umeonesha kuwa mazoezi rahisi ikiwemo kutembea, kucheza dansi kunaweza kupunguza zaidi uzeekaji wa ubongo.

Utafiti wa awali umeonesha mazoezi yanaweza kuusaidia ubongo kupambana na uzeekaji, lakini haukuonesha mazoezi ya aina gani ni mazuri zaidi.

Kwa mujibu wa utafiti huo mpya, umelinganisha mazoezi ya aina mbili tofauti yaani kucheza dansi na mazoezi ya uvumilivu.  Matokeo hayo yameonesha kuwa kucheza dansi ni kuzuri zaidi.

Watafiti wa Ujerumani wamewashirikisha wazee waliojitolea wenye umri wa wastani wa miaka 68, na katika utafiti wa miezi 18, wazee hao wote walijifunza kucheza dansi au kufanya mazoezi ya uvumilivu kila wiki.

Katika ufuatiliaji wa matokeo kikundi cha mazoezi ya uvumilivu kilitakiwa kurudia kufanya mazoezi ambayo ni pamoja na kupanda baiskeli na kutembea.

Nacho kikundi cha kucheza dansi kilitakiwa kujifunza mtindo mpya wa dansi kila wiki.

Kutokana na uangalizi wa eneo la Hippocampus la ubongo, mazoezi hayo mawili yote yaliweza kuinua uwezo wa eneo hilo, lakini kucheza dansi kuliinua zaidi uwezo wa uwiano wa wazee hao na hivyo kudhihirisha kuwa kucheza dansi kunatoa mchango katika mapambano dhidi ya uzeekaji wa ubongo.

Eneo la hippocampus ni eneo linalohusiana na uwezo wa kumbukumbu, ufahamu na uwiano.

Katika mchakato wa uzeekaji, udhoofishaji wa uwezo wa eneo la hippocampus unaweza kusababisha kupungua kwa uwezo wa ufahamu na uwezo wa mazoezi.

LEBRON ALAANI MCHORO WA UBAGUZI WA RANGI KATIKA NYUMBA YAKE

Mchezaji nyota wa kikapu katika ligi ya NBA, LeBron James, amezungumzia mkasa wa kubaguliwa kutokana na rangi yake baada ya nyumba yake mjini Los Angeles kuchorwa neno linalomdhalilisha mtu mweusi.

"Bila kujali una pesa kiasi gani, bila kujali wewe ni maarufu kiasi gani... kuwa mweusi hapa Marekani si jambo rahisi," alisema.

Taarifa ilitolewa polisi kuhusu mchoro huo siku ya Jumatano na nyota huyo wa Cleveland Cavaliers alizungumza baadaye.

Maafisa wa polisi wa Los Angeles wamevithibitishia vyombo vya habari kuhusu ubaya wa mchoro huo.

Polisi wanajaribu kufuatilia kamera za usalama waweze kubaini mhusika.

James amezungumza kutoka San Francisco, ambako timu yake inafanya mazoezi kujiandaa na mechi ya kwanza ya fainali za NBA.