Bill Gate tajiri aliyekatisha shule kufuata ndoto zake

|
Bill Gate tajiri aliyechukia shule na kufuata ndoto zake

Kwa kawaida watu wengi duniani wanaimani kwamba mtu anapoacha shule basi maisha yake ndiyo yanakuwa yameharibika.

Lakini Imani hiyo inaonekana siyo sahihi pale unapomzungumzia tajiri maarufu duniani Bill Gates.

Tajiri huyu aliyezaliwa Oktoba 28 mwaka 1955 katika familia ya William Henry Gates III na Mary Maxwell, Seattle Washington. Bill Gates alilelewa katika familia yenye uwezo wa kiasi pamoja na dada zake wawili; Kristianne ambaye ni mkubwa kwake na mdogo wake Libby.

Familia ya Gates ilikuwa inaishi kwa ukarimu na ukaribu zaidi, watoto wote watatu walihimizwa kuwa watu wa ushindani na wenye kupigania kilicho bora.

Bill alionyesha dalili za mwanzo kuwa na ushindani wakati akiratibu michezo ya kukimbia ya kifamilia katika majira ya kiangazi.

Akiwa na umri wa miaka kati ya 11 au 12, wazazi wake Bill walianza kuwa na wasiwasi juu ya tabia yake. Alikuwa akifanya vizuri shuleni, lakini alionekana kuchoka na kuacha mara kwa mara kitendo kilichowatia hofu wazazi wake.

Wazazi wake walikuwa wanaimani kubwa kwenye elimu ya Umma, Bill alipokuwa na umri wa miaka kumi na tatu, wazazi wake walimuandikisha katika Shule ya Lakeside, Seattle na katika shule hiyo Bill Gate alifaulu takribani masomo yote yakiwemo Hesabu, sayansi, uigizaji na kiingereza.

Tajiri huyo alikutana na Paul Allen katika Shule ya Lakeside, ambaye alikuwa amempita Bill kiumri kwa miaka miwili.  Wawili hao wakaanza urafiki wa haraka na pia wote walijikuta ni wenye shauku juu ya masuala ya tarakinishi (computer)

Mwaka 1970, Bill akiwa na umri wa miaka kumi na tano alianzisha biashara na rafiki yake, Paul Allen. Walizindua “Traf-o-Data,” progamu ya tarakinishi (computer) inayohusu uangalizi wa trafiki huko Seattle, walifanikiwa kupata Dola za Marekani 20,000 kwa jitihada zao.

Gates alitaka kuanzisha kampuni yake ila wazazi wake walimtaka amalize shule na kwenda chuo ambapo walitumai ya kuwa atakuja kufanya kazi kama mwanasheria, alijiunga na chuo cha Havard akiwa anasomea sheria.

Mtaalamu huyo wa ‘Microsoft’ alikuwa bado anawasiliana na rafiki yake Paul Allen, ambaye alisoma Chuo kikuu cha Washington kwa miaka miwili, na kuacha shule na kuhamia Boston, Massachusetts na kuanza kazi Honeywell.

Mwaka 1975, Gates na Allen waliunda ushirikiano wao na kuuita “Micro-Soft.”

Mwaka 1976, Bill Gates alianzisha Microsoft na kuingia mkataba na MITS (Micro Instrumentation and Telemetry Systems) Microsoft walifanya kazi kwa bidii  ya kuuza mfumo wa uendeshaji katika kampuni nyingine. Hatimaye ‘Microsoft’ walipata nafasi ya utengenezaji wa progamu.

Bill Gates alimuoa Melinda Ann French mwaka 1994 na walifanikiwa kupata watoto watatu ambao ni Jennifer (1996), Rory (1999) na Phoebe (2002)

Katika harakati zao za kimaisha Bill Gates na mke wake Melinda Gates walianzisha Taasisi inayoitwa “Bill&Melinda Foundation”

Gates alipata msaada kutoka kwa mwekezaji, Warren Buffet ambae alichangia Dola bilioni 17 kupitia taasisi hiyo.

Inakadiriwa kwamba taasisi ya Gates na mkewe Melinda imechangia msaada wa Dola za kimarekani bilioni 28 ikiwemo Dola bilioni nane ili kuboresha afya za watu mbalimbali ulimwenguni.

Katika mahojiano yake na gazeti la Daily Telegraph, Gates alisema licha ya kuwa na fedha nyingi ataiachia familia yake asilimia ndogo ya utajiri  wake  huku fedha nyingine akizitoa kwa watu wengine.

 

Maisha
Maoni