Tabia za Harmonize zamkimbiza meneja wake

|
Mwanamuziki Harmonize wakati wa mahusiano mazuri na meneja wake, Joel Vincent

Mmoja wa mameneja hodari wa muziki nchini Joel Vincent maarufu kama Puaz amethibitisha kuachana na Kundi la Muziki la Wasafi (WCB) baada ya kutokea kutoelewana na mwanamuziki Harmonize.

Kwa mujibu wa meneja huyo kupitia mazungumzo yake na mitandao ya kijamii, amesema, ameamua kumalizana na mwanamuziki huyo kufuatia kukosekana kwa maelewano baina yao katika biashara.

Puaz ameushukuru uongozi wa Wasafi kwa ushirikiano na fursa mbalimbali walizompatia kwa kipindi chote walichofanyakazi pamoja kujivunia mafanikio aliyoyapata mwanamuziki huyo huku yeye akiwa ni msaada mkubwa kwake.

Amesema, awali wakati akianza kazi na Harmonize alikuwa ni kijana mstaarabu lakini kadri siku zilivyokuwa zikisonga, mwanamuziki huyo aliyekiri kuwa anajituma alianza kubadilika suala alilodai kuwa huenda ni kutokana na mafanikio aliyoyapata na kwamba hana kinyongo naye na wala nia ya kumchafua.

Puaz amesema katika maisha licha ya kumtengeneza Harmonize kuwa ‘Brand’ inayouzika ameshindwa kuendelea kuvumilia tabia kadhaa za mwanamuziki huyo zikiwemo za dharau na kiburi na hivyo kuona ni bora afanye masuala yake.

''Naelewa kwamba ni kijana mdogo ambaye ametoka katika familia masikini, lakini utajiri na umaarufu aliopata kutokana na mafanikio ya muziki wake umeathiri tabia yake.

''Niliketi chini na Diamond Platinumz na kumuelezea yaliojiri na tukakubaliana kwamba sitaendelea kusimamia tena muziki wa Harmonize''. alisema  Puaz.

Kabla ya kuwa meneja wa Harmonize Puaz aliwahi kumsimamia mwanamuziki wa mtindo wa Rap nchini Shetta.

Akishirikiana na Harmonize kama maneja wake Puaz alihusika katika kuuza nyimbo kama vile DM Chick akimshirikisha msanii Sarkodie, Khadamshi ulioimbwa na Duly Syke, Nitarudi mbali na Kwangwaru uliogonga vichwa vya habari.

Maisha
Maoni