Washiriki wa Urembo watakiwa kuzingatia maadili ya kitanzania

|
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Juliana Shonza akiwa katika picha ya pamoja na washindi wa Miss Arusha

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Juliana Shonza ametoa wito kwa washiriki wa mashindano ya urembo  nchini kuzingatia maadili na tamaduni za kitanzania  kwa kuwa kielelezo bora kwa jamii .

Shonza ameyasema hayo jijini Arusha wakati wa shindano la kumtafuta mrembo wa Jiji hilo, yaliyoshirikisha warembo 19.

“ Ninyi  ni kioo cha jamii, mnaangaliwa na jamii nzima hivyo msibweteke mnapopata umaarufu bali muwe kielelezo bora cha utamaduni na maadili ya Kitanzania.” amesema Juliana Shonza .

Naibu waziri huyo akafafanua zaidi kuwa sanaa ya urembo ni ajira kama zilivyo ajira nyingine,na kuwaomba wazazi na jamii kutoa ushirikiano wa karibu katika kuhakikisha mabinti hao wanatimiza ndoto zao katika sanaa hiyo.

Aidha amesema, Serikali haitasita kuwachukulia hatua wale wote watakaojihusisha  na vitendo vya unyanyasaji na uzalilishaji kwa washiriki wa mashindano hayo.

Naibu waziri huyo pia hakuacha kuzungumzia yaliyopita baada ya mashindano hayo kuingia doa na kusimamishwa kwa kipindi cha mwaka mmoja kutokana na madai ya kuwepo kwa ubabaishaji na kukiukwa wa taratibu na sheria za kuendesha mashindano hayo.

“Serikali ilichukua uamuzi wa kumfutia leseni mwendeshaji wa awali, ila kwa sasa yamefunguliwa tena na jukumu hili linasimamiwa na Basila Mwanukuzi naamini tutaona mabadiliko mazuri katika tasnia hii,” amesema Shonza.

Katika mashindano ya kumtafuta mrembo wa kuwakilisha Mkoa wa Arusha kwenye mashindano ya kitaifa yalishuhudia mrembo Rukia Mhona akiibuka mshindi, huku nafasi ya pili ikichukuliwa na Teddy Mkenda na nafasi ya tatu ikienda kwa Belinda Matemu.

mitindo
Maoni