Test
Mugabe amzawadia shemeji yake wa kike zawadi ya dola 60,000

Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe amemzawadia shemeji yake wa kike zawadi ya dola za kimarekani  60,000 kama zawadi ya kuzaliwa, kwa mujibu wa gazeti la serikali la Herald.

Taarifa zinasema kuwa, zawadi hiyo ilitolewa kama shukrani pia kwa Junior Gumbochuma, ambaye ni dada mkubwa wa mke wa rais huyo kwaajili ya kumsaidia kulea watoto wake.

Kwa mujibu wa gazeti hilo la Herald, rais alitumia nafasi hiyo ya sherehe za kuzaliwa shemeji yake huyo ambaye ni mchungaji kukosoa mahubiri ya kanisa la Pentecostal alilodai linawaibia waumini wao fedha kwa kutengeneza miujiza, kanisa ambalo shemeji yake huyo anachunga.

Wakati akitoa zawadi hiyo, wadadisi wa mambo wanasema uchumi wa Zimbabwe kwa sasa uko mahututi huku nchi hiyo ikishuhudia upungufu wa fedha kwa kiwango kikubwa hususani noti za dola ambazo zimekuwa zikitumika kama fedha halali za nchi hiyo, huku kwa sasa ikibakia sarafu moja tu inayozunguka nchini humo.

Nelson Mandela 'shujaa' anayeendelea kukumbukwa duniani

Miongoni mwa majina makubwa ambayo kamwe hayatasagaulika duniani ni jina la mwanaharakati, mpigania uhuru, mwana ukombozi na mwana siasa mkongwe Hayati Rolihlahla Nelson Mandela.

Rolihlahla Mandela alizaliwa Julai 18, 1918 kwenye ukoo wa Madiba katika Kijiji cha Mvezo, Transkei. Nonqaphi Nosekeni na Nkosi Mphakanyiswa Gadla Mandela ni wazazi wa Nelson.

Mandela alisoma katika Shule ya Msingi ya Qunu ambapo mwalimu wake Mdingane alimpa jina la Nelson Mandela.

Baada ya elimu ya awali Mandela aliendelea na masomo ya Shahada yake ya kwanza ya Sanaa katika Chuo cha ‘Fort Hare.’

Katika maisha yake kiongozi huyo shujaa alipitia hatua mbalimbali wakati wa serikali ya Mandela ikiwemo kushiriki migomo ya wanafunzi na baadaye kufukuzwa chuo.

Harakati zake hizo za kupinga ubaguzi wa rangi zilipelekea mwaka 1944 ajiunge na Chama cha ANC na kuunda Umoja wa Vijana wa chama hicho (ANCYL).

Katika maisha yake ya ndoa na familia, Mandela alifanikiwa kumuoa mkewe wa kwanza Evelyn Mase  ambaye alikuwa ndugu yake na rafiki na mpigania uhuru mwenzake Walter Sisulu na kufanikiwa kupata watoto watatu, Madiba Thembekile, Makgatho na Makaziwe.

Mandela na mke wake Evelyn waliachana mwaka 1958.

Machi 21, 1960 katika mapambano ya kupinga Serikali ya kibaguzi chini ya Utawala wa Kikaburu, Polisi waliua watu 69 wasio na hatia kwenye mgomo wa Sharpville na kusababisha kutangazwa kwa hali ya hatari nchini humo.

Aprili nane, Vyama vya ANC na PAC vilipigwa marufuku huku Hayati Mandela na wenzake walikamatwa na kushtakiwa kwa uhalifu.

Mandela alifunga ndoa nyingine na Winnie Madikizela. Wawili hao walifanikiwa kupata watoto wawili Zenani na Zindziswa.

Januari 11 mwaka 1962, mwanaharakati huyo aliondoka nchini kwake kwa siri na kuelekea nchi mbalimbali za Afrika Tanzania ikiwemo na Uingereza kwa lengo la kupata uungwaji mkono wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi waliokuwa wakifanyiwa.

Alipokea mafunzo ya kijeshi nchini Morocco na Ethiopia na kurejea nchini Afrika kusini Julai mwaka huo. Alikamatwa na polisi Agosti 5 na kufikishwa Kwa rais wa chama cha ANC, Albert Luthuli ili amuelezee kuhusu safari yake.

Mandela alishtakiwa kwa kuondoka nchi hiyo bila kibali na kuhamasisha wafanyakazi kugoma na kufungwa miaka mitano jela.

Hata baada ya kufungwa miaka mitano, Mandela alifungwa tena miaka 27 jela kwenye visiwa vya Robben, nakuhamishiwa jela la Pollsmoor na Victor Verster kwa makosa ya kusababisha mapinduzi nchini.

Kutokana na shinikizo la ndani na la kimataifa huku pia akihofia vita vya ubaguzi wa rangi rais de Klerk alimuachia Mandela.

Mapambano yake ya kuleta uhuru nchini kwake yalizaa matunda na kumpelekea kuwa rais wa nchini hiyo. Mandela aliapishwa kuwa rais wa Afrika Kusini Mei 10, 1994.

Akiwa anasherehekea miaka 80 ya kuzaliwa, rais Mandela alifunga ndoa na mke wake wa tatu, Gracia Machel mwaka 1998.

Mandela mara baada ya kumaliza awamu yake ya kwanza ya urais mwaka 1999 aliamua alistaafu na kuendelea kutumikia mfuko wake uitwao ‘Nelson Mandela Children’s Fund’ ambao ulianzishwa mwaka 1995.

Pia Nelson Mandela alianzisha Taasisi mbili zilizoitwa ‘Nelson Mandela Foundation’ na ‘The Mandela Rhodes Foundation’

Na tarehe 5 Desemba mwaka 2013, Afrika Kusini na dunia kwa jumla ilimpoteza mtu wa muhimu mno Nelson Mandela.

Nelson Mandela aliaga dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Katika mazishi yake, dunia ilizizima kufuatia wageni kutoka pande zote za dunia kumiminika nchini humo.

Michele Obama mwanasheria aliyekuja kuwa mke wa rais wa Marekani

Michelle Obama ni mwanasheria wa Marekani, mwandishi na ni mke wa aliyekuwa rais wa kwanza mweusi nchini Marekani. 

Michelle Obama alizaliwa Januari 17 mwaka 1964, mjini Chicago kwenye familia ya Fraser Robinson na Marian. Alikuwa na kaka mkubwa, Craig.

Familia hiyo iliishi kwa ukaribu sana, walikuwa wanafanya kila kitu kwa umoja kama kula, kusoma na kucheza pamoja.

Mwanasheria huyo alisoma chuo cha Princeton, alihitimu mwaka 1985 na aliendelea na masoma yake ya sheria katika chuo cha Havard mwaka 1988.  Baada ya kuhitimu alifanya kazi kwenye ofisi ya Chicago law firm.

Michelle alifanya kazi kama mshirika katika tawi la Chicago kwenye kampuni ya masuala ya sheria ya Sidley Austin, katika kitengo cha masoko na mali.

Mwaka 1989 alikutana na Barack Obama, ambaye Michelle alikuwa msimamizi wake katika kazi. Wawili hao walipendana na kuanza uhusiano.

Baada ya miaka miwili ya uhusiano wao, Barack alifunga ndoa na Michelle katika kanisa la ‘Trinity United Church of Christ’ oktoba 3, mwaka 1992.

Malia ndiye binti wa kwanza wa wanandoa hao, aliyezaliwa mwaka 1998 na mwaka 2001 walifanikiwa kupata binti mwingine aitwaye, Sasha.

Mwanamama huyo aliacha sheria ya Ushirika, mwaka 1991 na kuendelea kufanya kazi kama msaidizi wa Meya, Richard Daley katika kutoa huduma kwa Umma.

Alijiunga na chuo Kikuu cha Chicago kama msaidizi wa kutoa huduma kwa wanafunzi, huku akiendeleza progamu yake ya kwanza ya huduma kwa jamii.

Mei 2005, Michelle aliteuliwa kuwa Makamu wa rais katika masuala ya jamii na nje kwenye Chuo cha Chicago Medical Center.

Barack Obama alichaguliwa kama Seneta wa Marekani mji wa Illinois, Novemba. Mwaka 2007, Michelle pamoja na mumewe Obama walifanya kampeni za kugombea urais.

Novemba 8, mwaka 2008, Obama alishinda na kuwa rais wa 44 wa nchi ya Marekani. Aliapishwa Januari 20, mwaka 2009.

Obama alishinda urais wa awamu ya pili mwaka 2012 akiwa amesaidiwa na mkewe Michelle katika kampeni za urais.

Michelle alitoa kitabu kama sehemu ya lengo lake la kukuza afya ya chakula. Kitabu hicho kimepewa jina la “American Grown: The Story of the White House Kitchen Garden and Gardens Across America (2012)”.

Michelle alichunguza uzoefu wake wa kutengeneza bustani ya mboga za majani pamoja na bustani za jamii mahali pengine.

Aliiambia Reuters kwamba anaona kitabu hicho kama fursa ya kuwasaidia wasomaji kuelewa "wapi chakula chao kinatoka" na "kuzungumza juu ya kazi tunayofanya kuhusu ubwenyenye wa watoto na afya zao.

Baada ya kumaliza kipindi chake cha pili kama rais, Michelle na Obama waligundua kuwa kuhama kutoka Chicago na kwenda Washington D.C. itasaida familia yao.

Wazazi hao wawili wanataka kuwalinda watoto wao na kuwalewa katika mazingira ya kawaida, kwasababu walizoea kuishi maisha ya kulindwa.

Bill Gate tajiri aliyekatisha shule kufuata ndoto zake

Kwa kawaida watu wengi duniani wanaimani kwamba mtu anapoacha shule basi maisha yake ndiyo yanakuwa yameharibika.

Lakini Imani hiyo inaonekana siyo sahihi pale unapomzungumzia tajiri maarufu duniani Bill Gates.

Tajiri huyu aliyezaliwa Oktoba 28 mwaka 1955 katika familia ya William Henry Gates III na Mary Maxwell, Seattle Washington. Bill Gates alilelewa katika familia yenye uwezo wa kiasi pamoja na dada zake wawili; Kristianne ambaye ni mkubwa kwake na mdogo wake Libby.

Familia ya Gates ilikuwa inaishi kwa ukarimu na ukaribu zaidi, watoto wote watatu walihimizwa kuwa watu wa ushindani na wenye kupigania kilicho bora.

Bill alionyesha dalili za mwanzo kuwa na ushindani wakati akiratibu michezo ya kukimbia ya kifamilia katika majira ya kiangazi.

Akiwa na umri wa miaka kati ya 11 au 12, wazazi wake Bill walianza kuwa na wasiwasi juu ya tabia yake. Alikuwa akifanya vizuri shuleni, lakini alionekana kuchoka na kuacha mara kwa mara kitendo kilichowatia hofu wazazi wake.

Wazazi wake walikuwa wanaimani kubwa kwenye elimu ya Umma, Bill alipokuwa na umri wa miaka kumi na tatu, wazazi wake walimuandikisha katika Shule ya Lakeside, Seattle na katika shule hiyo Bill Gate alifaulu takribani masomo yote yakiwemo Hesabu, sayansi, uigizaji na kiingereza.

Tajiri huyo alikutana na Paul Allen katika Shule ya Lakeside, ambaye alikuwa amempita Bill kiumri kwa miaka miwili.  Wawili hao wakaanza urafiki wa haraka na pia wote walijikuta ni wenye shauku juu ya masuala ya tarakinishi (computer)

Mwaka 1970, Bill akiwa na umri wa miaka kumi na tano alianzisha biashara na rafiki yake, Paul Allen. Walizindua “Traf-o-Data,” progamu ya tarakinishi (computer) inayohusu uangalizi wa trafiki huko Seattle, walifanikiwa kupata Dola za Marekani 20,000 kwa jitihada zao.

Gates alitaka kuanzisha kampuni yake ila wazazi wake walimtaka amalize shule na kwenda chuo ambapo walitumai ya kuwa atakuja kufanya kazi kama mwanasheria, alijiunga na chuo cha Havard akiwa anasomea sheria.

Mtaalamu huyo wa ‘Microsoft’ alikuwa bado anawasiliana na rafiki yake Paul Allen, ambaye alisoma Chuo kikuu cha Washington kwa miaka miwili, na kuacha shule na kuhamia Boston, Massachusetts na kuanza kazi Honeywell.

Mwaka 1975, Gates na Allen waliunda ushirikiano wao na kuuita “Micro-Soft.”

Mwaka 1976, Bill Gates alianzisha Microsoft na kuingia mkataba na MITS (Micro Instrumentation and Telemetry Systems) Microsoft walifanya kazi kwa bidii  ya kuuza mfumo wa uendeshaji katika kampuni nyingine. Hatimaye ‘Microsoft’ walipata nafasi ya utengenezaji wa progamu.

Bill Gates alimuoa Melinda Ann French mwaka 1994 na walifanikiwa kupata watoto watatu ambao ni Jennifer (1996), Rory (1999) na Phoebe (2002)

Katika harakati zao za kimaisha Bill Gates na mke wake Melinda Gates walianzisha Taasisi inayoitwa “Bill&Melinda Foundation”

Gates alipata msaada kutoka kwa mwekezaji, Warren Buffet ambae alichangia Dola bilioni 17 kupitia taasisi hiyo.

Inakadiriwa kwamba taasisi ya Gates na mkewe Melinda imechangia msaada wa Dola za kimarekani bilioni 28 ikiwemo Dola bilioni nane ili kuboresha afya za watu mbalimbali ulimwenguni.

Katika mahojiano yake na gazeti la Daily Telegraph, Gates alisema licha ya kuwa na fedha nyingi ataiachia familia yake asilimia ndogo ya utajiri  wake  huku fedha nyingine akizitoa kwa watu wengine.

 

Madoma : Upendo hushinda yote

Mwanamuzi wa siku nyingi na mwenye jina kubwa katika muziki wa Pop, Madonna, Jumanne Julai 11 alifungua rasmi Hospitali ya kisasa ya watoto nchini Malawi  huku akipokea pongezi za kipekee kutoka kwa Serikali na watu wa Malawi kwa jumla yao.

Mwanamuziki mwenye mapenzi ya kujitoa kwaajili ya wengine, amekuwa na uhusiano wa karibu na  nchi hiyo iliyopo kusini mwa Afrika na tayari amekwisha asili watoto wane kutoka nchini humo.

Kituo hicho cha kissasa ni miongoni mwa vituo bora duniani na kimejengwa kwa jitihada zake za kuchangia nchi hiyo. Kitakuwa ni kituo cha kwanza nchini Malawi kufanya upasuaji kwa watoto sanjari na kuwepo kwa chumba cha kulaza wale mahututi (ICU).  Hospitali hiyo imebeba jina la ‘Mercy James Institute for Paediatric Surgery and Intensive Care’.

Akizungumzia sababu ya kuiita jina hilo, Madona amesema, wakati alipomuasili Mercy alipata vikwazo na kukodi mawakili walipambana mahakani bila kukata tamaa, na alimpigania Mercy na kushinda. “ Tumepigania hii hospitali na tukashinda.Upendo hushinda yote.”

Rais wa Malawi, Peter Mutharika alimwagia sifa mwanamama huyo mwenye miaka 58 kwa kumwelezea kuwa ana “ Alama ya roho ya umama”  wakati wa kuifungua rasmi Hospitali hiyo ya watoto aliyoipa jina la binti yake aliyemuasili kutoka nchi hiyo Mercy James.

“Tutahakikisha kuwa siyo tu inakuwa hospitali ya kipekee duniani kwaajili ya watoto, lakini pia kituo bora cha kujifunzia.  Hii ni maalum kwaajili ya uponyaji kama ilivyo kwaajili ya kuwezesha,” alisema Madonna wakati anafungua rasmi hospitali hiyo.

Madonna alianzisha jitihada za taasisi isiyo ya kiserikali ya kuchangisha fedha nchini Malawi mwaka 2006 kwa lengo la kusaidia kutoa afya na elimu hususan kwa watoto wa kike. Michango ya taasisi hiyo imesaidia kujengwa kwa shule kumi nchini Malawi, kwa mujibu wa tovuti yao.

Hata hivyo alikosoa mfumo wa sharia na haki nchini Malawi ambao ulimpa wakati mgumu  alipofika kuasili binti mapacha mapema mwaka huu.  Alielezea matukio hayo kama vita alivyopigana na kushindana kuongeza kuwa Upendo umeshinda yote.

Mwanamuziki huyo mpaka sasa ameshaasili watoto wanne akiwemo, David Banda na Mercy James kati ya mwaka 2006 na 2009  ha hivi karibuni aliwaasili watoto mapacha wa kike Esther na Stella Mwale. Yeye binafsi anao watoto wawili Lourdes na Rocco,kutoka katika uhusiano wake wa awali.

Katika tukio hilo, Mercy  James aliyepokelewa kwa makofi mengi kutoka kwa umati uliojumuika hapo alisema “Watoto wengi wanakwenda kuokole maisha yao. Asante mama, wewe ni bomu. Haikuwa vita rahisi.”

Akizungumza Madona kwa hisia alisema, “Jaji wa kesi  alinikatalia kwa sababu nikuwa nimetoka kupewa talaka “.

Waziri wa Afya,  Peter Kumpalume amesema,  hospitali hiyo inakwenda kusaidia kuokoa maisha ya vichanga wa nchi hiyo ambayo bado inakabiliwa na tatizo la vifo vya watoto ambavyo idadi yake bado iko juu.

“Kwa Upande wetu tutakamilisha uwepo wa vifaa, na kuwaleta madaktari na dawa,” Kumpalume aliwaeleza Reuters.

Mpaka sasa idadi ya vifo vya watoto wachanga wakati wa kuzaliwa nchini Malawi inadaiwa kupungua kwani kati ya watoto 1000  hupatikana vifo 42 kwa mwaka  2016 kutoka vifo 135 katika takwimu za mwaka 1992, kwa mujibu wa takwimu za Serikali.

Celine Dion: Kutoka bendi ya familia hadi kufikia milionea

Ni Celine Dion aliyezaliwa Machi 30, mwaka 1968 huko katika mji wa Charlemagne Quecbec nchini Canada, akiwa mtoto wa kumi na nne kuzaliwa katika familia ya Adhemar na Therese Dion.

Alilelewa katika familia ya muziki na wazazi wake waliunda kundi la muziki lililoitwa “Dion’s Family”

Celine akiwa na miaka kumi na miwili alirekodi kipande cha wimbo aliouandika pamoja na mama yake na kumpelekea meneja na mtayarishaji, Rene Angelil, ambaye baada ya kuusikiliza  alimkaribisha Dion kuimba mbele yake na bila kuchelewa  Angelil alimsainisha Celine mara moja kwa sharti kwamba atamsimamia binti huyo mwenye kipaji katika safari yake ya muziki.

Meneja huyo baada ya makubaliano hayo, aliweka rehani nyumba yake ili aweze kufadhili albamu yake ya kwanza iliyoitwa La Voix du bon Dieu (Sauti ya Mungu).

Nyota huyo alipokuwa na miaka kumi na minane alikuwa amekwisha rekodi albamu tisa kwa lugha ya Kifaransa na kushinda tuzo nyingi za Felix na Juno  ( sawa na tuzo ya Grammy, nchini Canada).

Mwaka 1998 Dion alishinda mashindano ya Eurovision huko Dublin, Ireland, Mashariki ya Kati, Australia na Japan.

Mwaka 1990 Dion alirekodi albamu yake ya kwanza na Kampuni ya Unison kwa lugha ya Kiingereza. Albamu hiyo iliuza nakala zaidi ya milioni moja duniani kote.

 Mafanikio halisi ya Dion katika ustadi wa muziki wa pop yalikuja mwaka 1992, wakati aliandika mandhari ya Disney katika filamu ya “Beauty and the Beast” na Peabo Bryson. Wimbo ("Beauty and the Beast") ulishika namba 9 kwenye “Billboard Hot 100” na kushinda Tuzo za Grammy na Academy. Alitumia nyimbo hiyo katika albamu yake ya pili ya lugha ya Kiingereza, Celine Dion, ambayo ilikuwa rekodi yake ya dhahabu ya kwanza nchini Marekani na kuuza nakala zaidi ya milioni 12 kimataifa.

Mwaka 1994, Dion alifunga pingu za maisha na Angelil ambaye alimzidi miaka ishirini na sita.

Kabla ya kuwa na uhusiano uliozaa ndoa, Angelil  alikuwa na mke ambaye ni wa pili lakini walitalikiana katika miaka ya 1980.

Ndoa ya wawili hao ilifungwa katika mji wa Montreal’s Notre Dame Basilica katika sherehe iliyo sheherekewa nchi nzima ya Canada.

Mwishoni mwa mwaka 1998, Celine Dion alishinda tuzo sita katika tuzo za muziki za Billboard, ikiwemo ya mwanamuziki bora wa mwaka na albamu ya mwaka “Let’s Talk About Love”

Katika miezi ya mwanzoni mwa mwaka 2000, Dion alitangaza kwamba anasitisha shughuli za kimuziki na kuamua kuiangalia kwa karibu familia yake.

 Yeye na Angelil walikuwa wakijaribu kupata watoto kwa miaka mingi, na hatimaye waliamua kutumia njia ya kupandikiza. Mnamo Mei 2000, Dion alifanyiwa upasuaji mdogo katika kliniki ya uzazi katika mji wa New York ili kuimarisha uwezekano wa kupata ujauzito.

Hatimaye jitihada zake zilizaa matunda na mnamo tarehe 25 Januari 2001, Dion alipata mtoto wa kiume aliyepewa jina la Rene-Charles.

Katika mahojiano baada ya kumpata mtoto wake wa kwanza, Dion alitoa siri ya kuhifadhi yai jingine katika kliniki ya uzazi na alitamani siku moja kumpatia mwanae huyo ndugu yake.

Mnamo Oktoba 23, 2010, akiwa na umri wa miaka 42, Dion alizaa wajifungua watoto mapacha wa kiume.

 Hata hivyo  muda wote wa mapenzi ya wawili hao, ulikuwa na  tamu na chungu kwani mnamo mwaka 1999 Angelil  aligundulika kuwa na saratani ya ngozi uliomtesa kwa miaka mingi.

Baada ya mapumziko ya miaka miwili, nyota huyo alirejea na wimbo wake “A New Day Has Come,” ambayo ilishika nafasi ya juu zaidi ya nchi kumi na saba.

Gazeti la Forbes liliripoti mwezi Juni 2009 kwamba mwimbaji huyo alipata wastani wa dola milioni 100 mwaka 2008, na kumfanya kuwa mwanamuziki wa pili wa katika orodha ya juu la gazeti, baada ya Madonna.

2014 Agosti, Dion alisitisha maonyesho yake yaliyopangwa kufanyika mwezi Machi mwaka 2015 ili aweze kumuhudumia mume wake aliyekuwa na umri wa miaka  72 aliyekuwa akisumbuliwa na saratani ya koo pamoja na watoto wake.

Tarehe 14 ya mwaka 2016, mume wa Celine, Angelil alifariki dunia akiwa na miaka 73 nyumbani kwake Las Vegas.

Angelil alimuacha mkewe Dion na watoto wake Rene-Charles (14), mapacha Nelson na Eddy (5), na mtoto wake Patrick kutoka katika ndoa yake ya kwanza na Denise Duquette, Anne-Marie pamoja na Jean Pierre kutoka katika ndoa yake ya pili na Anne Renee.

 

Cristiano Ronald atarajia mtoto mwingine mwezi Oktoba.

 

Nyota wa Soka duniani Cristiano Ronaldo ambaye hivi karibuni aliwapokea watoto wake mapacha kutoka kwa mama wa kukodi (surrogate mother) anatarajiwa kuongeza familia hiyo kufuatia mpenzi wake, Georgina Rodriguez kudaiwa kuwa na mimba ya miezi mitano.

Nyota huyo alionekana na mchumba wake huyo mwenye umri wa miaka 23, katika safari ya kifamilia, Ibiza nchini Hispania alhamisi usiku.

Gazeti la “The Sun” linadai kuwa Georgina na Ronaldo wanatarajia kupokea mtoto wao wa kike mwezi Oktoba.

Georgina alimvutia mwananyota huyo katika sherehe ya “Dolce & Gabbana”

Walianza uhusiano wa siri kwa miezi michache kabla hawajatangaza uhusiano wao hadharani.

Wachumba hao walionekana hadharani mwanzoni wa mwaka wakihudhuria tuzo za FIFA za Soka huko Zurich.

Cristiano Ronaldo waliwatambulisha watoto wake mapacha kwa kaka yao mkubwa Cristiano Ronaldo Jr Jumanne katika likizo ya kifamilia.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 32 alipiga picha ya yeye na mtoto wake wa kwanza wa kiume wakiwa wamewashika mapacha hao wanaojulikana kwa majina ya “Mateo na Eva”, na kurusha katika ukurasa wake wa Instragam.

Mwanasoka huyo ambaye alikatishwa tamaa na matokeo ya mashindano ya kombe la mabara yaliyofanyika nchini Urusi, alifarijika baada ya kurudi nyumbani na kuwaona watoto wake hao mapacha kwa mara ya kwanza.

Ronaldo, ambaye amefunga mabao 285 katika michezo 241 ya Real Madrid, hakuweza kukutana na kijana na binti yake kwa sababu za soka lakini hatimaye aliwaona watoto hao kwa mara ya kwanza siku moja baada ya kutolewa katika michuano hiyo.