Warembo 16 wajitoa katika Fainali za Miss Burundi 2018

|
Miss Burundi 2018 wajitoa mashindano ya fainali

Wasichana 16 kutoka mikoa ya Burundi waliokuwa wamefika kwenye hatua ya fainali ya mashindano ya kumchagua mrembo wa Burundi (Miss Burundi) wamejitoa katika shindalo hilo.

Hatua hiyo sasa inaonekana kutishia uwezekano wa kufanyika kwa shindano hilo la taifa kwa mwaka huu 2018.

Wasichana hao katika waraka wao wamesema, wamefikia uamuzi huo kutokana na kuwepo na sintofahmu kubwa katika maandalizi ya mwaka huu wakitaja baadhi kuwa ni ahadi za atakachotunukiwa mrembo wa kwanza na wa pili.

Mapema iliahidiwa kuwa mshindi angejinyakulia gari jipya na kupewa kiwanja chenye ukubwa wa mita mraba 400. Lakini pia ingeambatana na fedha taslim.

Wasichana hao wamesema, licha ya aahidi hizo bado hawajaona uwezekano wa kutimizwa kwa ahadi hizo na waandaaji ambao ni Shirika la Burundi Event.

Shindano hilo la Miss Burundi lilidhamiriwa kuonyesha utamaduni, uweledi na urembo wa wanawake wa Burundi.

Fainali hiyo ambayo ilipangwa kufanyika Julai 21 kwa sasa  imeahirishwa na shirika hilo la Burundi Event limetangaza kuwa imesogezwa mbele hadi Julai 28. Na haijafahamika iwapo wataendesha mchakato mwingine wa kuwapata warembo wa shindano hilo ama la.

mitindo
Maoni