Waigizaji Chipukizi wang'ara Tuzo za Filamu Sziff2019

|
Washindi wa Kiume na Kike wa Sziff2019, Rashid Msigala na Flora Kihomba kutoka Filamu ya Tamaa

Waigizaji chipukizi kutoka katika  Filamu ya Kesho, Rashid Msigala na Flora Kihomba jana walijikuta wakitwaa tuzo za uigizaji Bora kwa upande wa kiume na kike huku wakiwaangusha wakongwe wa Filamu nchini katika kipengele cha waigizaji Bora wa filamu nchini.

Mbali na washindi hao, nayo Filamu ya SIYABONGA iliibuka kidedea kwa kutwaa Tuzo ya Filamu Bora kwa mwaka 2019 kupitia Tuzo za Kimataifa za Sinema Zetu (Sziff) zilizofanyika jana usiku, kwenye Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Flora Kihombo katika kipengele hicho cha Tuzo ya Muigizaji Bora wa Kike aliwabwaga manguli kama Wema Sepetu, Monalisa, Johari na wengine waliokuwa katika kinyang’aniro hicho.

Naye Rashid aliwabwaga masupa staa kama Hemed ,Salim Ahmed aka Gabo Zigamba ambaye licha ya kukosa tuzo hiyo ya mwigizaji bora wa kiume alishinda tuzo nyingine katika vipengele vya filamu bora ya Siyabonga na Filamu bora ya kitaifa ya Siyabonga.

Washindi wengine ni kutoka kipengele cha upande wa filamu fupi, ambapo mshindi wa Tuzo  Bora ya Cinematograph ilikwenda kwa Adam Juma katika Filamu ya Tamaa, Tuzo ya  Muongozaji Bora ikienda kwa Said Yusuf kupitia filamu ya Tamaa wakati Tuzo ya mchezo bora wa kuigiza ikienda kwa Christine Pande kutokana na filamu ya Supa Mama na Tuzo ya Uhariri Bora  ikinyakuliwa na Ibrahim Jabir wa Tamaa.

Tuzo nyingine zilizotolewa ni kwa upande wa Muziki Bora wa Asili ambayo imekwenda kwa Roger Mugabirwe katika filamu ya Sisi na Wao huku Christine Pande akitwaa Tuzo ya Filamu Bora ya Supa Mama.

Aidha Tuzo hizo pia zilienda kwa filamu bora za mikoani ambapo mikoa ya Arusha, Lindi, Mbeya, Morogoro, Mtwara na Mwanza waliibuka kidedea kupitia filamu zao zilizoingia katika kinyang’anyiro hicho.

Kwa upande wa tuzo katika kipengele cha Makala, Adam Juma amejikuta akijizolea tuzo ya Muongozaji Bora wa Makala pamoja na Filamu bora kupitia Makala yake ya WWR/AMKA.

Katika Tukio hilo la Sziff 2019, Tuzo nyingine zilizotolewa ni katika vipengele vya Filamu fupi bora, Makala bora, tamthilia bora ambayo tuzo zake zimenyakuliwa na Tamthilia ya Safari yangu.

Tamasha
Maoni