Rais Magufuli aguswa na kifo cha msanii King Majuto

|
Marehemu Amri Athuman maarufu King Majuto enzi za uhai wake

Rais John Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe kufuatia kifo cha msanii mkongwe nchini Mzee Amri Athuman maarufu kwa jina la King Majuto kilichotokea jana Agosti, 08 Jijini Dar es Salaam.

King Majuto alifariki dunia jana Jumatano, saa 1:30 jioni katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu.

Katika salamu hizo, Rais Magufuli amemtaka Dkt. Mwakyembe kufikisha salamu zake za pole kwa familia ya marehemu, wasanii wote nchini, wadau wa sanaa, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na kifo cha King Majuto.

Rais Magufuli amesema King Majuto atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa na wa muda mrefu alioutoa kupitia sanaa ya uigizaji na uchekeshaji, ambapo alishiriki kuelimisha jamii, kuendeleza na kukuza sanaa na kuunga mkono juhudi za chama na Serikali katika kuhimiza maendeleo.

"King Majuto alikuwa kielelezo cha safari ndefu ya sanaa kwa nchi yetu, kwa muda wote amedhihirisha kipaji, ujuzi na uwezo wa hali ya juu katika uigizaji na uchekeshaji na hivyo kuwa kipenzi cha Watanzania na wasanii wenzake, hatutasahau ucheshi wake, upendo na uzalendo kwa nchi yake wakati wote wa uhai wake" ilisema sehemu ya taarifa ya Rais Magufuli.

Rais Magufuli amesema anaungana na familia na wote walioguswa na kifo cha King Majuto katika kipindi hiki cha majonzi na amemuombea kwa Mwenyezi Mungu apumzike mahali pema peponi, Amina.

Kabla ya kukumbwa na mauti, taarifa za kuanza kuugua kwake zilianza kuenea tangu mwanzoni mwa mwaka huku na kisha kusafirishwa kwenda nchini India, kwaajili ya matibabu zaidi.

Akiwa katika Hospitali ya Tumaini, King Majuto aliwahi kutembelewa na viongozi mbalimbali akiwemo Rais John Magufuli na mkewe Janeth, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, Waziri wa Michezo na Utamaduni,, Dkt. Harrison Mwakyembe pamoja na viongozi wengine kadhaa na wasanii wenzake ambao walikuwa wakimtakia uponyaji wa haraka.

Katika mitandao ya kijamii, wasanii wenzake na watu maarufu waliandika kwenye kurasa zao kuonesha kuguswa na msiba huo.

Maisha
Maoni