BINTI MFALME WA JAPAN AKUBALI KUACHA NAFASI HIYO AOLEWE

|
Binti Mfalme

Mjukuu wa kike wa Mfalme Akihito wa Japan, Binti Mfalme Mako, amekubali kupoteza hadhi na haki zote za umalkia ili aweze kuolewa na mpenzi wake, waliyekutana tangu akiwa chuo kikuu.

Taarifa zilizotangazwa jana na kituo cha televisheni cha umma, NHK, juu ya uamuzi huo wa Binti Mfalme Mako zimeitikisa Japan nzima.

Magazeti, televisheni, redio na mitandao ya kijamii imeamka ikiwa na habari hiyo, huku uchumba rasmi ukitazamiwa kutangazwa wiki chache kutoka sasa.

Mchumba wake, Kei Komuro, ni kijana wa miaka 25 aliyewahi kupewa jina la “Mwanamfalme wa Bahari” katika mashindano ya kushajiisha utalii hivi karibuni.

Mwanamume huyo kutoka familia ya watu wa kawaida, amezungumza na waandishi wa habari muda mfupi uliopita, ambapo amekwepa kabisa kuzungumzia suala la uchumba, akisema kuwa atasema “pale tu muda utakapowadia.”

Habari za uchumba huu zimezuwa mashaka makubwa sio tu juu ya nafasi ya mwanamke kwenye ukoo wa kifalme, bali pia mustakabali wa ufalme huo, ambao kwa mara ya kwanza ndani ya karne mbili zilizopita utachukua hatua ya kumuondoa madarakani mfalme aliye hai katika wakati ambapo warithi wa kiume ni wachache.

Mako, ambaye pia ana umri wa miaka 25, ni binti mkubwa wa Mwana Mfalme Akishino, ambaye ni mtoto wa pili wa kiume wa Mfalme Akihito, na kama ilivyo kwa wanafamilia wote wa kike wa ufalme huo, anapoteza hadhi na haki yake ya kifalme kwa kuolewa na mtu wa kawaida, kutokana na sheria zao.

Hata hivyo, sheria hiyo haiwahusu wanaume, ambapo Akihito na wanawe wameowa watu wa kawaida, na ambao sasa ni sehemu ya ufalme.

Maisha
Maoni